JPM atoa somo EAC

23Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JPM atoa somo EAC

RAIS John Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusimamia vizuri rasilimali walizonazo na kukusanya kodi vizuri, ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Rais Dkt. John Magufuli akiwa ameshikana mkono na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta huku wakifurahia jambo, walipokutana nchini Uganda kwenye mkutano wa Wakuu wa EAC. Pembeni ni Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (mwenye kofia)

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema jana kuwa Rais Magufuli alitoa wito huo jana mjini Kampala, Uganda wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa nchi za EAC unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

Ilisema kabla ya Rais Magufuli kutoa mchango wake, marais walioshiriki mkutano huo walipokea taarifa ya mkutano wa majadiliano ya kisekta kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

Ikulu ilisema taarifa iliyowasilishwa ilieleza kuwa katika miaka 10 ijayo nchi za EAC zitahitaji dola za Marekani bilioni 78 (Sh. trilioni 175.5) kutekeleza miradi ya miundombinu inayopendekezwa.

Ilisema taarifa hiyo imechangiwa na wadau mbalimbali wakiwamo marais, wawakilishi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo ambao wameelezea njia mbalimbali za kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo ikiwamo kutumia mfumo wa Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).

Katika mchango wake, Rais Magufuli alisema pamoja na kutumia mfumo wa PPP ni muhimu kwa serikali za kila nchi kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine, ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.

Alitahadharisha kuwa ingawa mfumo wa PPP ni mzuri, ni vyema wataalamu wakachukua tahadhari za kutosha, ili kuepusha serikali kuingia katika mikataba isiyokuwa na maslahi kwa nchi zao kutokana na baadhi ya wadau wa sekta binafsi kutaka kutengeneza faida kubwa kwa kupandisha gharama za miradi.

Rais Magufuli alitolea mfano wa miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa nchini ukiwamo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stieglers' Gorge), imeelezwa.

Katika mifano hiyo, imeelezwa, Rais Magufuli alisema serikali imeamua kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha zake baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri rasilimali zake na kubana matumizi.

"Mimi naamini tukiamua tunaweza," taarifa ilimkariri Magufuli akisema, kwa kuwa "nchi zetu zina rasilimali nyingi za kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo".

"Mathalani tafiti zinaonesha kuwa kama nchi zetu zitaweza kukusanya vizuri mapato ya kodi, zinaweza kutekeleza nusu ya miradi yake ya maendeleo.

"Lakini ukiachilia mbali mapato ya kodi, tunapoteza fedha nyingi kupitia utoroshaji wa rasilimali zetu, ripoti ya jopo la Umoja wa Afrika lililoongozwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki imeeleza kuwa nchi za Afrika zinapoteza dola za Marekani bilioni 150 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa rasilimali."

Marais waliohudhuria mkutano huo ni mwenyeji Yoweri Museveni, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Salva Kiir wa Sudan Kusini wakati viongozi wa Rwanda na Burundi waliwakilishwa.

Leo Rais Magufuli atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa EAC, taarifa ilieleza zaidi.