JPM awaonya wabunge uvamizi maeneo hifadhi

10Jul 2019
Mary Geofrey
Nipashe
JPM awaonya wabunge uvamizi maeneo hifadhi

RAIS John Magufuli, amewaonya wabunge wanaoogopa kuwaeleza ukweli wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi za taifa, mapori ya akiba, mapori tengefu na maeneo ya hifadhi yanayomilikiwa na jamii (WMA) kwa kuogopa kunyimwa kura.

Amesema wananchi wamekuwa na tabia za kuvamia maeneo hayo huku wabunge wa maeneo yao wakiogopa kuwaambia ukweli kwa kuhofia kunyimwa kura wakati wa uchaguzi.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa hafla uzinduzi wa hifadhi mpya ya Burigi, katika Kijiji cha Mkolani, wilayani Chato, mkoani Geita.

Alisema wananchi wanapaswa kulinda hifadhi na maeneo ya mapori ya akiba na tengefu na kuacha kusogelea maeneo ya hifadhi kwa sababu watasababisha maeneo hayo kupotea kutokana na shughuli za binadamu na mifugo.

"Wabunge wamekuwa wakisogelea maeneo ya hifadhi. Na sisi wabunge kwa sababu ya kutaka kura kila siku wanasema wananchi wangu, wananchi wangu 'tusicompromise' (tusijadili) siasa na maendeleo ya Watanzania, tunapotea, waambieni ukweli ili mwananchi akikunyima kura akunyime, lakini hifadhi iendelee kuwapo na taifa lineemeke," alisema Rais Magufuli.

"Hizi siasa za kudanganyana ili tupate kura ni mbaya ndugu zangu wabunge, mimi ni mwanasiasa vile vile, lakini kule Tuangoma niliwaambia ukweli, Kasenga niliwaambia ukweli ifike mahali tuseme ukweli na ukweli utasimama kuwa ukweli."

Alisema serikali iliunda tume ya kuchunguza maeneo ya Hifadhi ya Burigi yaliyovamiwa ripoti ambayo imewasilishwa, hivyo kwa maeneo ambayo yaliyovamiwa yatafanyiwa marekebisho.

Alisema marekebisho hayo ya kuweka mipaka hiyo yatakuwa ya mwisho kwa sababu wakiendelea kuruhusu uvamizi na kufanya marekebisho hifadhi hiyo na nyingine zitapotea.

"Ndugu zangu wa maeneo yote niliyoeleza tuache tabia ya kuyavamia maeneo haya kwa sababu tusipoacha tutayapoteza yote," alisema Rais Magufuli.

Aliwaagiza viongozi wa mikoa ya Kagera na Geita wasimamie maeneo yote ambayo yatawekwa alama ili kusiwapo na watu wanaoendelea kusogea eneo hilo la hifadhi.

Kadhalika aliwakemea viongozi wa vijiji vinavyozunguka maeneo yote ya utalii wenye tabia za kuchukua fedha kutoka kwa wafugaji na kuwaingiza katika maeneo hayo kuacha mara moja.

"Kumekuwapo na tabia ya viongozi wa vijiji wanapokea hela kutoka kwa wafugaji wanawaruhusu wananchi wapeleke ng'ombe zao katikati, msiruhusu ng'ombe waende huko," alisema Rais Magufuli.

Vile vile, alisema anatambua uhitaji wa maeneo ya kufugia mifugo na tayari serikali ina mpango wa kuainisha baadhi ya maeneo ya hifadhi kwa ajili ya ufugaji.

"Tunaangalia katika hii tume iliyoundwa na mawaziri wanane, tutaangalia baadhi ya maeneo ya hifadhi za misitu ambayo tutayatenga ili mifugo ipelekwe huko, watu wakafuge ng'ombe zao na tutayatangaza baadaye," alisema Rais Magufuli.

Alisema changamoto iliyokuwapo maeneo ya hifadhi yalikuwa yanapanuliwa, lakini ya wafugaji na makazi ya watu yalikuwa hayapanuliwi.

Alisema kwa sasa nchini ng'ombe wamefika milioni 30.5 na kuna watu milioni 55, hivyo kama maeneo ya mifugo na ya kuishi watu hayataongezwa uvamizi utaongezeka.

Rais Magufuli aliwasihi Watanzania kuendelea kutunza maeneo yote yaliyoainishwa na serikali kuwa sehemu za vivutio sambamba na kulinda amani kwa lengo la kujiongezea kasi ya kupata watalii wengi na kusaidia kukuza uchumi wa taifa.

Alisema sekta ya utalii inachagia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni nchini zinatokana na utalii hivyo kushika nafasi ya kwanza pamoja na kutoa ajira nyingi.

Alisema kutokana na umuhimu wa hifadhi mpya tatu, serikali inaendeleza mpango wa kuendeleza utalii kwa upande wa Kusini mwa Tanzania, mpango ambao ulizinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Alisema mradi huo utatekelezwa kwa gharama ya Sh. bilioni 340 inayohusisha miundombinu na uwezeshaji wa wananchi.

Rais Magufuli pia aliitaka Hifadhi ya Taifa (Tanapa) kuwahamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya hifadhi kwa kupunguza gharama za utalii kwa wazawa.

Kadhalika aliwasihi Watanzania kuanzisha hifadhi ndogo ndogo ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii nchini.

VIONGOZI WALIOFANIKISHA HIFADHI

Pia, aliitaka wizara kumpongeza kwa mchango wake mkubwa wa kuwezesha kupatikana kwa hifadhi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adelardus Kilangi.

Wengine waliopongezwa ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerani mstaafu, Salum Kijuu, ambaye alipatiwa cheti na hundi Sh. milioni 10 kwa mchango wake mkubwa katika hifadhi hiyo.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamuro, Saada Malunde, ambaye alikuwa mhamasishaji na kuwasaidia wananchi wasiingie katika hifadhi hiyo, alipatiwa cheti na hundi ya thamani ya Sh. milioni tano.

Faustine Masalu Kaimu Kamishna wa operesheni za ulinzi wa hifadhi, alipongezwa kwa kuwa kiungo cha hifadhi hiyo ambaye alipatiwa cheti na hundi ya Sh. milioni 2.5.

Naye Bilamungu Kagoma ambaye alikuwa Msimamizi wa pori kwa kukamata wanyama ambao hawakuwa wanakamatika ambaye alipigwa vita na kusimamishwa kazi na baadaye Rais Magufuli aliagiza arudishwe kazini, alipatiwa cheti na hundi ya Sh. milioni mbili.

Awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala, alisema hifadhi ya Burigi Chato iliyopandishwa hadhi kutoka katika mapori ya akiba ya BBK yaliyojumuisha Biharamuri, Burigi na Kimuso,
Awali zilikuwa zikifanyika shughuli za uwindaji katika mapori hayo, hivyo shughuli hizo zitabadilika, kutakuwa na ulinzi wa kutosha na usalama wa eneo lote.

Alisema hifadhi hiyo ya tatu kwa ukubwa nchini ikitanguliwa Ruaha na Serengeti itakuza sekta ya utalii kwa sababu wana uhusiano wa karibu na wakazi wa mikoa inayozungukwa na hifadhi hiyo.