JPM aagiza vifaa kinga vichunguzwe

22May 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM aagiza vifaa kinga vichunguzwe

RAIS John Magufuli ameagiza vifaa vinavyotolewa kama msaada kwa ajili ya kujikinga na virusi vya corona vipokewe na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na kuchunguzwa kama havina virusi kabla havijatumika.

Aliyasema hayo jana Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, alipowaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni na kuagiza endapo vifaa hivyo vikikutwa na maambukizo ya corona, wahusika washitakiwe kwa jinai ya mauaji.

Rais Magufuli alilifafanua kuwa juzi aliona Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikipokea vifaa vya kujikinga na corona.

“Kama ni kupokea kifaa chochote cha kupambana na corona, lazima kipitie Wizara ya Afya na kifanyiwe uchunguzi, siyo mtu amekaa huko ana kitaasisi chake, tunaomba michango mingine ya watu ya kupambana na corona, kuna mahali fulani walikuwa wanaitisha mradi tukachangeni, hapana.

“Ninaawaomba Wizara ya Afya, Naibu Waziri (Dk. Godwin Mollel) upo hapa, Waziri Ummy, Katibu Mkuu, mkasimamie hili. Mtu yeyote atakayepewa vifaa vya corona, halafu mkapima na kukuta vina corona, huyo mtu apelekwe kwenye kesi ya jinai hata ya mauaji kama wauaji wengine," aliagiza.

Aliwatahadharisha watendaji serikalini kuhusu kile alichokiita 'kupokea pokea', akikumbusha kuwa tayari Waziri Ummy ameshaomba fedha ili barakoa zitengenezwe nchini.

“Tutanunua vifaa ambavyo tunajua vimepimwa kwenye maabara zetu na kujua hiki ni kifaa kweli ninachofaa kwa ajili ya matumizi ya Watanzania,” alisema.

Rais Magufuli alisema ugonjwa wa corona ni vita na katika misaada, huenda wananchi wakapewa barakoa zenye corona.

“Mwenendo wa maambukizo unakwenda vizuri kutokana na hatua tunazozichukua, yapo mengi tunayoyachukua, mengine hatuyatangazi. Vya bure vibaya, ndiyo maana tunaipongeza Wizara ya Afya kwa kazi nzuri iliyofanya chini ya Waziri wake, Ummy Mwalimu,” alisema.

Rais Magufuli aliipongeza wizara hiyo na watendaji wengine kwa kuwa sasa barakoa zinashonwa Tanzania na Jeshi la Wananchi linafanya kazi nzuri, huku Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikishona vazi maalum kwa watoa huduma za afya kujikinga (PPE) kwa gharama nafuu.

“Nilifikiri fedha za mfuko wa Global Fund zitumike kutengeneza vifaa vyetu wenyewe, kwanza zitajenga ajira na kuokoa na zitatumika kwa watu wengi," alisema.

Rais aliwataka Watanzania wachukue tahadhari kubwa kwa sababu maambukizo ya corona nchini yanashuka chini na yanaelekea kuisha.

“Lakini, tusije tukapandikiziwa corona kwa uzembe wetu au kwa uzembe wa mtu yeyote, mtu akitaka kusambaza msaada hatukatai, peleka Wizara ya Afya, pale kuna wataalamu watakichunguza kifaa, mkalisimamie hili, dezo zinaua.

“Tunahitaji misaada na tunawashukuru sana kwa ambao wameamua kutusaidia kwa mfano wanaotusaidia kwenye elimu kama ulivyozungumza Profesa (Waziri wa ELimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako), wafikishie salamu nchi ya Canada, European Union (Nchi za Umoja wa Ulaya) na wengine ambao wanajitolea kutusaidia," alisifu.

AMSIFIA WAZIRI UMMY

Rais Magufuli pia alisema Waziri Ummy anastahili pongezi kutokana na kujituma katika janga hilo la corona, akibainisha kuwa 'amesimama kweli' licha ya kwamba hana taaluma ya udaktari.

“Kuna wakati fulani niliona anasimama peke yake kwenye wizara, yeye siyo daktari wa kusomea, unajiuliza mwanasiasa anasimama peke yake kuzungumzia taaluma ya udaktari, wasaidizi wake wote ni madaktari huoni matokeo, ninakupongeza sana Ummy, ninajua nilikutesa.

“Sitaki kueleza mengi, lakini ni kweli aliteseka kwa sababu kwa siku mara nyingine alikuwa anapigiwa simu zaidi ya mara nane, iwe saa nane iwe saa ngapi, unapokuwa kwenye vita, saa nyingine kubembelezana hapana," alisisitiza.

Rais Magufuli alisema Waziri Ummy alisimamia wizara hiyo kwa ujasiri mkubwa na kumtaka Naibu Waziri mpya, Dk. Mollel aende kumsaidia.

“Kwa mfano Mollel kwenye jimbo lako hospitali ikajengwa na kumalizika halafu usipeleke dawa, hapo kwenye jimbo lako usipeleke madaktari, wewe upo.

“'Message sent' (ujumbe umefika), mshikamano unaanzia nyumbani, unapopewa jukumu lazima utimize wajibu," alisema.

MAGEREZA YABADILIKA

Rais Magufuli pia alisema baada ya kufanya mabadiliko Magereza, Kamishna Jenerali wa Magereza, anafanya kazi na katika kipindi cha miezi mitatu, hajaomba fedha serikalini kwa ajili ya kulisha wafungwa.

“Wale waliokuwapo wa vyeo vyeo waliokuwa wanamsumbua kidogo, akaandika barua huku napo ikacheleweshwa, baadaye nikamwambia Katibu Mkuu Kiongozi shughulikia, ninafikiri umelishughulikia wale mmeshawahamisha, walikuwa wanavuta kamba, makamishna nikasema toa hapo,” alisema.

Alisema Kamishna Jenerali wa Magereza wa sasa amepanda mikorosho, akibainisha kuwa hatua hiyo imemfanya ajiuelize "waliokuwapo hawakuona?"

“Mtu anayekupenda anakueleza, ambaye hakupendi hakuelezi. Nina matumaini makubwa mabalozi watatu mlioteuliwa, mtakwenda kufanya kazi, mmepelekwa nchi ambazo ni mkakati ambazo ni Kenya, Msumbiji, Algeria,” alisema.

Rais pia alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) aliyemwapisha siku hiyo, asiende kustarehe, bali akafanye kazi ili yanayowasumbua wananchi wa kawaida ikiwamo rushwa yakashughulikiwe.

“Nendeni mkafanye kazi kwa sababu kila mmoja alikuwa na nafasi na mkajitathmini mlikosea wapi na mjirekebishe. Nendeni mkachape kazi, hizi ni kazi za watu,” alisema.

Habari Kubwa