JPM asisitiza ushirikiano Nordic

09Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
JPM asisitiza ushirikiano Nordic

RAIS John Magufuli amezishukuru nchi za Nordic kwa uhusiano na ushirikiano wao mzuri na nchi za Afrika ikiwamo Tanzania na kuzitaka kujielekeza zaidi katika ushirikiano wa kiuchumi.

Aliyasema hayo jana alipohutubia Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mawaziri 29 wa nchi za Afrika na watano Norway, Sweden, Denmark, Finland na Iceland, Rais Magufuli alisema Afrika inakumbuka mchango mkubwa uliotolewa na nchi za Nordic kabla na baada ya harakati za ukombozi.

Alisema katika mchango huo, nchi hizo zilichangia katika huduma za kijamii na kiuchumi kama vile afya, elimu, kilimo, sayansi na teknolojia, nishati, mazingira pamoja na kulinda amani na usalama.

Rais alitolea mfano wa Tanzania kutokana na nchi za Nordic kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Kibaha, Chuo cha Utafiti wa Kilimo Uyole, vyuo mbalimbali vya ufundi na kampeni za kufuta ujinga katika miaka ya 1970.

Hata hivyo, alisema kuna haja ya kubadilisha mwelekeo na kuingia katika mwelekeo wa kisiasa unaojikita katika ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji.

Alisisitiza kuwa nchi za Nordic zenye watu wapatao milioni 27 zina uchumi mkubwa unaofikia pato la mwaka la Dola za Marekani trilioni 1.7 ikilinganishwa na nchi za Afrika zenye watu milioni 1.2 lakini pato la mwaka ni Dola za Marekani trilioni 2.334.

Kutokana na hali hiyo, alisema Afrika inapaswa kujifunza kutoka Nordic na amezikaribisha nchi hizo kuwekeza Afrika katika viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao, kuzalisha ajira na kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo.

Rais alibainisha kuwa Afrika ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwamo eneo la ukubwa asilimia 30 ya eneo lote duniani linalofaa kwa kilimo, ukanda wa pwani ya bahari wenye urefu wa kilometa 30,500, mifugo, misitu, wanyamapori, mafuta, gesi, utalii na uchumi wake unaokua vizuri kwa wastani wa asilimia 4.1.

Pia alitoa wito kwa Afrika kujenga mazingira mazuri yatakayovutia uwekezaji kutoka nchi za Nordic na kusema kwa kutambua hilo, Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti za kuvutia uwekezaji huo ikiwamo kuwa na sheria za kuwalinda wawekezaji, kutekeleza mkakati wa kurekebisha na kuboresha mazingira ya biashara (The Blue Print) na kutenga kanda maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na uwekezaji.

Hatua zingine, kwa mujibu wa Rais, ni kujenga na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kama vile barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, kujenga meli, kununua ndege na kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme.

Baada ya kuhutubia mkutano huo, Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Ann Linde; Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Ine Marie Eriksen Søreide na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Pekka Haavisto.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli aliwaomba mawaziri hao kupeleka salamu zake kwa wakuu wa nchi zao na amewahakikishia kuwa Tanzania iko tayari wakati wote kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano uliopo, mkazo zaidi ukiwa katika biashara na uwekezaji.

Habari Kubwa