JPM amtumbua Makalla Katavi

16May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JPM amtumbua Makalla Katavi

RAIS John Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amos Makalla.

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amos Makalla.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amemteua Juma Homera kuwa Mkuu wa Mkoa huo kuanzia juzi.

 

Taarifa hiyo ilisema kuwa kabla ya uteuzi huo, Homera alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma.

 

“Homera anachukua nafasi ya Makalla ambaye uteuzi wake umetenguliwa, uteuzi wa Homera unaanza Mei 14,” ilieleza taarifa hiyo.

 

Aidha, taarifa hiyo ilisema uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru utafanywa baadaye.

 

JPM ALIVYOMMWAGIA SIFA

Alipokuwa kwenye ziara mkoani Ruvuma hivi karibuni, Rais Magufuli alimpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo, Homera kuwa amekuwa mkali na amesimama vyema kusukuma maendeleo.

 

“Inawezekana hamumhitaji sana hapa, lakini kama kuna mikoa itakuwa imezubaa zubaa mtu nitakayempa ukuu wa mkoa ni huyu hapa (Homera), anajua kunyoosha mambo mimi sisemagi pembeni” alisema na kuongeza:

 

“Najua makangomba wanamchukia, unataka kupendwa na wote umeshapendwa na mke wako imeshatosha, hata angefanyaje hawezi kupendwa na wote, kwa hiyo wewe chapa kazi,” alisema Rais Magufuli wakati huo.

 

MAKALLA NI NANI?

 

Makalla aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Septemba 14, 2015.

Machi 12, 2016, wakati Rais Magufuli alipofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya alimhamishia Makalla Mkoa wa Mbeya kabla ya kumpeleka Katavi Julai, mwaka jana.

 

Makalla pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwenye serikali ya Kikwete na baadaye Mweka Hazina wa CCM Taifa.

 

Makalla aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010 kupitia Jimbo la Mvomero akimwangusha kwenye kura za maoni aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo (CCM), Suleman Sadiq.

 

Kwa mara ya kwanza, Makalla alianza kuwania jimbo hilo mwaka 2005 lakini aliangushwa na Murad kwa kura chache kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho.

 

Makalla pia aliwahi kuwa Mweka Hazina wa CCM, Taifa na Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na nafasi zingine kwenye umoja huo.

Habari Kubwa