JPM aagiza uchunguzi wa kina waliobambikwa kesi

19Jul 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
JPM aagiza uchunguzi wa kina waliobambikwa kesi

RAIS John Magufuli ameagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kutembelea magereza yote nchini ili kubaini na kuwaachia huru mahabusi wanaosota rumande kwa kubambikwa kesi.

RAIS John Magufuli.

Alitoa agizo hilo jana wilayani Kongwa mkoani Dodoma alipozungumza na wakazi wa wilaya hiyo ikiwa ni siku tatu tangu afanye ziara ya kushtukiza kwenye Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza.

Akiwa katika gereza hilo, Rais Magufuli alibaini kuwapo kwa changamoto ya msongamano wa wafungwa na mahabusu kunakosababishwa na ubambikaji wa kesi na mahabusi kutofikishwa mahakamani.

Kutokana na ziara hiyo ya Rais Magufuli gerezani huko, juzi mahabusi 200 waliachwa huru ikiwa ni hatua ya utekelezaji uliofanywa na wizara hiyo ikiihusisha Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.

“Walikwenda pale Butimba na kuwasilikiza kwa zaidi ya saa saba, kisha waliwaachia watu 75," Rais Magufuli alisema.

Alibainisha kuwa mahabusi wengine walioachwa huru ni 100 kutoka Bariadi, Mugumu Serengeti (52), Tarime (6), Bunda (24) na Kahama (43).

Rais Magufuli alisema wako mahabusi wamewekwa mahabusu kwa makosa ya kuonewa na wengine kesi zao halisi zingefikishwa mahakamani mapema, wangehukumiwa kifungo cha miezi sita jela lakini wameonewa kwa kukaa rumande kwa zaidi ya miaka minane.

Akifafanua zaidi kuhusu changamoto hiyo, Rais Magufuli alimtolea mfano mahabusi aliyemkuta kwenye Gereza Kuu la Butimba ambaye alikamatwa akiuza mafuta ya magendo, akakamatwa na kuombwa rushwa ya Sh. milioni moja na aliposhindwa kutoa, alijikuta akipelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa kesi ya mauaji.

“Siwezi nikatawala nchi ya machozi, haya yataniumiza, siwezi, watu wanasikitika, wapo kwenye unyonge wa kuonewa,” Rais Magufuli alisema.Kiongozi wa nchi huyo aliwaonya askari polisi wanaowabambika kesi wananchi, akiwataka wawe na hofu ya Mungu.

Rais Magufuli alisema miongoni mwa mahabusi walioachwa huru juzi, ni askari polisi wanane waliokuwa wanatuhumiwa kushiriki katika utoroshaji wa dhahabu na ameagiza warejeshwe kazini.

“Hata kwa kuwaona tu unaweza ukajua kwenye macho yao, DPP amewaachia, nimeamua warudishwe kazini kwa sababu walikuwa wameshafukuzwa,” alisema.

“Lakini liwe fundisho kwa watu wanaopenda 'virushwarushwa', waache kuwapambikiza kesi, siyo kitu kizuri, lazima tumwogope Mungu."Rais Magufuli pia aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Kongwa kwa kutenga eneo kwa ajili ya jeshi kuwa Mkoa wa Dodoma ni makao mkuu ya nchi na suala la kuwa na kambi za jeshi haliepukiki.

Rais Magufuli pia alieleza sababu za kutohamia kwake mkoani Dodoma kwa wakati aliokusudia, akisema ni kutokana na kuugua kwa mama yake."Hata mimi ilikuwa nihamie (Dodoma) lakini bahati mbaya wakati najiandaa kuhama, mama yangu aliugua... kwa hiyo, inabidi nimhudumie, lakini mara nyingi nimekuwa nikija hapa Chamwino, tunataka ndoto hii itimie kwa vitendo," alisema.

Akiwa wilayani Kongwa jana, Rais Magufuli alitoa mchango wa Sh. milioni tano kusaidia ukarabati wa Shule ya Msingi Sagala iliyoezuliwa na kimbunga hivi karibuni.

Rais pia alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha viongozi wa serikali, dini na siasa kuchangia ukarabati huo, akifanikisha kukusanywa zaidi ya Sh. milioni sita, mabati 252 na mifuko ya saruji 300.

Awali, Mbunge wa Kongwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipongeza mafanikio ambayo serikali ya tano imeyapata na kueleza changamoto zinazowakabili wananchi wa Kongwa.

Ndugai aliiomba serikali kuliboresha eneo lililotumiwa kuhifadhi wapigania uhuru wa nchi za Afrika, kujengwa kwa kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) na kukarabatiwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kongwa ili uwe wa akiba.

Habari Kubwa