JPM afichua viongozi serikalini, CCM wachochea migogoro ardhi

30Jun 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM afichua viongozi serikalini, CCM wachochea migogoro ardhi

RAIS John Magufuli amesema migororo ya ardhi katika mikoa ya Morogoro na Pwani inachochewa na baadhi ya viongozi ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais John Magufuli akiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe na viongozi mbalimbali akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki ya reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Kilosa mkoani Morogoro, jana. PICHA: IKULU

Alitoa kauli hiyo jana wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mahandaki ya reli ya kisasa(SGR) kutoka Morogoro hadi Makutupora.

“Kuna baadhi ya viongozi walioko ndani ya serikali wanahusika na migogoro hii, nimeshapata habari hata viongozi wa chama changu, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (ya Kilosa), analaumiwa kwa kuhusika na migogoro hii, na mimi ni msema kweli, msema kweli ni mpenzi wa Mungu,” alisema.

Rais Magufuli aliongeza akionya: “Sasa niwaombe viongozi wote wanaohusishwa na migogoro ya mashamba, muitatue kwa kumtanguliza Mungu mbele, siwezi nikawa na taifa la Watanzania milioni 60, wanakosa mahali pa kulima.

"Nimeambiwa kuna eneo amepewa mwekezaji wala siyo Mtanzania. Hebu Watanzania mjiulize mkienda kutafuta ardhi kwenye maeneo yao hao, mtapata hata ekari moja?"

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999, Sheria ya Vijiji Na. 5 ya Mwaka 1999 na Sheria ya Matumizi ya Ardhi ya Mwaka 2007, na hata Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995, ardhi ya Tanzania atamilikishwa Mtanzania peke yake.

"Akipatikana mtu ambaye siyo Mtanzania na anataka kumiliki hiyo ardhi, lazima aende Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), akapewe kibali na mkataba maalum wa kuiendesha na kwa masharti maalum.

"Na kwa mujibu wa sheria hiyo hiyo, unapopewa ardhi, ni lazima uiendeleze, lakini watu wamechukua maeneo na hawayaendelezi, kuanzia Pwani hadi Morogoro," alisema.

Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, kuunda tume ambayo itafanyia kazi migogoro ya ardhi katika maeneo hayo.

Pia, aliagiza Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, kuwa sehemu ya tume itakayoundwa.

“Ninataka ndani ya siku saba, yale mashamba yaliyobaki nayo tuyafute, lakini ninataka mpange mikakati ya namna ya kuwagawia wananchi maskini,” aliagiza.

Rais aliwaomba viongozi wa dini kusaidia katika kutatua migogoro hiyo, huku akizitaka mamlaka kutowaonea watu ambao wanamiliki mashamba na wameyaendeleza.

“Lakini niwaombe viongozi, wasiwaonee watu wengine ambao wana mashamba yao na wameyaendeleza, lisije hili agizo likatafsiriwa kwamba sasa ni kwenda kuchukua mashamba ya watu.

"Wapo walio na mashamba yao na wameyaendeleza, nina uhakika mkipanga vizuri matumizi ya ardhi na mkashirikisha viongozi mpaka kwenye ngazi za vijiji, tutatatua hili tatizo," alifafanua.

Rais Magufuli aliagiza kuundwa kwa tume hiyo baada ya kutangaza kuwa tayari ameshafuta umiliki wa mashamba 46 na mengine yanasubiri uamuzi ambao aliahidi kuutoa kabla ya Jumamosi.

DC, DED WAONYWA

Kiongozi huyo wa nchi pia aliwaonya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kushindwa kutatua kero za wananchi wa eneo hilo pamoja na kudaiwa kuhusika katika kashfa mbalimbali.

“Nimeambiwa mkurugenzi wa hapa naye ana matatizo, ajirekebishe, siwezi nikamtumbua mbele ya askofu, madhambi yake anayajua, ameuza eneo na alifanya kikao siku hiyo hiyo na mkataba akasaini siku hiyo hiyo.

“DC (Mkuu wa Wilaya) wa Kilosa na wewe jirekebishe, sitaki kuwaficha ndugu zangu, taarifa ninazo za kutosha, ninasikia unaenda na polisi kwenda kuwazuia wananchi wasiingie kwenye shamba, badala ya kuwatetea wananchi unatetea ambao hata huwajui," alionya.

Habari Kubwa