JPM atoa ndege za Rais kubeba abiria

12Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
JPM atoa ndege za Rais kubeba abiria

RAIS John Magufuli, emetoa ndege mbili zinazotumika kwa safari zake za kikazi, zipakwe rangi na kuandikwa jina la Shirika la Ndege Tanzania 
(ATCL) ili zitumike kusafirisha abiria.

Amesema ameamua kutoa ndege hizo kwa kuwa hana utaratibu wa kusafiri mara kwa mara, hivyo haoni sababu na ndege hizo kukaa bila shughuli ilhali kuna Watanzania wanaohitaji usafiri.

Rais Magufuli alitangaza uamuzi huo jana, alipokuwa akizungumza katika hafla ya kupokea ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 iliyowasili jana saa 9:5 alasiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ikitokea nchini Canada.

“Nimeshatoa maagizo, ndege za Rais ambazo zipo tatu, ipo ya Fokker 60 na Fokker 29 zitapakwa rangi ya Air Tanzania ili ziwe zinabeba abiria. Siku zinapokuwa hazitubebi  huku kwetu, ziwe zinabeba abiria. Kwanza Rais hatembei tembei sana, sasa kwa nini zikae tu wakati kuna watu wanatakiwa kubebwa na ndege?” alihoji Rais Magufuli.

Alisema ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiria 50 kila moja, zinaweza kupangiwa safari za kwenda katika mikoa mbalimbali nchini kuchukua abiria kwa ajili ya maendeleo ya nchini.

Rais Magufuli alisema lengo la serikali ni kuwa na ndege za kutosha zinazobeba Watanzania kwa sababu hayo ndio matamanio yake.

Aidha, alisema baada ya kupokea ndege ya sita jana, zingine mbili zinatarajiwa kuwasili nchini mwishoni wa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao ambazo zitafanya kufikia ndege nane.

Kwa mujibu wa Rais, ndege aina ya Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 kutoka nchini Marekani inatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka huu na kwamba nyingine aina ya Bombardier inatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka 2020.

“Hii ndege ya sita niliyopokea leo (jana) si ya mwisho, zingine mbili zinakuja mwishoni mwa mwaka huu na kufanya jumla ziwe ndege nane.  Ndege hizi zitakuwa zinapishana tu angani, maana tulishuhudia kuona ndege kwenye nchi za wengine,” alisema Rais Magufuli.
 
Ucheleweshaji ndege walipa

Rais  Magufuli alisema kampuni ya ndege iliyokuwa ikitengeneza ndege hiyo, iliichelewa kufanya kazi hiyo, hivyo imetozwa Dola za Marekani milioni 1.3 kwa shirika la ndege kama fidia na fedha hizo zimeshalipwa.

Alisema ndege ya Bombardier  nayo walichelewesha hivyo walikuwa wakilipa Dola za Marekani  1,500 kila siku hadi walipokamilisha na kwamba fedha hizo zimerudishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kupangiwa shughuli zingine za miradi ya maendeleo.

“Hii ndiyo biashara na ndiyo Tanznaia ninayoitaka mimi,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa wataalam wa ATCL walipookwenda Canada kufuata ndege hiyo, walimweleza kuwa ilicheleweshwa na wanatakiwa kulipa fidia.

“Walivyokuwa Canada niliwaambia wasiondoke bila kuandikiwa ‘cheque’ (hundi) kabisa na kweli wakafanya hivyo. Lakini ingekuwa enzi zile wangezichapa hizo fedha huko huko bila sisi kufahamu chochote,” alisema.

Pia alisema kuwapo kwa ndege hizo kumewezesha mabinti 102 kupata ajira kwenye shirika la ndege na marubani 50 ambao wameshaajiriwa.

 “Hizi ndege zisingekuwapo hawa marubani walioendesha ndege kutoka Canada hadi hapo wangepata wapi kazi, si wangeendesha matoroli pale mjini, lakini leo wameendesha ndege,”

ATCL waendeshe kwa faida

ATCL wapunguze matumizi ya hovyo na kuhakikisha kila bishara wanayofanya wanapata faida na siyo kujiendesha kwa hasara.

Alisema kama hawataweza kujiendesha kwa faida anaweza kuwanyang’anya ndege na kulipatia shirika lingine ili kuendesha ndege hizo kwa faida.

Nye Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, alisema wanatarajia kuanza safari za ndege kwenda Dodoma kila siku kuanzia Januari 16, mwaka huu.  

Alisema ATCL ina mpango wa kufufua safari za ndege katika mikoa ya Lindi na Mtwara baada ya kukamilika kwa ukarabati katika viwanja vya ndege pamoja na ukle wa uwanja wa Songea mkoani Ruvuma.

Kuhusu Airbus
Ndege ya Airbus A220-300 ambayo ni ya pili kuwasili nchini ilitanguliwa na ile iliyowasili nchini Disemba 23, mwaka huu ambayo ina urefu mita 38.7 na kwa jumla inaweza kupakia abiria 141.

Urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5, na upana wa mabawa yake ni mita 35.1.
Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa Kilometa 5,920 kwa safari moja na inaweza kupaa ikiwa na uzani wa tani 67.6, na kutua ikiwa na uzani wa tani 58.7.

A220-300 ndiyo ndege kubwa miongoni mwa ndege za familia ya A220 na iliundwa kulenga soko la safari za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.

Habari Kubwa