JPM apiga ‘stop’ michango shuleni 

18Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JPM apiga ‘stop’ michango shuleni 

RAIS John Pombe Magufuli amepiga marufuku michango katika shule za msingi na sekondari na kuagiza kuchukuliwa hatua dhidi ya viongozi na watendaji ambao shule  zilizoko katika maeneo yao, zinaendelea kuwatoza wanafunzi.

Rais John Magufuli akizungumza baada ya kukutana na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako Ikulu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, ilisema michango hiyo ni kinyume cha mwongozo uliotolewa na serikali wa utoaji wa elimu bila malipo na amewaonya viongozi watakaozembea kutekeleza maagizo hayo.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli alisema serikali inatoa Sh. bilioni 23.875 kila mwezi kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa elimu bila malipo, lakini inashangaza kuona bado kuna walimu wanaendelea kuwatoza michango au kuwarudisha nyumbani wanafunzi ambao wanashindwa kutoa michango hiyo.

“Nawaagiza mawaziri, sitaki kusikia mwanafunzi anarudishwa nyumbani kwa kushindwa kutoa michango na fikisheni maagizo haya kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wote wanaohusika. Nikisikia tena mahali jambo hili linaendelea hawa niliowateua mimi wataondoka,” alikaririwa Rais katika taarifa hiyo.

Aliongeza kuwa: “Haiwezekani tumefuta ada, halafu walimu wanaamua kuanzisha michango tena mikubwa ambayo watu maskini wanashindwa kusomesha watoto wao, na kama wazazi wanataka kuchangia kitu shuleni wapeleke michango yao kwa mkurugenzi, lakini sitaki kusikia mwanafunzi anapewa sharti la kutoa mchango ndipo apokelewe shule.”

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo baada ya kupata taarifa kuwa ziko baadhi ya shule ambazo wanafunzi wanadaiwa michango mbalimbali tena kwa kiwango kikubwa ikiwamo chakula, maabara, madawati na ziara za kujifunza, hali iliyosababisha wazazi kushindwa kumudu.

Kutokana na agizo hilo, Waziri Prof. Ndalichako aliagiza walimu na viongozi wa halmashauri kuwarudisha shuleni mara moja wanafunzi wote waliorudishwa nyumbani kwa kutotoa michango. Pia aliagiza kurejesha mara moja michango iliyokusanywa kinyume cha mwongozo wa serikali.

Kwa upande wake, Waziri Jafo aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwasilisha taarifa ya shule ambazo zimetoza michango kinyume cha mwongozo wa serikali ifikapo kesho, ili hatua zichukuliwe dhidi ya walimu na maofisa elimu ambao  wamekiuka mwongozo huo.   

Habari Kubwa