JPM kuigeuza Mwanza kitovu cha biashara

08Sep 2020
Gwamaka Alipipi
MWANZA
Nipashe
JPM kuigeuza Mwanza kitovu cha biashara

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema atahakikisha Jiji la Mwanza linakuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Maziwa Makuu.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wake wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mkuu katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza jana. PICHA: IKULU

Amesema tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, alijikita kuimarisha miundombinu ya usafiri, huduma za kijamii zikiwamo maji, elimu, afya na umeme katika jiji hilo.

Aliyasema hayo jana katika uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza akiomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Magufuli alisema katika kuhakikisha Jiji la Mwanza linakuwa kitovu cha biashara, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza umefanyika kwa kilometa 3.5, ili kuziwezesha ndege kubwa kutua.

“Katika mipango ya miaka mitano ijayo kama nitachaguliwa tutanunua ndege zingine tano, ambazo zingine zitakuwa zinatoka Mwanza kwenda moja kwa moja Ulaya.”

“…Ukipanda hapa unakwenda moja kwa moja Jiji la London, Uingereza, ukitoka London unateremka Mwanza. Hiyo ndiyo dhamira yetu tuliyoipanga.”

Dk. Magufuli alisema katika kutimiza hilo, mkakati uliopo ni kuhakikisha meli za MV Mwanza na Victoria zinaanza kufanya safari kutoka Mwanza-Kemondo-Uganda-Kisumu-Musoma, kisha zirudi Mwanza, lengo ni kuwawezesha wananchi wa Mwanza kutengeneza pesa pamoja na kupanua biashara.

Pia ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Isaka hadi Mwanza utapanua fursa za kibiashara kwa wananchi wa jiji hilo pamoja na kukuza kipato.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika Jiji la Mwanza katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake, alisema ujenzi wa barabara kutoka Nyakato-Veta-Busheru, Makongoro-Mwaroni, ujenzi wa Daraja la Furahisha pamoja na stendi ya Nyegezi.

Kwenye usafiri wa majini, Dk. Magufuli alisema serikali imekarabati chelezo, ukarabati na ununuzi wa meli mpya, pamoja na kukarabati vivuko vya Mv Mara na Ilemela.

Kwenye sekta ya anga, Dk. Magufuli alisema, serikali imenunua rada kubwa, ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege Mwanza pamoja na eneo la kuhifadhia minofu ya samaki.

Kwenye sekta ya afya, Dk. Magufuli alisema serikali imeboresha huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufani ya Sekou-Toure, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa saratani, pamoja na ujenzi wa miundombinu katika afya kwa gharama ya Sh. bilioni 11.4.

Kuhusu elimu, Dk. Magufuli alisema serikali imejenga nyumba za walimu, madarasa, mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa shule kongwe, pamoja na kutoa Sh. bilioni 53.7 kufanikisha huduma ya elimu bure mkoani Mwanza.

Kwenye maji, Dk. Magufuli alisema zaidi ya Sh. bilioni 92 zimetumika kufanikisha miradi ya maji Nansio, Magu na Misungwi. Alisema vijiji 144 vimeshafikiwa na huduma ya umeme, huku Sh. bilioni 30 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya kumalizia vijiji vilivyosalia.

Sekta ya madini, alisema serikali imetoa leseni 147 kwa wachimbaji wadogo, ujenzi wa kiwanda cha kusafishia madini chenye uwezo wa kusafisha kilo 300 kwa siku.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano kupitia sheria mpya ya madini na kulinda rasilimali ilipitishwa pamoja na kufikia makubaliano na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick ya kuanzisha kampuni mpya ya Twiga.

Katika kampuni hiyo, Barrick wanamiliki asilimia 84 na Tanzania 16, na faida itakayopatikana itagawanywa asilimia 50 kwa 50.

Habari Kubwa