JPM awaalika wawekezaji wa Qatar

22Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
JPM awaalika wawekezaji wa Qatar

RAIS John Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman J.A. Al Thani, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro mgeni wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al Than mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema viongozi hao walizungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili na dhamira yao ya kuhakikisha unaendelezwa na kukuzwa zaidi hususani katika uwekezaji kwenye gesi, madini, utalii na miundombinu ya barabara, bandari, nishati, reli na huduma za kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli alimshukuru Sheikh Mohammed kwa kuja kwake hapa nchini pamoja na ujumbe wa wawekezaji wenye dhamira ya kuwekeza nchini na kumwomba ampelekee salamu za shukrani kwa Mtawala wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kwa kuendeleza uhusiano na Tanzania.

Rais Magufuli alisema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji zikiwamo uchakataji wa gesi, madini, utalii na usafiri wa anga, hivyo akamwomba Sheikh Mohammed kuwahamasisha wafanyabiashara wa Qatar kushirikiana na Tanzania kuwekeza katika maeneo hayo.

“Natambua kuwa Qatar mna utaalamu wa kuchakata gesi na sisi tunayo gesi nyingi. Kwa hiyo nawakaribisha mje tushirikiane kuwekeza katika sekta ya gesi. Pia natambua kuwa nyie ni wanunuzi wakubwa wa dhahabu na sisi tunayo dhahabu nyingi na hivi sasa tumeanzisha vituo vya ununuzi wa dhahabu. Nawakaribisha mje mnunue dhahabu na tutawapa ushirikiano wote mtakaouhitaji,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli aliiomba Qatar kushirikiana na serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo uzalishaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa reli, barabara na madaraja na amemwalika Mtawala wa Qatar kufanya ziara Tanzania.

Sheikh Mohammed kwa upande wake, alimshukuru Rais Magufuli na serikali yake kwa kuendelea kushirikiana na Qatar katika masuala mbalimbali na kubainisha kuwa Qatar inathamini uhusiano huo.

Pia aliahidi kuwa Qatar iko tayari kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Rais Magufuli na kuzileta kampuni za nchi hiyo kuwekeza katika maeneo yenye fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema baada ya kukutana na Rais Magufuli, yeye na Sheikh Mohammed watakuwa na mazungumzo ya kina kuhusu maeneo ya ushirikiano.

Mazungumzo ya viongozi hao yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Abdullah Jassim Mohammed Al Medadi.

Habari Kubwa