JPM aahidi mamilioni kwa wafanyabiashara

06Aug 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
JPM aahidi mamilioni kwa wafanyabiashara

RAIS John Magufuli amewasili Dodoma akitokea Dar es Salaam, akikubali ombi la wafanyabiashara ndogo wa Dumila mkoani Morogoro, kupanua barabara na kujenga vibanda vya kisasa vya biashara kwenye eneo hilo.

Rais John Magufuli akila mhindi wa kuchoma alioununua katika eneo la Dumila Darajani, aliposimama kuzungumza na wafanyabiashara wadogo akiwa njiani kuelekea Dodoma, jana. PICHA: IKULU

Akiwa Dumila jana wakati wa safari yake hiyo, Rais Magufuli alizungumza na wakazi wa eneo hilo ambao wanajishughulisha na biashara ndogo za kuuza mahindi ya kuchoma, mahindi mabichi, nyanya, vitunguu, mboga na bidhaa nyingine zinazozalishwa katika eneo hilo.

Rais Magufuli aliahidi kuwa serikali itatoa Sh. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vibanda hivyo na pia akamwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro kufanya upanuzi wa barabara katika eneo hilo ili kupunguza msongamano wa magari.

“Nawaahidi nitawapa Sh. milioni 100 kwa ajili ya kujenga mabanda mazuri na kupanua eneo lenu la kufanyia biashara,” alisema Rais Magufuli.

Awali, wafanyabiashara hao walimwomba Rais Magufuli awaongezee eneo lililoko kando ya barabara ya kwenda mkoani Dodoma, ili walitumie kufanya biashara zao.

Mmoja wa wafanyabiashara hao alisema wanaomba eneo la shamba liliko karibu na barabara ya kwenda Dodoma wapewe ili kuongeza eneo la kufanyia biashara.

Akiwa kwenye eneo hilo, Rais Magufuli alionekana kufurahia huduma ya chakula alichopewa na wenyeji wake hao, akiyasifu mahindi yao kuwa ni matamu.

Rais Magufuli ambaye ameteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu, wiki hii anatarajia kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kwenye Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dodoma.

Habari Kubwa