JPM atoa neno  uchaguzi mitaa

16Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
GEITA
Nipashe
JPM atoa neno  uchaguzi mitaa

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kuchagua viongozi bora na wasiotoa rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Rais Magufuli alitoa rai hiyo jana alipokuwa anawasalimu wananchi wa Kata ya Nyankumbu mjini Geita baada ya msafara wake kusimama kutokana na umati mkubwa wa watu waliotaka kusikia neno kutoka kwa kiongozi wao huyo.

Alisema wananchi wanapaswa kuutumia uchaguzi huo kuwachagua viongozi bora ambao hawatawashawishi kwa rushwa na watakuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa.

Rais Magufuli alisema serikali ya awamu ya tano inahitaji viongozi bora, wachapakazi na wanaochukia vitendo vya rushwa.

"Ndugu zangu wananchi, mwaka huu ni kipindi cha uchaguzi wa kuchagua viongozi wa serikali za vijiji, vitongoji na mitaa, chagueni viongozi bora na siyo bora viongozi, chagueni wasiotoa rushwa na wawe viongozi watakaoweza kuzuia rushwa," alisema.

Rais Magufuli pia aliwataka wananchi kutokubali kugawanya na itikadi za kidini na kisiasa, badala yake waendelee kudumisha amani na mshikamano nchini.