JPM asamehe wafungwa 5,533

10Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
JPM asamehe wafungwa 5,533

MAADHIMISHO ya miaka 58 ya Uhuru na miaka 57 ya Muungano yameacha kicheko kwa wafungwa 5,533 kusamehewa wakiwamo wa uhujumu uchumi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alitoa msamaha kwa wafungwa hao waliopo katika magereza mbalimbali ambao wamebakiza muda wa siku moja hadi miezi 12 na waliotumikia kifungo cha muda mrefu na kubakiza muda usiozidi mwaka moja.

Miongoni mwa wafungwa waliopewa msamaha huo ni pamoja na mahabusi 345 na wenye kesi za makosa ya uhujumu uchumi 256.
Msamaha huo wa Rais Magufuli unatokana na mrundikano wa wafungwa katika magereza mengi nchini kufuatia ziara yake aliyoifanya katika baadhi ya magereza likiwamo la Butimba.

"Mnakumbuka miezi michache iliyopita nilitembelea baadhi ya magereza likiwamo Gereza la Butimba, kweli nilishuhudia kuwapo kwa mrundikano wa wafungwa, nikaelezwa hali kama hiyo haipo Butimba peke yake bali ni kwa magereza yote nchini na mpaka sasa tunavyozungumza leo kuna wafungwa 17,547, mahabusi 18,256, hivyo wafungwa na mahabusi tulionao katika magereza yetu ni 35,803," alisema Magufuli.

Ameeleza kuwa kama mwanadamu hali aliyoishuhudia alipotembelea Gereza la Butimba, Julai 16, mwaka huu ilimsikitisha na kwa kuwa Mwenyezi Mungu anasamehe na kwa kuwa dini zote zinafundisha kusamehe, kwa mamlaka aliyonayo amewasamehe wafungwa hao.

"Kwa mujibu wa madaraka niliyopewa katika ibara ya 45 ibara ndongo ya kwanza kifungu cha ‘a’ mpaka ‘e’ cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara hii imeandika mamlaka ya kusamehe au kufuta adhabu ya mtu aliyetiwa hatiani na mahakama, ibara hiyo ikisomwa pamoja na kifungu cha 49 cha Sheria ya Magereza, sura ya 58 ,ndugu zangu nimeguswa na nimeamua leo tarehe 9 Desemba, 2019 katika kusherehekea miaka 58 ya Uhuru wetu nasamehe idadi kubwa sana ya wafungwa jumla ya wafungwa 5,533," alisema Rais Magufuli.

"Najua ni idadi kubwa na watu wanashangaa, lakini nimeguswa na moyo wangu ninasamehe wafungwa 5,533," alisisitiza.

Alitaja mikoa ambayo wafungwa wao wamesamehewa na idadi yake kwenye mabano ikiongozwa na Mkoa wa Kagera (713), ikifuatiwa na Dodoma (385), Morogoro (365), Dar es Salaam (293), Mara (260), Mbeya (259) na Kigoma (252).

Mingine ni Tanga (245), Geita (230), Rukwa (214), Arusha (208), Manyara (207), Tabora (207), Mwanza (190), Ruvuma (181), Singida (139), Simiyu (136), Lindi (129), Pwani (128), Iringa (110), Songwe (96), Katavi (74) Shinyanga (74) na Njombe (70).

Wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo walionyesha kufuruhishwa uamuzi huo wa Rais na kuibua shangwe, vigelegele, na makofi.

Maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru yamefanyika jijini Mwanza kwa mara ya kwanza tangu kupatikana kwa Uhuru na kuhudhuriwa na idai kubwa ya watu, baadhi yao wakiamua kwenda uwanja wa Furahisha na Rock City Mall kufuatilia kupitia matangazo mubashara yaliyorushwa na vyombo mbalimbali vya habari baada ya kukosa nafasi ya kuingia ndani.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na Nipashe walieleza kufurahishwa na maadhimisho hayo.

"Leo ni siku ya historia kwangu, niliisubiri kwa muda hatimaye imefika na nimekuja hapa mapema alfajiri saa kumi na nimekuta baadhi ya watu wameshaingia," alisema, Lidya Erro, mkazi wa Ilemela.

"Mimi nimelala hapa ndugu yangu, ninakaa kule Ndagalu Wilaya ya Magu na niliona nikilala nyumbani usafiri wa kunifikisha hapa asubuhi na mapema hakuna, nisingewahi, ningekuta geti zimefungwa kwa hiyo nimekuja hapa jana, nikalala hapa 'uwanjani', asubuhi sijasumbuka kutafuta usafiri wala sehemu ya kukaa," alisema Shihologanya Maliganya, mkazi wa Ndagalu, Wilaya ya Magu.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa serikali, waliostaafu, mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali nchini na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Maadhimisho ya mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu 'Miaka 58 ya Uhuru na Miaka 57 ya Jamhuri, Uzalendo, Uwajibikaji na Ubunifu ni Msingi wa Ujenzi wa Uchumi wa Taifa Letu'.

Habari Kubwa