JPM ataka Watanzania kukataa ubaguzi

21Oct 2020
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
JPM ataka Watanzania kukataa ubaguzi

ZIKIWA zimebaki siku saba kuelekea uchaguzi mkuu, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, amewataka Watanzania kujitenga na propaganda za ubaguzi zinazoenezwa na baadhi ya wagombea.

Pia amewatahadharisha Watanzania wakimwona mtu anazungumza na kutangaza chuki, wafahamu kwamba hayupo kwa maslahi ya taifa, bali ana malengo mabaya ya kuleta machafuko nchini.

Alitoa rai hiyo jana wilayani Korogwe mkoani Tanga, wakati akiwahutubia wananchi na wanachama wa CCM waliojitokeza katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Korogwe. Pamoja na mambo mengine, aliwakumbusha Watanzania kuendelea kudumisha amani.

“Wenye roho mbaya watajitokeza kwa sababu wameiona Tanzania imetoka katika umaskini wa mwisho. Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 Afrika ambazo uchumi wake unakua. Tanzania ina mali kila sehemu, watu wanaimezea mate, watafurahi siku moja kuona Watanzania wanapigana ili wao waje kutuuzia silaha huku wakichimba madini,” alisema na kuongeza:

“Mkimaliza kupigana mnakuta wamemaliza kila kitu. Lazima Watanzania kujitenga na watu wa propaganda hizo. Wataleta watu wa uchonganishi, wameshashindwa lakini wanahamasisha watu kuandamana.”

Magufuli alisema mataifa mengi duniani huwa yanaingia katika machafuko kutokana na kuenezwa kwa uduni, ukabila na umaeneo, hivyo akawataka Watanzania kuwapuuza viongozi wanaohamasisha masuala hayo.

“Wagombea urais tupo 15, ukiona mtu anazungumza na kutangaza chuki ujue hayuko kwa maslahi ya taifa. Mapigano mengi duniani huchonganishwa kwa udini, ukabila au umaeneo, Nawasihi hata vijana wetu ambao hata hamuangalii historia ya taifa hili kuweni watulivu,” alisisitiza.

Kuhusu Mkoa wa Tanga, Dk. Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano serikali ilitoa Sh. bilioni 55.7 kugharamia elimu bure, Sh. bilioni 17.8 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwamo ukarabati wa shule ya wasichana Korogwe.

Dk. Magufuli alisema, katika afya, serikali ilipeleka Sh. bilioni 17.4 kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa wa dharura na jengo la kuchuja damu kwa wagonjwa wa figo kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.

Alisema pia serikali imejenga hospitali za wilaya tano ambazo tatu katika Wilaya za Korogwe, Muheza na Tanga Jiji, huku mbili zikiwa katika wilaya za Handeni na Mkinga ambazo ujenzi wake bado unaendelea.

Kuhusu sekta ya maji, Rais  Magufuli alisema serikali imetekeleza miradi 64, mjini ikiwa ni miradi 10 na vijijini miradi 54, kwamba miongoni mwa miradi hiyo ni wa Pungwe-Muheza uliogharimu Sh. bilioni 3.07 ambao hadi sasa umefikia asilimia 85.

Alitaja mradi mwingine ni Mkata-Malesi uliogharimu Sh. bilioni 2.53. Alisema mradi wa Mto Pangani kutoka Korogwe-Mheza wenye thamani ya Sh. bilioni 200 utaanza kujengwa mwanzoni mwa mwaka ujao.

Wakati huohuo, Rais Magufuli akiwa wilayani Same mkoani Kilimanjaro alimwagiza mkandarasi anayejenga mradi wa maji wa Bwawa la Nyumba ya Mungu kuongeza kasi ya ujenzi wa bwawa hilo ndani ya siku 30.

Pia alimtaka Mkurugenzi wa Wizara ya Maji, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Waziri, kuhakikisha wanafika katika mradi huo na kumpeleka ripoti.

“Mradi ulitakiwa kukamilika tangu mwaka 2017, haiwezekani hadi leo uwe bado. Haiwezekani wananchi wa Hedaru wazame kisa tatizo la maji, wamesubiri kwa muda mrefu, nawaomba radhi, kwa hiyo kama wapo watu walikula pesa za mradi huo Sh. bilioni 200 waanze kuzitapika kuanzia leo,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza:

“Nawahakikishia kuwa siwezi kuzungumza uongo, ninafahamu kuzungumza uongo ni dhambi, uwe Waziri au Naibu Waziri au Katibu Mkuu au Mkurugenzi kwa sababu mimi bado ni rais, nataka kesho waende kukagua mradi nikifika Moshi waniletee ripoti,” alisema Dk. Magufuli.

Habari Kubwa