JPM afungua vyuo, kidato cha sita

22May 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM afungua vyuo, kidato cha sita

RAIS John Magufuli ametangaza kuanzia Juni Mosi, vyuo vyote pamoja na kidato cha sita vitafunguliwa na kuwaagiza watendaji wake ndani ya siku tisa kuandaa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo.

Rais John Magufuli, akizungumza na viongozi aliowaapisha katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma jana. PICHA: IKULU

Machi 17 mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza kufunga shule zote za awali, msingi na sekondari na baadaye vyuo vyote kwa muda wa siku 30 kutokana na janga la corona.

Akizungumza jana Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, Rais Magufuli alisema ameamua kufungua vyuo kwa sababu maambukizo ya corona yamepungua.

“Kutokana na hali kwenda vizuri, tumeamua vyuo vyote vifunguliwe Juni Mosi, niwaombe wizara zinazohusika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Fedha na Mipango ambayo inahusika kwenye kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi. Leo (jana) ni Mei 21, tuna siku tisa.

"Wizara hizi zinazohusika, Wizara ya Elimu na Wizara ya Fedha zijiandae ili vyuo vitakapofunguliwa, kusiwe na kero nyingine, kama mwanafunzi anastahili kupata, mkopo wake uwe umeandaliwa mapema," aliagiza.

Rais alisema siku tisa kwa wizara ambayo ipo makini, haiwezi kushindwa kumaliza na kufanya maandalizi na ndiyo maana ameamua kutangaza mapema ili ndani ya siku hizo wajipange.

Aliagiza wanafunzi wa kidato cha sita ambao wanajiandaa kwa ajili ya mitihani yao ya mwisho, nao watarudi kwenye shule zao kuanzia Juni Mosi.

“Wizara ya Elimu ipange vipindi ili wafanye mtihani wao bila kuharibu mwenendo wao wa kuingia vyuo vikuu kama ilivyopangwa, corona usiwacheleweshe,” aliagiza.

Kuhusu shule za msingi na sekondari, Rais Magufuli alisema wameona watoe muda zaidi kwa sababu wanafunzi walioko katika ngazi hiyo ya elimu ni wadogo, hivyo kuna haja nchi kujipa nafasi kadri wanavyopambana na corona.

NDEGE ZA WATALII

Rais Magufuli pia alisema serikali imeamua kuanzia Mei 27 na 28 mwezi huu, ndege za watalii zitaanza kuingia nchini na hawatawekwa karantini kwa siku 14.

“Bahati nzuri wapo wengi ambao wameomba kuja, kuna mashirika mengine yamejaa karibu mwezi Agosti, hatuwezi kuiachia fursa hii na kuendelea kujifungia wakati wao wanaona sehemu za kustarehe ni huku.

“Na utalii mwingine wanaweza kufanya huo wa nyungu kama alivyoeleza (Seleman) Jafo (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi) nao ni utalii wa aina yake.

“Utalii siyo kuona wanyama tu, hata mtu kujifukiza na akanywa dawa za kienyeji na kupona, inawezekana ikawa sekta moja wapo ya kusaidia watu waliokaa kule wamefungwa kwa miezi, wanakuja Tanzania kuona jua na utukufu wa Mungu na wanyama walivyo,” alisema.

HALI YA CORONA

Rais Magufuli alisema hali ya maambukizo imeshuka, akitolea mfano Mkoa wa Singida ambao una wagonjwa watatu tu wanaosubiri vipimo vya mwisho, ili watoke hospitalini.

“Nimetembea kwa gari kutoka Mkoa wa Geita mpaka Dodoma, njiani watu wanajishughulisha na shughuli zao, wanalima, hiki ndicho tunataka kwa ajili ya kujenga uchumi wetu,” alisema.

Habari Kubwa