JPM: Huu ndiyo ukweli

22Feb 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM: Huu ndiyo ukweli

RAIS John Magufuli ametaka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya.

Rais Dk. John Magufuli akizungumza jambo na Padre Dk. Alister Makubi, baada ya kushiriki katika Ibada ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresima katika Kanisa Katoliki
Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

Vilevile, kiongozi huyo wa nchi amesema serikali haijazuia matumizi ya barakoa katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, bali wachukue tahadhari kwa kutumia zilizotengenezwa nchini zikiwamo za Bohari Kuu ya Dawa (MSD) au zilizotengenezwa na Watanzania wenyewe.

Amesema matumizi ya barakoa kutoka nje ya nchi huenda yakawa na madhara kwa kuwa bidhaa hizo zinazoingizwa kutoka ughaibuni, zina shaka ya kuwa siyo salama.

Raia Magufuli pia amewashukuru Watanzania kupitia madhehebu yao ya dini kwa kuitikia wito wa maombi na kufunga ili Mungu aepushe ugonjwa huo wa corona unaosababisha vifo vya watu duniani na kutoa wito kwa Wakristo ambao wapo katika kipindi cha Kwaresma na Waislamu wanaokaribia kuingia katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani, kuendelea kumwomba Mungu.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana kanisani kwenye Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam, alipoungana na waumini wa kanisa hilo kusali Misa Takatifu ya Jumapili.

Alisema Watanzania waendelee kumwomba Mungu kwa kuwa pamoja na jitihada za kibinadamu za kukabiliana na ugonjwa huo, Mungu ndiye muweza wa yote kuhusiana na kila jambo.

Pia, alisisitiza matumizi ya njia za asili ikiwamo za kujifukiza katika kukabiliana na magonjwa ya kupumua ikiwamo ugonjwa huo wa corona.

Aliwataka Watanzania kuondoa hofu inayopandikizwa ambayo ina madhara zaidi na kusisitiza kuendelea kumwamini na kumtanguliza Mungu kwa kuwa njia za kujikinga kwa barakoa, kutogusana na kutokaribiana pamoja na kujifungia majumbani, zimeonekana kutokuwa suluhisho la uhakika.

Alisema mataifa yanayofanya hivyo, watu wake wanapoteza maisha kwa maelfu kulinganishwa na Tanzania.

"Huu ndiyo wakati wa kushikamana kikamilifu na kumtanguliza Mungu tukiwa tunachukua tahadhari. Watu wangefurahi hata Watanzania wote wakifa, mnaweza kuletewa hata barakoa zenye corona, unaivaa kumbe unapata corona ili ukaambukize Watanzania wengine, ni lazima tutumie busara kwa barakoa tunazozivaa.

"Kama alivyozungumza jana Waziri Mkuu, hatujazuia kuvaa barakoa, lakini tuwe waangalifu na ndiyo maana mnamwona hata Waziri Mkuu hakuwa amevaa barakoa jana, mmemwona Makamu wa Rais hajavaa barakoa, siyo kwamba hawaogopi kufa, wote tunaogopa kufa lakini angalau tunaamini kwamba Mungu yupo na tuwe waangalifu katika janga hili, otherwise (vinginevyo) tutaangamia wote.

"Sijasema msivae barakoa, wala msininukuu vibaya, lakini zipo ambazo siyo nzuri, ninataka niwaambie huu ndiyo ukweli; mtaletewa barakoa zingine ambazo ndizo zenye matatizo.

"Mimi ni kiongozi wenu, ninajua mengi, ni lazima niwaambie ukweli. Ukitaka kuvaa barakoa, kavae zilizotengenezwa na Wizara ya Afya au MSD, ukishindwa za namna hiyo, shona yako mwenyewe. Kachukue kitambaa hata kama ni kanga, ikunje hata mara tano, ninawaambia ndugu zangu, mimi ni mwenzenu, ninaifahamu hii ni vita," alionya.

Rais aliwaomba Watanzania kuacha kuogopa kwa kuamini kwamba Mungu yupo na anaweza kila kitu.

"Msifikiri tunapendwa mno, vita ya uchumi ni mbaya na ndiyo maana ninawapongeza watu waliovaa barakoa za kujitengenezea wao.

"Hizi tunazonunua madukani, tunajiua wenyewe, ni lazima niliseme, watatukana lakini nina wajibu wa kusema ukweli.
"Hebu tutaje ni nchi gani ambayo watu hawajafa na corona? Maelfu wanakufa, kuna nchi iliwahi kupoteza watu elfu tatu kwa siku moja na wanavaa barakoa na saa nyingine wanavaa mbilimbili.

"Sisi tuchukue tahadhari za kiafya kama ambavyo inatangazwa, tumtangulize Mungu lakini pia tutafute mbadala ikiwa ni pamoja na kujifukiza," alisisitiza.

Rais Magufuli alitaja baadhi ya dawa ambazo zimekuwa zikitumiwa hospitalini ambazo alisema  zimesaidia wengi kuwa ni pamoja na dawa ya Bupiji, Covidol na kuwasisitiza wananchi kujifukiza.

"Kuna Covidol, kuna dawa za kila aina wanazitumia Watanzania. Ninawaomba ndugu zangu Wakristo na Watanzania, tutoe hofu ya corona, tutapita!

"Mungu akiamua, hata bila corona utakwenda, kwa malaria utakwenda, hata kwa saratani, kwa ajali ya gari au hata kwa kutembea tu utakwenda. Sisi wakati huu ndiyo wa kumwomba Mungu kwelikweli," alisema.

Rais Magufuli alisema kama ambavyo Tanzania ilivuka mwaka jana, ndivyo itakavyovuka na mwaka huu.

"Mwaka jana tulipita salama mpaka watu wakawa wanatushangaa, hata marais wenzangu wakawa wananiambia 'ninyi ni wachawi huko Tanzania?' nikasema mchawi ni Mungu.

"Wapo walioathirika kidogo, lakini tulipita na sasa tutapita. Inawezekana tumekosea mahali, wapo waliotoka nje ya nchi wakaenda kuchanjwa kule, wakapewa haya magonjwa.

"Na wengine watakaoeneza corona katika nchi hii ni wale wanaovaa barakoa ambazo hawajui zimetoka wapi. Lakini ni lazima pia tujiulize, barakoa inatakiwa ivaliwe kwa saa nne?

"Siku ina saa 24, maana yake tunatakiwa tubadilishe barakoa sita. Hebu jiulize, ni wangapi watakaoweza kubadilisha idadi hiyo kwa hizo saa na tuko watu milioni 60? Ni miujiza ya Mungu tu ndiyo itafanya kazi.

"Ninataka niwape moyo ndugu zangu Watanzania, njia tunayotumia ya kumtanguliza Mungu ndiyo itakayotuokoa.
Tusimame na Mungu wetu, kila mmoja katika imani yake tutafika. Tuchukue tahadhari zinazotolewa na madaktari, lakini tusimsahau Mungu kamwe, tutashinda.”

Hadi jana saa 9:09 alasiri, watu milioni 111 waliokuwa wameambukizwa virusi hivyo duniani, milioni 62.7 wakipona huku milioni 2.46 wakipoteza maisha.  Tanzania iliripoti kupata mgonjwa wa kwanza wa corona Machi 16 mwaka jana.

Habari Kubwa