JKT waingia barabarani kufanya usafi

01Aug 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
JKT waingia barabarani kufanya usafi

SIKU mbili baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda kuagiza usafi wa mazingira kwa kila mkazi wa mkoa huo kwa ajili ya maandalizi ya kupokea wageni watakaohudhuria mkutano wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),limeanza kutekeleza agizo hilo.

Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa, wakifanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam jana, kuelekea Mkutano wa SADC unaotarajiwa kufanyika, mapema mwezi huu. PICHA: JOHN BADI

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa jiji hilo wamekosoa hatua za kushurutishwa kufanya usafi kwa kusubiri ujio wa wageni badala ya kuwa utaratibu endelevu.

Jana Nipashe ilishuhudia vijana wa JKT katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa wanasimamiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakitekeleza agizo hilo kwa vitendo katika maeneo ya Mwenge, Msasani Namanga na Mikocheni.

Mwajuma Hassan mkazi wa Mwenge alisema kazi ya kufanya usafi ni jambo jema ingawa serikali ilitakiwa kujiandaa mapema kwa kuhakikisha maeneo yote ya jiji yana vifaa vya kuhifadhia taka na viongozi wenye dhamana wanasimamia kikamilifu.

"Tunaweza kusema serikali inafanya vizuri kuhamasisha wananchi kufanya usafi, lakini usimamizi kwenye jiji usiwe kwa ajili ya matukio kama hili, bali ufanyike wakati wote. Badala ya kutumia nguvu kazi ya JKT kusafisha jiji ambalo lingetakiwa kusafishwa na wananchi wenyewe na kuliacha lifanye shughuli za kujenga taifa," alisema Mwajuma.

 

Alisema wananchi wanapaswa kuzingatia kanuni za usafi kuanzia nyumbani, mitaani na maeneo yote ya jiji na kuhakikisha maeneo yote ya bustani yanayotunzwa wakati wote badala ya kuachwa.

Naye Omary Kazimoto Mkazi wa Tabata Magengeni, alisema lengo la mkuu wa mkoa huo ni nzuri isipokuwa, mpango mkakati wa utekelezaji wake siyo sahihi kwa kuwa ulitakiwa kuwa mpango endelevu.

Alisema yalitakiwa yafanyike maandalizi ya muda mrefu badala ya kutumia nguvu kwa sababu jiji hilo lina mkanganyiko wa watu wa daraja la chini wanaoishi katika mazingira ya uchafu kulingana na utendaji wao wa kazi.

"Mfano wa shughuli za mmachinga wa Kariakoo ambaye anashinda juani kutwa nzima na jasho linamtoka wakati wote anaweza vipi kuwa katika hali ya utanashati wakati wote," Omary alihoji.

Makonda alitangaza operesheni hiyo mapema Jumatatu wakati akizindua kampeni ya usafi wa jiji la Dar es Salaam ikiwa ni moja ya maandalizi ya mkutano wa 39 wa SADC unaotarajiwa kufanyika hapa nchini Agosti 17 na 18, mwaka huu.

"Tabia ya kuja mjini hujafua, hujaoga usitutie aibu kama umezoea kuja mjini hujaoga wala kufua nguo baki nyumbani walau huu mwezi wa nane uishe, tunataka sio usafi tu wa mazingira, usafi pia wa wananchi wetu, watu wamejaa chawa tu hapa," Makonda alisema.

Aliwaonya  wananchi wenye tabia ya kutupa taka ovyo wakiwa kwenye vyombo vya usafiri hususani daladala kuwa watashushwa na kupewa adhabu kali ikiwa ni pamoja na kufanyishwa usafi.

Pia, Makonda ameagiza mtu yeyote mwenye gari atakayetupa takataka barabarani asitozwe faini badala yake apewe eneo la kufanya usafi. Alisema baadhi ya watu hao wana jeuri ya fedha, hivyo kwao faini siyo adhabu.

Mwenyekiti wa kamati ya usafi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, alisema shughuli ya usafi itafanywa na vijana 130 JKT na mgambo 300 katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Habari Kubwa