JPM awapa mtihani Jafo na mkurugenzi

25Feb 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
JPM awapa mtihani Jafo na mkurugenzi

RAIS John Magufuli amekubali Kituo Kikuu cha Mabasi Mbezi Luis jijini Dar es Salaam kuitwa jina lake kwa masharti kwamba watendaji wahakikishe hakuna ukandamizaji wa wananchi wanyonge ambao mara zote anawatetea.

Akizindua kituo hicho jana, jijini humo, kilichojengwa kwa Sh. bilioni 50.95, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo, na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, kuhakikisha machinga hawafukuzwi kituoni.

Alisema kituo hicho kitahudumia mabasi 3,454 yakiwamo 1,000 yatakayolala na kina maegesho ya magari madogo 280 na kuagiza kuwapo pia maegesho ya bodaboda.

"Nimeshangaa Jafo kuandika stendi hii kwa jina langu kwa sababu angeandika Jafo Bus Stand, sifurahii majina yangu kutumika kwa sababu ninaogopa kitu kimoja mnaweza kuandika jina Magufuli halafu wananchi maskini, machinga wakawa wananyanyaswa hapa.

"Mara nyingi sina uhakika hapa, vitu vizuri vinavyotengenezwa vinapokamilika, machinga wanafukuzwa, watu wa kawaida wanafukuzwa, ndiyo maana nitaumia sana kama wananchi hawa wanyonge kufukuzwa halafu mmeandika jina Magufuli, maana yake Magufuli ndiye anawafukuza. Waziri inawezekana umejichongea kwa kuita stendi Magufuli, ninataka haya yafanyike," aliagiza.

Rais Magufuli alisema ndani ya stendi hiyo, kuna Ofisi ya Idara ya Uhamiaji, hoteli, nyumba za kulala wageni ambazo hana uhakika kama zitamgusa mmachinga.

"Nitoe wito waziri na mkurugenzi, mmenipa jina nimelikubali kwa ajili ya kuwatetea hawa watu. Ninataka niwe balozi wao kama mnataka hivyo. Ninataka stendi itapoanza, machinga wasifukuzwe kwa sababu ni kwao," aliagiza huku akishangiliwa.

Alisisitiza kuwa wasifukuzwe kwa sababu stendi hiyo kuna mabasi 3,000 ambapo abiria wanaotaka kununua chakula cha hoteli au machinga, wafanye hivyo. "Serikali ninayoiongoza, ni kwa ajili ya Watanzania wote hasa wanyonge. Watendaji mnaohusika, wananchi hawa waruhusiwe.

"Mtengeneze mbinu baadaye, mabasi yanapokuja, mtu anakimbia pale pembeni ananunua bidhaa zake, hapo ndipo tunapojenga Dar es Salaam yenye upendo, isiyokuwa na ubaguzi wa mtu yeyote.

Rais Magufuli alisema hataki kuona madalali wakiwadhulumu wananchi kwenye stendi hiyo na kumwagiza Waziri Jafo kulisimamia suala hilo.

"Nitashangaa siku moja nije hapa nikute stendi imechafuka, imeandikwa maandishi, haitamaniki wakati mmeeleza stendi itapokea magari kutoka nchi za jirani - Zimbabwe, Malawi, Kenya, Uganda na sehemu zingine, hii ni stendi ya kimataifa, sura ya kimataifa, lazima iendelezwe.

"Watakaotumia waitunze, kitunze kidumu, kwa hili nina uhakika tutajenga Tanzania mpya, nani alitegemea Kibamba kuwe na stendi nzuri kama hii? Miaka 60 hakujajengwa stendi kama hii, hakujajengwa 'fly over' kama ya Mfugale," alisema.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alitoa eka 52 za Wizara ya Kilimo zilizopo Jimbo la Kibamba baada ya Mbunge wake, Issa Mtemvu, kumwomba kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na kuagiza zikabidhiwe ndani ya siku tatu.

Kiongozi huyo wa nchi pia alisema barabara nyingi za Ubungo hazijajengwa kwa lami na kubainisha kuwa hakuwahi kuombwa kufanyika kwa ujenzi huo.

"Walikuwa hawapo waliokuwa wanaomba, nimeshangaa kusikia barabara za lami katika jimbo lako ni kilometa tano tu, huwezi kuamini kama kulikuwa na viongozi na wabunge wanaowawakilisha watu.

"Nitasaidia kuongeza barabara, Mtendaji Mkuu upo hapa, pita uniletee mapendekezo tuone barabara ipi tujenge kwa lami.

"Unapata raha unapoombwa kwa lugha nzuri. Mtu unaombwa kwa kutukanwa na wewe unamtukana kwa kumnyima mradi kwa sababu unaowaomba siyo malaika.

"Ni malaika ambaye anaweza kutukanwa bado akakusamehe, lakini kwa binadamu mwenye moyo, anahitaji kuombwa kwa unyenyekevu. Suala la maji, barabara na mengine, wanaohusika shughulikieni," aliagiza.

Habari Kubwa