Joshua Nassari avuliwa ubunge

15Mar 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Joshua Nassari avuliwa ubunge

BUNGE limetangaza kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, amepoteza sifa za kuwa Mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jioni na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai, amemwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, kuwaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki liko wazi.

Nipashe ilipomtafuta Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Athuman Kihamia, kuhusu barua hiyo kama wameipokea, alisema: “Ni kweli tumeipokea barua hiyo leo (jana) kutoka bungeni na tumeanza mchakato kumpata mbunge mpya.”

Dk. Kihamia alisema sheria inasema mwisho wa kuzibwa nafasi ni miezi 12 kabla ya Bunge la mwisho linalotarajia kuvunjwa Julai, mwakani.

Taarifa ya Bunge ilibainisha kuwa jimbo la Arumeru Mashariki linaloongozwa na Nassari kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) liko wazi kutokana na mbunge huyo kupoteza sifa.

Pia taarifa hiyo ilisema Nassari amepoteza sifa hiyo kwa kutohudhuria mfululizo mikutano ambayo ni mkutano wa 12 wa Septemba 4 hadi 14, mwaka jana, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16 na mkutano mwaka 2018.

Pia taarifa hiyo ilisema Nassari hakuhudhuria mkutano wa 14 uliofanyika kuanzia Januari 29 hadi Februari 9, mwaka huu.

“Uamuzi huu wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71 (1) (c). Ibara hii inaeleza kuwa, ‘Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ibara hiyo imefafanua katika Kanuni ya 146 (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari, 2016.

“Kanuni hiyo inaeleza kuwa, ‘Kuhudhuria vikao vya Bunge na Kamati zake ni wajibu wa kwanza wa Mbunge. Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataiarifu NEC,” ilisema.

Aidha, taarifa hiyo ilisema tume ya uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Arumeru Mashariki.

Habari Kubwa