JPM awaonya wafanyabiashara kutumia machinga kukwepa kodi

26Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM awaonya wafanyabiashara kutumia machinga kukwepa kodi

RAIS John Magufuli amewaonya wafanyabiashara wakubwa wanavyokwepa kodi ya serikali kwa kuwatumia machinga kuuza bidhaa zao.

Alitoa onyo hilo jana, alipohutubia wananchi baada ya kuzindua jengo la Jitegemee lililoko Lumumba jijini Dar es Salaam ambalo ndani yake, zimo ofisi za vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Vilevile, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi katika Soko la Kisutu ambalo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara 1,500 wakati awali lilihudumia 669.

Akizungumza katika viwanja vya Mnazimmoja, Rais Magufuli alisema katika suala la kodi, wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao siyo waaminifu, wanawatumia machinga kufanya biashara zao ili kukwepa kodi.

"Mfanyabiashara anakuwa na stoo halafu anapeleka biashara kule. Unakuta anayefanya biashara kweli siyo machinga, bali ni mfanyabiashara mkubwa na mali ni za mfanyabiashara, siyo machinga.

"Ninatoa wito kwa TRA (Mamlaka ya Mapato) ambao wakati mwingine wamekuwa wakitoa makadirio makubwa sana kwa wafanyabiashara na wafanyabiashara wanaacha au wanatafuta mbinu nyingine ya kukwepa kodi, mfuatilie," aliagiza.

Rais Magufuli aliitaka TRA ijifunze katika kutoa haki kwa wafanyabiashara ambao wana nia nzuri ya kulipa kodi.

"Ninaamini yote yakienda kwa pamoja, tutafanikiwa kwa sababu saa nyingine TRA nako kuna wafanyakazi ambao ni wala rushwa. Anakwenda anakukadiria cha juu sana ili ukishindwa kile utakachokuwa nacho ugawane naye.

"Lazima TRA wajirekebishe, nitoe wito kwa Wizara ya Fedha na Mipango, mkasimamie haya kwa sababu tunahitaji kodi, tunahitaji ushuru, lakini uwe wa haki kwa watu wanaolipa," aliagiza.

Vilevile, alisema amepokea malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu gharama za uzoaji taka ambazo ni kati ya Sh. 20,000 hadi 250,000.

"Maduka ya vifaa vya ujenzi hutozwa Sh. 50,000, maduka ya dawa hutozwa Sh. 200,000. Ninajua jiji limepatikana, malalamiko mengine yatafanyiwa kazi ili kurekebisha," alisema.

Rais Magufuli alisema lipo tatizo la wafanyabiashara kuacha kutoa risiti na kuweka bei tofauti kwa bidhaa zinazokatiwa risiti na zisizokatiwa risiti na kuviagiza vyombo husika visimamie suala hilo.

"Wafanyabiashara kuweni waaminifu unapotoa risiti ndogo wakati mtu kalipa kingi, ni wizi! Fedha zinazohitajika ndizo zinatumika kwa ajili ya maendeleo," alisisitiza.

Alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo, kuhakikisha vitambulisho vya wajasiriamali wadogo vinatolewa.

Kuhusu Soko la Kisutu na mengine yanayojengwa, Rais Magufuli alisema yanawawezesha wakulima wauze bidhaa zao kwa bei nzuri.

Alisema masoko hayo pia yanaiwezesha serikali kufahamu matatizo ya wafanyabiashara kwa kufanya tathmini ya uzalishaji na matumizi kwa walaji.

"Mpaka sasa masoko yaliyojengwa ni 24, yapo yaliyokamilika na mengine bado, yanajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 119.9. Tumejenga pia stendi karibu 18, haya yote ni katika kuboresha miji yetu.

"Soko la Kisutu ni miongoni mwa miradi saba inayotekelezwa Dar es Salaam, masoko mengine ni Magomeni, Tandale, Kibada, Mburahati, Machinjio Vingunguti na Kituo Kikuu cha Mabasi Mbezi Luis," alisema.

Alisema Soko la Kisutu litakapokamilika litakuwa na vizimba zaidi ya 500 na machinjio ya nyama, kuku, migahawa, mama lishe na baba lishe, huduma za kibenki na maegesho ya magari 43 kwa wakati mmoja na ofisi za huduma nyingine.

Habari Kubwa