JPM aagiza mkuu wa shule iliyoungua aachiwe

17Sep 2020
Na Waandishi Wetu
Kagera
Nipashe
JPM aagiza mkuu wa shule iliyoungua aachiwe

RAIS John Magufuli ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kumwachia Mkuu wa Shule ya Msingi Byamungu Islamic, anayeshikiliwa baada ya kutokea kwa ajali ya moto na kuua wanafunzi 10, wengine sita kujeruhiwa.

Kadhalika, ameitaka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kukagua na kuhakikisha shule zote na zinazoanzishwa zinazingatia masuala ya kisheria, lengo likiwa ni kuzuia matukio ya kuungua kwa shule kujirudia.

Alitoa agizo hilo jana mkoani Kagera wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM, waliojitokeza katika viwanja vya Gymkhana kumsikiliza.

“Wakati uchunguzi unaendelea juu ya tukio hilo la kuungua kwa shule, ninaomba mkuu wa shule aachiliwe, nikuombe RPC (Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa) umuachie…alianzisha shule kwa ajili ya watoto wetu kusoma na siyo kuwaunguza. Tukiendelea kumuweka ndani tunamwongezea mateso zaidi,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Kama kuna uzembe ulifanyika basi hata akiwa nje upelelezi unaweza kufanyika na ataweza kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi. Nina imani huyu mkuu wa shule hana roho mbaya ya kuamua kuwachoma wanafunzi,” alisema Rais Magufuli.

Shule ya Msingi Byamungu iliyoko kata ya Itera, wilayani Kyerwa iliteketea kwa moto juzi na kusababisha vifo vya wanafunzi hao.

Kadhalika, Magufuli ambaye anagombea urais kwa awamu ya pili, alielezea mafanikio yaliyopatikana katika Mkoa wa Kagera kwa kipindi cha miaka mitano.

Alisema Mkoa wa Kagera ulikuwa unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo matukio ya ujambazi.

Alisema baadhi ya maeneo wananchi walikuwa wanashindwa kusafiri nyakati za usiku, ikiwamo msitu wa Kisindaga kwenda Karagwe, malori yalikuwa yanatekwa na majambazi.

“Leo hii matukio hayo yameisha na baadhi ya maeneo yamepungua, nivipongeze vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha Kagera na Tanzania kwa ujumla inakuwa salama,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha Tanzania inakuwa salama, serikali iliamua kuyageuza baadhi ya mapori kuwa hifadhi za akiba, kama vile pori la Rumanyika, Burigi-Chato.

Kuhusu utalii, Rais Magufuli alisema serikali ina mkakati wa kuhakikisha ukanda wa Mkoa wa Kagera unakuwa wa utalii kama ulivyo wa Kaskazini.

Alisema: “Sekta ya utalii ndiyo inatengeneza ajira nyingi zaidi. Kwa kipindi cha miaka mitano imetengeneza ajira milioni nne. Mwaka 2019 ilichangia Sh. bilioni 2.6 ikishika nafasi ya pili baada ya sekta ya madini kuongoza kwa kuingiza Dola za Marekani bilioni 2.7.”

Kuhusu elimu, alisema serikali katika kipindi cha miaka mitano imejenga shule za msingi 27 mkoani Kagera, shule za sekondari 28, pamoja na kutoa Sh. bilioni 57.23 kufanikisha elimu bure.

Alisema pia walimu 1,658 wameajiriwa mkoani humo kwa kipindi cha miaka mitano, ujenzi wa madarasa 1,119 pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu 286.

Aliahidi atakapostaafu atahamishia makazi yake mkoani Kagera.

KAULI YA MUFTI

Akizungumzia tukio hilo jana jijini Dar es Salaam, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi, aliagiza wamiliki wa shule nchini waimarishe ulinzi ndani ya shule zao na kuchukua tahadhari za kina na kuhakikisha mifumo ya umeme, uzio na vifaa vya kuzima moto vinakuwapo.

Alisema Baraza Kuu la Waislam linaendelea kusubiri taarifa rasmi ya vyombo vya ulinzi na usalama.

“Baada ya taarifa hii ya moto nilituma ujumbe wa viongozi wa Bakwata Mkoa wa Kagera ukiongozwa na Katibu Mkoa na wenzake ambao walituthibitishia ajali hii ya moto.

“Ninatoa pole kwa mkuu wa shule na wazazi waliopoteza watoto na waliojeruhiwa katika ajali hii, pole kwa Rais Magufuli, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Sheikh wa Mkoa huo na mmiliki wa shule,” alisema.

*Imeandaliwa na Romana Mallya, Frank Maxmillian (DAR), Gwamaka Alipipi na Lilian Lugakingira (BUKOBA)

Habari Kubwa