JPM ataka vyombo vya habari kuwa na utaifa, uzalendo

26Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM ataka vyombo vya habari kuwa na utaifa, uzalendo

RAIS John Magufuli, amevitaka vyombo vya habari vitoe taarifa za ukweli bila kuweka chumvi, kuzingatia maslahi ya taifa na uzalendo.

Alitoa rai hiyo, jana, alipozungumza na wananchi baada ya kuzindua miradi jijini Dar es Salaam, akisisitiza habari wanazihitaji, lakini lazima zikitolewa zitangulize uzalendo.

"Wito wangu kwa wanahabari na Watanzania, vyombo vya habari tunavihitaji, habari tunazihitaji, lakini tutangulize sana uzalendo. Uzalendo ni kitu muhimu, kitu muhimu kingine ni haki kwa yule anayeandikiwa habari.

"Kumekuwa na habari nyingi za uzushi zinatolewa mara fulani kafa, vigogo wafa, vigogo wapuputika. Ni mambo ya ajabu. Imefikia hatua Watanzania wanaombeana kufa, ni upendo wa ajabu," alisema.

Rais Magufuli alisema katika taarifa ambazo taifa linachafuliwa, wapo watu bila kujali wanazishabikia na hiyo inaonyesha uzalendo umepungua.

"Niwaombe Watanzania na wanahabari mtangulize uzalendo, hapatatokea mtu atakayejenga taifa letu. Yapo mataifa ambayo yanatokea ya ajabu sana katika maeneo yao, lakini huwezi kusikia yameandikwa au kuweka mtandaoni.

"Tumekuwa wepesi kwa sababu ya uhuru huu, kila kitu hata kile ambacho hakifai kinaandikwa. Niwaombe Watanzania wote na hili siyo kwa waandishi wa habari tu kwa sababu wanaotuma mitandaoni wengine siyo waandishi," alisema.

Rais Magufuli aliwataka wananchi watangulize maslahi ya taifa na uzalendo kwanza kwa sababu wanaojenga na kubomoa nchi ni wao wenyewe.

Vilevile, alitoa wito kwa watendaji wa serikali kuhakikisha wanakuwa wepesi kutoa taarifa kwa waandishi wa habari pindi wanapozihitaji kwa kuwa baadhi ya wizara wamekuwa wakizificha.

"Ziko wizara ambazo waandishi wakienda kuzitaka taarifa, zinafichwa pamoja na kwamba tuna wawakilishi. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, fuatilia hili," aliagiza.

Alitaka serikali iwe inatoa taarifa mapema ambazo zinaleta faida kwa Watanzania badala ya kuzificha hata zinazohusu maendeleo.

"Unakuta yamefanyika mambo mazuri, lakini hayatolewi kwa wananchi ili kujua ni yapi yamefanyika. Tusiogope kukosolewa, tukubali pia kujirekebisha kwa ajili ya kuwapatia wananchi habari muhimu kwa sababu ni haki yao," alisema.

Rais Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano, serikali imeimarisha haki na uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha vinatoa haki.

"Serikali haichukii wanaotupa changamoto na kutukosoa kwa staha. Kitakwimu tumeruhusu vyombo vingi vya habari katika kipindi hiki kuliko wakati wowote tangu uhuru.

"Mwaka 2015, tulikuwa na vituo vya redio 106. Hadi mwezi sasa, vipo 193. Televisheni zilikuwa 25 na sasa zipo 46. Redio za mtandaoni zilizosajiliwa ni 23 na televisheni za mtandaoni zipo 440.

"Tangu mwaka 2016 ilipopitishwa Sheria ya Uhuru wa Habari, serikali imetoa leseni za magazeti ya kila siku na ya kila wiki na mwezi 247," alibainisha.

Kuhusu mali za CCM, Rais Magufuli alisema: "Ufisadi hata CCM upo, ufisadi hauna chama, ndiyo maana nilipoingia madarakani nikamchukua Dk. Bashiru (Ally) kuongoza timu ya uchunguzi wa mali za chama na kukuta Channel Ten ilichukuliwa na watu wengine."

Alisema wakati wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliamua jengo la Jitegemea ambalo kituo hicho cha televisheni kinarushia matangazo yake, liwe Chuo Kikuu cha kwanza cha Tanganyika na kilichoanza na wanafunzi 14 na kueleza kuwa kwa miaka 16 limekuwa gofu na kueleza kuwa siyo ajabu lingeuzwa.

Habari Kubwa