JPM aongoza maelfu kumuaga Dk. Mengi

08May 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
JPM aongoza maelfu kumuaga Dk. Mengi

RAIS John Magufuli jana alishindwa kujizuia na kujikuta akijifuta machozi mbele ya jeneza lililokuwa na mwili wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ambaye aliagwa jana jijini Dar es Salaam.

Rais John Magufuli akiongoza maelfu ya Watanzania kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam jana.

Dk. Mengi alifariki dunia usiku wa kuamkia alhamis iliyopita nchini Dubai, Falme za Kiarabu.

Shughuli za kuaga mwili wa marehemu Dk. Mengi ambao ulirejeshwa nchini juzi, zilizofanyika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, zilihudhuriwa na Rais Magufuli, mawaziri, wabunge, mabalozi wa nchi mbalimbali na viongozi wastaafu akiwamo Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.

Wamo pia Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilali; mawaziri wakuu wastafu John Malecela, Cleopa Msuya na Mizengo Pinda pamoja na Spika mstaafu, Anne Makinda.

 

Viongozi wengine waliohudhuria ni kutoka taasisi mbalimbali za serikali, sekta binafsi, taasisi za kitaifa na kimataifa.

Shughuli za kuaga mwili huo zilianza saa 5:15 asubuhi ambapo ziliongozwa na Rais Magufuli ambaye mara baada ya kupita kwenye jeneza hilo alionekana akitoa miwani yake na kufuta machozi.

Baada ya Rais Magufuli kuaga alifuata Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na ndipo viongozi wengine wa serikali na wastaafu nao walipata nafasi hiyo.

Wengine ni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi, Mkurugenzi Usalama wa Taifa, Katibu Mwenezi CCM, Humprey Polepole, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Baada ya viongozi wakuu kumaliza kuaga, mwanamuziki wa nyimbo za injili, Joel Lwaga aliimba wimbo sitabaki nilivyo uliowatoa machozi waombolezaji wengi wakiwemo wanafamilia ya marehemu Dk. Mengi.

SALAMU ZA SERIKALI

Akitoa salamu za rambirambi za serikali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema serikali inatoa pole kwa familia, mke wa marehemu, watoto, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wao Dk. Mengi.

"Tunatoa pole kwa wafanyakazi kwa kuondokewa wa kiongozi, sisi tunatambua mchango wake, upendo wa dhati na ukarimu wake aliokuwa nao kwa kipindi chote. Ni dhahiri kifo chake ni pigo kubwa, “alisema.

Alisema serikali, Watanzania na dunia kwa ujumla imepokea kwa simanzi na masikitiko taarifa za kifo cha Dk. Mengi kutokana na ukweli kwamba kifo chake kimekuwa cha ghafla mno.

 

Prof. Kabudi alisema baada ya serikali kupata taarifa kupitia ubalozi mdogo Dubai kwa kushirikiana na familia ulianza maandalizi ya kuuhifadhi na kuusafirisha mwili wa marehemu kuja nchini.

Alisema licha ya muda kuwa mfupi ikizingatiwa siku ya Ijumaa ni ya mapumziko nchini humo, lakini walihakikisha nyaraka za kuusafirisha mwili huo zinapatikana siku hiyo hiyo saa 10 jioni na hatimaye juzi kuuleta Tanzania.

Prof. Kabudi alisema serikali inamshukuru Balozi Nassoro Mbaruku kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha taratibu zinakamilika na mwili huo unarejeshwa nchini mapema.

"Kifo ni fumbo, na fumbo hili alijuaye ni Mungu peke yake, tunamshukuru Mungu kwa kila alichoamua, serikali imeguswa na kifo cha Dk. Mengi ambaye amefanya mengi katika maeneo ya uchumi, gesi, madini, kilimo na afya ametoa ajira, kuboresha mazingira ya biashara, kutoa ajira, amevutia wawekezaji, alichangia kushauri sera za kiuchumi, alikuwa na jawabu ya namna gani ya kuboresha sera zetu," alisema.

Prof Kabudi alisema Dk. Mengi amewezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kwamba serikali itaendelea kumuenzi kwa aliyoyaacha.

"Katika kulifanya hili kwa vitendo hivi karibuni alionyesha nia ya kuwekeza kwenye viwanda tofauti, kiwanda cha dawa, uunganishaji magari, simu, nidhahiri mchango wake ni mkubwa, Watanzania tunaweza kuwekeza nchini tukiwa na nia,"alisema

Alisema serikali inatambua mchango wake, moyo wake wa upendo na ukarimu hususani kwa wanyonge, maskini na watu wenye ulemavu.

Prof Kabudi aliongeza: “Hii ni ishara tosha moyo wa upendo, ukarimu na huruma na kuandaa chakula kwa ajili ya watu wenye ulemavu.”

Alisema Dk. Mengi amepata tuzo mbalimbali duniani, amekuwa mdau mkubwa wa sekta ya mazingira na amehamasisha upandaji wa miti sehemu mbalimbali nchini ikiwamo kuzunguka Mlima Kilimanjaro.

Alisema kitabu chake cha I Can, I Must, I Will ni hazina kwa sababu kinafundisha mengi na aliwataka Watanzania wahamasike kukinunua ili kiwawezeshe kubadilisha hali ya maisha yao.

 

SALAMU ZA TPSF

 

Akitoa salamu za sekta binafsi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte, alisema Mungu amechukua roho yake lakini nyota yake itaendelea kung'aa na kuonyesha njia.

"Tumempoteza mwasisi kiongozi, muongoza njia na mpendwa wetu aliyekuwa na mchango mkubwa kwenye sekta binafsi na uchumi wa nchi," alisema.

 

Alisema baada ya kupata taarifa za kifo chake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, aliwawakilisha kwenda Dubai kushirikiana na serikali na familia kukamilisha taratibu za kuurejesha mwili nyumbani.

Shamte alisema Dk. Mengi alikuwa muumini wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma kwa sababu ndiyo nguzo muhimu kuleta maendeleo ya nchi.

Shamte alisema Dk. Mengi alikuwa nguzo muhimu katika sekta binafsi kwani aliiongoza kwa miongo minne na muda wote mchango wake ulikuwa mkubwa na wenye manufaa kwao.

Aliongeza kuwa Dk. Mengi alitamani nchi iwe na mabilionea wengi kumzidi yeye kwa sababu aliamini hilo linawezekana iwapo watu watafanyakazi na kuamini kwamba wanaweza.

"Jukumu la kutengeneza wajasiriamali ni letu sote kwa kuwajenga watoto kuanzia shule na kuweka mazingira bora, aliamini dhana pana ya uongozi wenye maadili na alithubutu kukemea rushwa hadharani kwa kutaja majina,” alisema Shamte.

Alisema Dk. Mengi alipenda kuwawezesha wananchi kiuchumi ambapo aliamini kwamba kwa utajiri ambao nchi imebarikiwa kuwa nao wananchi wake hawakupaswa kuwa maskini.

Shamte alisema Dk. Mengi aliamini dhana ya uongozi wa kujitolea na alikubali madaraka na kuongoza taasisi nyingine mbali ya kampuni zake.

Alisema Dk. Mengi aliishi maisha yenye unyenyekevu na kujali wasiojiweza na kwamba kitabu alichokiacha ni wosia tosha kwa Watanzania hivyo wanapaswa kukisoma ili kujiongezea maarifa na ujuzi zaidi.

 

BALOZI UFARANSA

 

Naye Balozi wa Ufaransa nchini, Frederick Clavier, alisema Dk. Mengi alikuwa mshauri mzuri na kwamba tangu aje nchini yapo mengi amejifunza kutoka kwake ikiwemo fursa.

SHIVYAWATA

 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye ulemavu (Shivyawata), Ummy Hamis, alisema mara nyingi alikuwa akisimama kumshukuru Dk. Mengi kwa namna alivyoshiba maisha yao.

"Tulipokea kwa mshtuko na tumefadhaika na kuumia sana kwa sababu alikuwa akitetea jamii yetu kiuchumi, utu wetu, kisiasa na kijamii kwa kuamini utu na uzalendo,” alisema.

Pia alisema: "Hakika kwetu alikuwa baba mshauri na mtetezi wetu, alitumia ushawishi wake kuwaita rafiki zake kuunga mkono masuala ya walemavu, alianzisha 'Dk. Reginald Mengi Foundation for Disability' na mwaka jana alianzisha tuzo za I Can ambazo mwaka huu tulipatiwa zawadi mbalimbali.”

 

KAULI YA CCM

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole,

alisema zipo aina mbili za matajiri duniani ambapo ya kwanza ni waliobarikiwa utajiri, wazalendo wa taifa ambao hutumia kusaidia watu na ya pili ni wale waliopata kwa ujanja ujanja na kujinufaisha wenyewe.

Polepole alisema Dk. Mengi alibarikiwa neema ya utajiri na alikuwa mshauri wa uchumi na kila kulipokuwa na mkwamo kati ya serikali na sekta binafsi alishauri namna bora ya kutatua matatizo hayo kabla mambo hayajaharibika.

 

JAMES MBATIA

Mbunge wa Vunjo (NCCR Mageuzi), James Mbatia, alisema amemfahamu Dk. Mengi miaka 28 iliyopita na katika kipindi cha mwaka huu alimshirikisha mambo yake mengi.

Alisema Machi 20, mwaka huu kwenye mazungumzo ofisini kwake, Dk. Mengi alizungumzia maridhiano ya vyama ili uchaguzi ujao usimwage damu na kusisitiza kuwa maisha yapo kwenye ndimi, hivyo zikitumika vizuri Tanzania itakuwa salama.

"Maisha mema ya Dk. Mengi iwe sauti huru na haki na matendo yetu. Mathayo 5:3 inasema heri yao wapatanishi..Nawashauri familia iendeleze pale alipoacha Dk. Mengi ili kazi zake ziendelee kuishi," alisema.

 

UPINZANI

Akisoma salamu za Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kwa niaba ya kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema hana maneno ya kutosha kufikisha ujumbe wake kwa niaba ya wana Hai, lakini alimshukuru Mungu kwa maisha aliyompatia duniani na kuwa baraka kwa wengi aliowajua na asiowajua.

 

RC MAKONDA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema wamempoteza baba, rafiki, mwajiri ambaye alikuwa mkombozi kwa watu wengi na aliwaomba radhi wananchi kwa kufunga barabara juzi ili kutoa heshima kwa Dk. Mengi kwa mema aliyoyafanya nchini.

Alisema anamtambua Dk. Mengi kama mwamba wa kaskazini, sikio kwa waliokata tamaa na ambaye alikuwa tayari kuwa mfano kwa wanyonge na maskini na amepigana vita vizuri.

 

“Mchaga anakubali kumpa mali mtu hata asiyekuwa na ndoto, matumaini siyo jambo rahisi, kwa hili nazidi kusema siyo tu tumepoteza mchaga bora katika wachaga wote, bali tumepoteza Mtanzania aliyekuwa zaidi ya kabila lake,” alisema Makonda.

Alisema mwaka jana Dk. Mengi alimwambia aandae tukio kwa ajili ya chakula na viongozi wa dini na kutokana na serikali kutokuwa na bajeti ya tukio hilo ilimbidi akope fedha sehemu mbalimbali ikiwamo Sh. milioni 50 kwa rafiki wa mke wake na baadaye Dk. Mengi alilipa deni lote la Sh. milioni 147.

 

"Nilipata tabu nikaanza mandalizi na kamati niliyounda ilinihoji fedha tutatoa wapi, lakini nami nikawaambia waendelee na maandalizi na ilinibidi nikope kwa rafiki wa mke wangu Sh. milioni 50 kwa ajili ya malipo ya awali, baada ya shughuli kuisha Dk. Mengi alirejea nchini nikamwambia nina deni akaniambia kwa sababu umesikia sauti ya Mungu fedha zipo, akalipa deni lote Sh. milioni 147," alisema.

CLOUDS MEDIA GROUP

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group (CMG), Joseph Kusaga, alisema licha ya kwamba Dk. Mengi alikuwa anamiliki vyombo vya habari, lakini mara alipokutana naye alikuwa akimshauri namna ya kuviendesha.

Alisema Dk. Mengi amewaongoza katika tasnia ya habari kwa miaka 20 kwa kupigania haki ya uhuru wa vyombo vya habari.

“Binafsi nilimjua Dk. Mengi miaka 26 iliyopita nilikuwa nakwenda nyumbani kwake kupiga disco, akawa anazungumza mambo ya redio, yeye akaanza na mimi nikaendelea kupata mawazo. Mtu anachombo cha habari lakini anakupa mawazo ya kufungua chombo cha habari,” alisema.

Kusaga alirudia maneno ya Dk. Mengi ambayo aliyasema wakati wa msiba wa Ruge Mtahaba kuwa, “Ruge hajafa’ na kueleza kuwa, “Dk. Mengi hajafa”.

 

SALAMU ZA CTI

 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Subash Patel, alisema wamempoteza mshauri mkubwa ambaye alikuwa mwenyekiti aliyetumikia kwa miaka minne CTI.

“Mchango wa Dk. Mengi kwenye jamii ulikuwa mkubwa, utajiri wake aliishi nao kwa msaada, elimu aliyotupa ya kuishi duniani ni kubwa kuliko fedha alizokuwa nazo, tulikuwa marafiki alikuwa mshauri wangu,” alisema.

Patel aliwataka Watanzania wenye utajiri wamuige Dk. Mengi kwa kuwa na moyo wa kutoa na kusaidia wengine.