Jeshi lasambaza mashushushu

22Jun 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Jeshi lasambaza mashushushu

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amesema jeshi limesambaza maofisa wake kutoka idara ya intelijensia kutokana na kuwapo kwa taarifa za tishio la kufanyika kwa matukio ya kigaidi nchini.

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro.

Hata hivyo, IGP Sirro amesema taarifa walizonazo ni kwamba hadi sasa, Tanzania haina tishio la kufanyika kwa matukio ya kigaidi, lakini katika kuchukua tahadhari, tayari jeshi limeshapanga watu wake maeneo mbalimbali.

IGP Sirro alitoa kauli hiyo juzi baada ya Ubalozi wa Marekani nchini kutoa taarifa katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter ukitahadharisha na kutoa angalizo la kiusalama ukidai kuna uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam.

"Jeshi la Polisi tayari limepita kwenye hoteli mbalimbali na maeneo ya biashara na ili kuzungumza nao, tumepanga watu wetu maeneo mbalimbali, siwezi kuyasema, kuhakikisha kwamba kama likitaka kutokea, tutahakikisha tunalizuia, kama litatokea kwa bahati mbaya, tutahakikisha wahusika tunawapata.

Alisema Jeshi la Polisi huwa linapokea taarifa zote bila kujali ni ndogo kwa kiasi gani na kuzifanyika kazi.

Alisema taarifa ya UbaloziĀ  wa Marekani ilitakiwa ipitie kwanza Jeshi la Polisi ili kuona ukweli wa jambo lenyewe kabla ya kutangazwa kwa umma.

"Kuna haya matishio ambayo toka tumeyapata si muda mrefu, lakini tumejipanga vizuri, niwahakikishie Watanzania tuna timu zetu za kutosha kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, tupo vizuri.

"Haya mambo mengine ambayo yameonekana kwenye mitandao, ni taarifa ambayo Jeshi la Polisi linazifanyia kazi, hata kama ni ndogo kiasi gani, tunazifanyia kazi," IPG Sirro alisema.

Aliongeza kuwa ndani ya jeshi hilo wapo wanaopata mafunzo kupitia ubalozi huo na wamepanga kuonana nao na kufanya mazungumzo ili waone taarifa iliyotolewa ikoje na kuifanyia kazi.

"Tanzania ipo vizuri sana, watu wetu wa intelijensia wapo vizuri, operesheni na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vipo vizuri, siku zote lazima tukae na tahadhari kwa sababu nchi yetu siyo kisiwa, ukiona inatokea nchi nyingine na kwetu inaweza kutokea, kikubwa ni ushirikiano, ukiona jambo halipo vizuri ambalo linatia shaka tupeni tuifanyie kazi," alisema.

Juzi, serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ulimwita Kaimu Balozi wa Marekani nchini ili kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa yao.

Mwaka 1998, ikiwa ni takriban miaka 21 sasa, wapiganaji wa Jihadi walishambulia kwa pamoja Balozi za Marekani za Kenya na Tanzania.

Agosti 7, mwaka huo, saa 4:30 asubuhi, wakati magaidi wawili walilipua lori moja lililokuwa limejaa mabomu mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Nairobi Kenya. Dakika tisa baadaye, bomu lingine lililipuka katika Ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam.

Takriban watu 242 waliuawa katika mashambulizi hayo yalioharibu kwa kiwango kikubwa ofisi za balozi hizo za Marekani na kusababisha kuporomoka kwa nyumba zilizokuwa karibu.

Habari Kubwa