JKCI yaokoa bil. 3/- kila mwaka

03Aug 2017
Salome Kitomari
Nipashe
JKCI yaokoa bil. 3/- kila mwaka

 TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imefanikisha kupunguza wagonjwa wanaotibiwa nje kwa matatizo ya moyo kutoka 156 mwaka 2014/15 hadi 31 mwaka 2016, hivyo kuokoa zaidi ya Sh. bilioni 3.2 zilizokuwa zikitumika kila mwaka.

Gharama za mtu mmoja kupata matibabu ya moyo nje ya nchi ni wastani wa Sh. milioni 27 huku nchini upasuaji wa kufungua kifua ni Sh. milioni 15, na matibabu mengine yakianzia Sh. 300,000 kutegemea na tatizo la mhusika.

Mwaka juzi serikali ilipeleka watu 156 nje kwa matibabu ya moyo zilitumika Sh. bilioni 4.2 ukiwa ni wastani wa Sh. milioni 27 kwa kila mmoja, lakini tangu kuanza kazi kwa taasisi hiyo zimetumika Sh. milioni 837.

Ofisa Mawasiliano wa JKCI, Anna Nkinda, aliieleza Nipashe kuwa kutokana na huduma hiyo kutolewa nchini, mwaka jana waliokoa zaidi ya Sh. bilioni 2.6 kwa wagonjwa waliotakiwa kupelekwa nje.

Alisema mwaka 2016 wagonjwa waliolazwa ni 2,390, na hadi Juni mwaka huu wamefikia 1,840 na kati yao, 17 wamepelekwa nje.

Alisema mwaka 2016 upasuaji ulifanyika kwa watu 393, huku idadi ya vifo ikiwa ni chini ya asilimia 7, asilimia 4 ikiwa ni upasuaji wa kufungua kifua, asilimia moja ni bila kufungua kifua na wengine kabla ya kupata huduma hizo.

“Uzoefu unaonyesha wagonjwa wengi wanafikishwa hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho, ni vyema kukawa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kujijua,” alisema.

Kwa mujibu wa Nkinda, mwaka jana walifanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973 na kati yao 620 walipatiwa matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua kwa kupitishwa mishipa ya damu kwa kutumia mtambo maalum huku upasuaji ulifanyika kwa wagonjwa 393.

“Miaka ya nyuma upasuaji wa mogonjwa ya moyo wa kufungua kifua na bila kufungua ulifanyika nje ya nchi na kusababisha serikali kutumia fedha nyingi kuwapeleka India, lakini kwa sasa tunatoa huduma nchini,” alisema.

Alibainisha mambo yanayochangia ongezeko la magonjwa ya moyo ni mfumo wa maisha, kutokufanya mazoezi na watu kutumia muda mwingi kwenye magari pamoja na ofisini.

Nkinda alisema mwaka 2017, taasisi imejipanga kufanya upasuaji wa kupasua kifua kwa wagonjwa 700 na bila kufungua kifua 1,000 lengo ni kuhakikisha matatizo ya moyo yanapungua.

“Tumejipanga kutoa elimu kwa Watanzania kupitia vyombo vya habari, pia moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kwenda shuleni kwa kuwa magonjwa mengi ya moyo yanapatikana katika umri mdogo,” alisema.

Habari Kubwa