JPM amkabidhi nyumba Mzee Mwinyi

19Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
JPM amkabidhi nyumba Mzee Mwinyi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, jana alimkabidhi nyumba mpya ya kuishi Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.

Nyumba hiyo imejengwa na Serikali ya Tanzania na kisha kukabidhiwa kwa Mhe. Rais Mstaafu Mwinyi kwa mujibu wa sheria ya mafao ya viongozi wa kisiasa namba 3 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2005 ambayo inaelekeza kuwa Marais wanapostaafu wanastahili kujengewa nyumba na Serikali.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurian Ndumbaro, alisema ujenzi wa nyumba ya Rais Mstaafu Mwinyi ulioanza mwaka 2005 ulisimama kwa muda mrefu na baadaye mwaka 2018 uliendelea chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Shirika lake la Suma JKT kwa ushirikiano na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) hadi ulipokamilika.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa nyumba hiyo, Rais Mstaafu Mwinyi alimshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msukumo mkubwa wa kukamilishwa kwa nyumba hiyo na pia ameishukuru Suma JKT na TBA kwa kujenga kwa ubora wa hali ya juu.

Rais Magufuli alimpongeza Rais Mstaafu Mwinyi kwa kupata nyumba hiyo, na amemtakia heri na maisha mema katika makazi yake hayo mapya. Pia ameipongeza Suma JKT na TBA kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekagua jengo la nyumba ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete inayojengwa katika eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam.

Ujenzi wa nyumba hiyo ulianza mwaka 2018 chini ya TBA na Rais Magufuli ameiagiza TBA kuhakikisha ujenzi wa nyumba, uzio na mandhali yake unakamilika ifikapo tarehe 30 Januari, 2021.

Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kujenga barabara ya lami yenye urefu wa meta 800 itakayounganisha nyumba hiyo na barabara ya lami iliyokaribu nayo.

Rais Mstaafu Kikwete alimshukuru  Rais Magufuli kwa ujenzi wa nyumba hiyo ambayo amesema anatarajia ndipo ataishi maisha yake yote.

Mapema jana subuhi, Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli walikwenda kumsalimu Mjane wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa nyumbani kwake Masaki Jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa