JPM afuta barua rangi ya bendera

15Dec 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
JPM afuta barua rangi ya bendera

RAIS John Magufuli amefuta mara moja maelekezo ya barua iliyoandikwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya kupokea maelekezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Ndani, kuhusu matumizi sahihi ya bendera, nembo na wimbo wa taifa.

RAIS John Magufuli.

Wakati Rais akiweka msimamo huo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeibuka na kusema rangi hizo zitabaki kama ilivyokuwa awali tofauti na maelekezo ya  Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa rangi ya njano katika bendera ya taifa  iliyozoeleka sasa itabadilishwa na kuwa ya dhahabu,

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais amesema maelekezo hayo yanaathiri uzalendo wa Watanzania na kuleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo katika bendera.

“Hata mimi mwenyewe tangu nasoma shule hadi leo nafahamu kuwa Bendera ya Taifa ina rangi ya njano na siyo rangi ya dhahabu na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote siyo dhahabu pekee yake,” alisema Rais.

Kutokana na barua hiyo, Rais Magufuli alisema ameamua kufuta barua hiyo na kama kuna mabadiliko basi ni lazima yazingatie taratibu zote kwa kuwa jambo hilo ni la kitaifa na siyo la mtu mmoja.

“Nimeagiza bendera, nembo na wimbo wa taifa viendelee kutumika kama ilivyokuwa kabla ya kuandikwa kwa barua hii na natoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao na kuitangaza popote walipo ili mradi wazingatie sheria na maslahi mapana ya Taifa,” alisema Rais Magufuli.

Awali Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilitoa maelekezo kwa vyuo, taasisi kuhusiana rangi za bendera ya taifa huku Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ikisema rangi hizo zitabaki kama ilivyokuwa awali.

Juzi, kwenye mitandao ya kijamii ilisambaa barua ya Novemba 23, mwaka huu, iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Dar es Salaam ikitoa maelekezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  kuhusu matumizi sahihi ya bendera, nembo na wimbo wa taifa.

Akizungumza jana katika kipindi cha East Africa Break Fast kinachorushwa na kituo cha redio cha East Africa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Ave Maria Semakafu, alisema rangi ya njano kwenye bendera ya taifa itabaki kama ilivyo na si dhahabu kama ambavyo imeelekezwa kwenye taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Dk. Semakafu alisema rangi ya njano ina maana yake kwenye bendera na haiwezi kubadilika kama barua iliyosambaa mitandaoni inavyodai.

"Unajua hizi rangi zina maana na haiwezi kubadilika na ndiyo hali halisi. Naomba  muwe mnasikiliza vitu vinavyosemwa na waziri mwenye dhamana lakini hao wanaosemea mitandaoni inatakiwa watoe maelezo wenyewe,” alisema.

Dk. Semakafu alikumbusha kuwa rangi nyeusi inasimama kwa ajili ya watu, kijani kwa ajili ya mazao, bluu kwa ajili ya maji na njano kwa ajili ya madini.

“Wewe si umeenda hadi Ikulu kaka yangu, ile bendera ina tatizo lolote lile uliloliona? Huyo aliyesema ametoa ufafanuzi mfuate yeye umuulize, umshikie bendera ya taifa halafu usikie majibu atakayokupa.

“Ninachoweza kukueleza ni kwamba tumekaa na watoto wetu miaka yote wanaimba bendera ya taifa ina rangi nyeusi, kijani, bluu na njano na hata ukienda Ikulu ile bendera unayoiona ina rangi ya njano,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Huyo aliyekwambia dhahabu akupe bendera ya rangi ya dhahabu, sisi tutaendelea na bendera kama ilivyo sasa. Huo  ndio msimamo na macho yetu yanaona kilichopo kwenye bendera ni njano.”

Barua iliyosambaa mitandaoni juzi yenye kumbukumbu namba CHA-56/193/02/16, kuhusu matumizi sahihi ya bendera, nembo na wimbo wa taifa, iliainisha waliotakiwa kutekeleza agizo hilo.

Maelekezo hayo yalitolewa kwa wakuu wa vyuo vya ualimu, vyuo vya maendeleo ya jamii, wakuu wa vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Barua hiyo ilifafanua kuwa maelekezo hayo yameletwa kwa sababu imebainika kuwa taasisi za serikali zinatumia isivyo sahihi alama za taifa.

Barua hiyo ambayo iliandikwa na Wizara ya elimu na ikiwa na muhuri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ilisema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inaelekeza kuwa Wimbo wa Taifa utapigwa kwa dhifa za kitaifa pekee.

“Endapo hadhi ya sherehe haitambuliki, taasisi inalazimika kuomba kibali kwa Waziri mwenye dhamana, wimbo unatakiwa kuimbwa kwa ukamilifu beti zote mbili kwa kuzingatia ‘nota’ na maneno,” ilisema.

Pia barua hiyo ilielekeza kuwa rangi sahihi za bendera ya taifa kuwa ni kijani, dhahabu, nyeusi na bluu na kwamba ni makosa kutumia rangi ya njano.

Kadhalika barua hiyo ilisema kuwa uwiano wa bendera ni theluthi katika urefu na upana.

Habari Kubwa