JPM kulivunja Jiji la Dar es Salaam

25Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM kulivunja Jiji la Dar es Salaam

RAIS John Magufuli ametangaza atalivunja Jiji la Dar es Salaam muda wowote kuanzia sasa na kulihamishia kwenye Manispaa ya Ilala, ili fedha zilizokuwa zinatumika, zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo.

Alitangaza kusudio hilo jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa makutano ya barabara Ubungo jijini ambayo ujenzi wake umegharimu Sh. bilioni 252.642 huku Sh. bilioni 8.375 zikitumika kuwafidia wananchi waliopisha mradi huo.

Rais Magufuli alisema amekusudia kufanya mambo makubwa katika Jiji la Dar es Salaam, ili liwe na hadhi inayostahili.
"Kwa wana Dar es Salaam ninategemea kufanya mabadiliko kidogo ya kuwa na Manispaa ambazo zinawakilisha maeneo.

Ninategemea kulivunja Jiji la Dar es Salaam, tutengeneze jiji la eneo fulani, tunaweza kuifanya Ilala kuwa jiji.

Rais Magufuli aliwataka wale waliokuwa wanataka nafasi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, wajiandae kisaikolojia kwa sababu meya atapatikana Manispaa ya Ilala au manispaa mojawapo.

"Huu ndiyo kweli na rasimu nimeshaletewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleman Jafo. Nikitoka hapa, nitakwenda kutia saini, ili turahisishe mambo.

"Bajeti ya Jiji ambayo haipo, fedha zilikuwa zinapotea, waheshimiwa wabunge, Ilala inafaa kuwa Jiji. Ubungo mtasubiri kwa sababu hata barabara hazijatengenezwa," alisema.

Rais Magufuli alisema anafanya hivyo kwa kuangalia matumizi mazuri ya fedha na kusisitiza lazima Dar es Salaam liwe jiji la kisasa.

"Kuwa na madiwani ambao wanakaa juu wanachangiwa fedha, wanakula posho, hili nitalikataza. Ninazungumza hapa, wale wanaojiandaa kuwa mameya wa Jiji la Dar es Salaam halafu wanakaa hawana maeneo, wajue hilo limekwisha," alisema.

Rais Magufuli alisema wanataka manispaa moja katika Jiji la Dar es Salaam ndiyo ipandishwe hadhi ya kuwa jiji kisha zingine zibaki kuwa manispaa.

Alisema wanafanya hivyo kama ilivyo kwenye majiji mengine na kutolea mfano Mwanza na Dodoma.

"Unapokuwa na manispaa nne au tano halafu unakuwa na madiwani hawawakilishi yoyote, wanawakilisha kwenye manispaa zao, halafu wanatengewa bajeti, hizo fedha ni vizuri zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo ya barabara. Haya ndiyo matumizi bora ya fedha za walipakodi," alisema.

Rais alisema wamejipanga kuboresha maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kuahidi wananchi wa mkoa huo wataona barabara nyingi za juu.

"Ninataka kuwahakikishia wana Dar es Salaam, ninajua makao makuu Dodoma, Dar es Salaam sitaiacha, nitajenga hata barabara za mitaa, miaka mitano iliyopita, tumefanya mageuzi makubwa katika mitaa yenu.

"Amezungumza Mkuu wa Mkoa, tumetumia Sh. trilioni moja kufanya mabadiliko makubwa katika mitaa, nenda Mbagala utakutana na lami, Sinza utakutana na barabara nne, hapa tumetandika barabara nane, wengine wanasema ni pana mno," alisema.

DARAJA LA BALOZI KIJAZI

Rais Magufuli alipendekeza daraja hilo liitwe Balozi John Kijazi ambaye alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, aliyefariki dunia wiki iliyopita.

"Balozi Kijazi alifanya kazi kwa uadilifu na miradi yote ya Dar es Salaam ikiwamo masoko, stendi alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Alikuwa kiongozi baraza na alichangia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa miradi mingi ikiwamo ya barabara.

"Ninafikiri wana Dar es Salaam, mtakubaliana nami Kijazi amefanya kazi kubwa sekta ya barabara, alikuwa hana makuu, alikuwa mkurugenzi wa barabara nchini, baada ya kutoka akateuliwa Mhandisi Patrick Mfugale (Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS).

"Baada ya Mfugale, akaja Alhaji Iyombe na baadaye akawa Katibu Mkuu na Kijazi akawa Katibu Mkuu, Mfugale ameumisi ukatibu mkuu kwa sababu hata umri hawezi kuteuliwa ukatibu," alisema.

Rais Magufuli alisema mchoraji wa madaraja likiwamo hilo la Ubungo ni Mfugale, akifafanua na kutania kidogo akisema:

"Ndiye mtaalamu wa madaraja. Alichora mchoro wa Daraja la Mkapa, Mfugale, Umoja, Busisi, ndiyo maana ninamwombea asife mapema au kujinyonga kwa sababu Wahehe wakishindwa mambo, wanajinyonga.

"Ninataka aendelee kuchora michoro ya madaraja mengine ili Dar es Salaam ibadilike."

Rais Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 60, wanafahamu shida zilizokuwa Ubungo ambapo wapo waliopoteza maisha, ndoa kuvunjika kutokana na foleni iliyokuwapo.

"Wapo waliopoteza maisha yao, ninakumbuka mwaka 2015 wakati wa kampeni, Staff Sajenti alifia hapa kwenye mataa. Mungu aziweke roho za marehemu wote zilizotangulia kwa amani.

Alisema mwaka 2017, alifika hapo na Rais wa Benki ya Dunia (WB) kuweka jiwe la msingi na kwamba walifanya hivyo kwa sababu walihitaji fedha.

"Tungeweza kulijenga daraja, lakini kupanga ni kuchagua ukiwa unaaminika kwenye mikopo, ukikopeshwa na kulipa, Tanzania ni tajiri na matajiri wengi wanakopa na sisi matajiri Tanzania tukaenda kukopa Sh. bilioni 250 ambazo tutaanza kuzilipa," alisema.

Alisema wakati akitoka Posta kwenda Ubungo, alipita barabara ya Mwenge na ameshangaa kuona idadi kubwa ya nyumba za ghorofa Dar es Salaam, akisema sasa baadhi ya mitaa iliyopo inafanana na ya nchi za Ulaya.

Awali, Mfugale alisema kwa siku magari 68,800 yanapita katika makutano hayo na ili kuwezesha kupita, zamani yalikuwa yanatumia zaidi ya saa mbili na nusu kusubiriana.

"Daraja kutoka Kimara kwenda mjini lina urefu wa mita 260 ambalo linaruhusu gari kupita bila kusimama, limenyanyuliwa kwa mita 8.9 kutoka chini. Daraja kutoka Mwenge kwenda Buguruni limenyanyuliwa kwa mita 16.38 ambalo lina urefu wa mita 700," alifafanua.

Habari Kubwa