JPM aahidi kumaliza rushwa

26Oct 2020
Gwamaka Alipipi
MANYARA
Nipashe
JPM aahidi kumaliza rushwa

MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, amewahakikishia Watanzania kumaliza tatizo la rushwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo na maskini kupata haki zao.

MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli.

Vilevile, ameahidi kuwatetea wananchi waliopokwa ardhi, kinamama waliodhulumiwa hati, pamoja na kumaliza viporo ambavyo hajavitekeleza.

Aliyasema hayo jana wakati akiwa katika Uwanja wa Kwaraa, wilayani Babati mkoani Manyara, wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM waliojitokeza kumsikiliza akiomba kura ya kuchaguliwa kwa mara ya pili kuwa rais.

“Katika kipindi cha miaka mitano tumefanikiwa kupambana na vitendo vya rushwa, wizi pamoja na mali za umma, rushwa ilitapakaa kila idara, tukasema ndani ya miaka mitano lazima tutokomeze,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza:

“Najua bado rushwa haijaisha, sasa naomba miaka mingine mitano nikaitokomeze, nataka watu maskini wapate haki zao, wengine wamedhulumiwa ardhi, kinamama waliopokwa hati zao, nataka hayo yote yakaishe,” alisema.

Aliwataka Watanzania kuwakataa wagombea wanaohubiri na kutaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjike.

Alisema moja ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ni kudumishwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umedumu kwa takribani miaka 56.

Pia, alisema serikali imedumisha na kuitunza amani, ambayo ilijengwa tangu utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na kuhudumisha uhuru.

“Tanzania imekuwa ni kisiwa cha amani kwa mataifa mengi kukimbilia hapa, tumefanikiwa kudumisha amani ambayo iliasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere.”

Alisema kwenye sekta ya afya, serikali imefanikiwa kujenga hospitali za wilaya 99 katika kipindi cha miaka mitano, zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za mkoa 10 pamoja na hospitali za rufani tatu.

Kadhalika, aliwataka Watanzania wakati wa upigaji kura kuwachagua viongozi wanaotunza tunu za nchi, kwamba mwenye sifa hiyo ni yeye (Dk. Magufuli).

Vilevile, alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, CCM kitaibuka na ushindi mkubwa wa kimbunga, kutokana na idadi kubwa ya wananchi kuhudhuria mikutano ya kampeni.

“Ushindi wa mwaka huu ni kimbunga, kila nilipokuwa nafika katika mikutano ya kampeni nakuta watu wamejaa, nilipokuwa naingia Manyara nilipofika eneo la Minjingu nikakuta watu wengi, hata nilipofika Magugu nikadhani nimeingia makao makuu ya wilaya,” alisema Dk. Magufuli.

Aliahidi katika kipindi kijacho, serikali imeweka mkakati wa kuziendeleza bandari, kununua vichwa 36 vya treni pamoja na mabehewa 800.

Kuhusu Mkoa wa Manyara, Dk. Magufuli alisema miaka mitano ijayo serikali itatua kero ya ukosefu wa maji, umeme, ujenzi wa barabara kutoka Babati hadi Kiteto.

Vile vile, aliahidi ujenzi wa barabara za ndani, mitaro, ujenzi wa viwanda, kuajiri wataalamu wa afya, kufuta mashamba ya wawekezaji ambayo hayajaendelezwa, kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wakazi na hifadhi ya Ziwa Manyara, pamoja na ujenzi wa stendi ya kisasa.

Habari Kubwa