JPM aapa kuchukua jimbo lililokaa upinzani miaka 25

25Oct 2020
Gwamaka Alipipi
Karatu
Nipashe Jumapili
JPM aapa kuchukua jimbo lililokaa upinzani miaka 25

MGOMBEA Urais, Dk. John Magufuli (CCM), amesema ni wakati mwafaka kwa wananchi wa Jimbo la Karatu kufanya uamuzi wa kuuondoa upinzani katika jimbo hilo uliodumu kwa miaka 25.

Alisema kama wameongozwa na kiongozi wa upinzani kwa miaka hiyo na hakuna maendelea waliyoyapata, sasa ni wakati mwafaka wa kumchagua mbunge kupitia CCM kwa miaka mitano ijayo.

“Karatu kama mnataka mabadiliko, mleteni Danieli Awack, kama mmekaa kwa miaka 25, jaribuni kuja CCM kwa miaka mitano halafu mniulize,” alitamba.

Dk. Magufuli alisema Mgombea Ubunge wa CCM, Awack, alikuwa ni mjumbe wa NEC na ni mkulima wa vitunguu, lakini amekuwa akipigwa vita kwa sababu hana elimu ya shahada.

“Ninahitaji mbunge atakayewatetea watu, kuwasemea shida zao, ambaye atakuwa kiunganisho kati ya wananchi na serikali. Sihitaji mtu mwenye 'degree' (shahada), kwani kuwasemea watu shida ya barabara lazima uwe na 'degree'?" Dk. Magufuli alihoji.

Mgombea huyo pia alimwagia sifa Balozi Wilbroad Slaa, akimwelezea kuwa ni kiongozi bora kutoka chama cha upinzani, mtu makini na mjenga hoja wakati wote akiwa Mbunge wa Karatu.

Alisema Dk. Slaa alikuwa mwadilifu, mzalendo wa kweli kwa taifa lake na kwamba yawezekana alikuwa hivyo kutokana na kazi yake aliyowahi kuifanya ya kuwa kiongozi wa dini.

"Kwenye upinzani kama kulikuwa na mtu ambaye alikuwa kiongozi bora kuwahi kutokea ni Dk. Slaa, kati ya wapinzani wazalendo nchini, Dk. Slaa ni nambari moja," Dk. Magufuli alisifu.

Alisema Dk. Slaa alikuwa mtu mstaarabu tofauti na wabunge wengine wa upinzani, akisisitiza kuwa hakuwahi kutoa kauli za matusi wala kuweka kibandiko mdomoni kama wanavyofanya wabunge wa upinzani.

"Baada ya kukaa upinzani na kuona ubabaishaji, akaamua kujitoa mwenyewe, nami kwa kutambua uwezo wake, nikamteua kuwa balozi katika nchi tisa," alisema.

Alifafanua kuwa Dk. Slaa kwa sasa anaiwakilisha Tanzania katika nchi za Sweden, Norway, Denmark, Island, Finland, Ukraine, Lativia, Estonia na Lithuania.

Dk. Magufuli pia alisema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imejenga Hospitali ya Wilaya Karatu na upanuzi wa Kituo cha Afya Karatu kwa kujenga wodi ya wanawake na wanaume.

Alisema serikali pia imefanya upanuzi wa zahanati tano, kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh. milioni 131 hadi Sh. milioni 450 zilizokuwa zinatolewa kila mwaka.

Alisema serikali imetoa Sh. bilioni 7.4 kwa ajili ya kugharamia elimu bure, ujenzi wa madarasa 208, utengenezaji wa madawati zaidi ya 4,000, ujenzi wa nyumba za walimu 84, barabara ya changarawe kilomita 34 na kupeleka umeme katika vijiji 47 kati ya 57 vilivyokuwa havijaunganishwa na huduma hiyo.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili ijayo, serikali itahakikisha inavifikia vijiji 10 vilivyobaki kupata umeme wa uhakika.

Habari Kubwa