JPM kuwaachia wahamiaji haramu 1,789 wa Ethiopia

26Jan 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM kuwaachia wahamiaji haramu 1,789 wa Ethiopia

SERIKALI ya Tanzania imesema iko tayari kuwaachi huru wahamiaji haramu 1,789 ambao wamefungwa kwa makosa ya kuingia nchini bila vibali.

Rais Dk. John Magufuli akimpokea mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Ethiopia Sahle-Work Zewde mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Geita mjini Chato jana kwa ziara ya kikazi ya siku moja. PICHA: IKULU

Akizungumza wakati akimkaribisha Rais wa Ethiopia, Zahle Zewde ambaye alitembelea nchini jana kwa ziara ya kikazi ya siku moja, na kufanya mazungumzo Chato mkoani Geita, Rais John Magufuli alisema wako tayari kuwasamehe na kuwarudisha kwao wahamiaji hao haramu bila masharti yoyote.

“Kuna wafungwa 1,789 kutoka Ethiopia ambao ni wale wanaoingia nchini isivyo halali na wamehukumiwa.
Tumezungumza namna ya kupanga mbinu za kuwaruhusu warudi kwao na nimemweleza kwamba hatuna masharti na tunawaruhusu waondoke free (huru),” alisema Rais Magufuli.

“Hao wakimbizi ambao wengine wamekaa zaidi ya miaka saba watarudi kwao na niko tayari kuwaachi hata wale ambao watakuwa wamefungwa leo (jana), ili waondoke, huo ndio undugu.”

Katika mazungumzo yao, viongozi hao walikubaliana mambo mbalimbali ikiwamo kuimarisha uchumi kati ya nchi hizo mbili.

Pia kuimarisha ushirikiano katika majeshi, huku Tanzania ikiahidi kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Adis Ababa nchini Ethiopia.

Makubaliano mengine ni kuimarisha sekta ya mifugo, huku Tanzania ikiomba kujifunza kwa nchi hiyo ambayo inafanya vizuri na kufaidika na mifugo yake.

“Ethiopia ni ya kwanza kwa mifugo Afrika, sisi ni wa pili, lakini yenyewe imefaidika, inatengeneza bidhaa ambazo inaziuza hadi Ulaya, lakini Tanzania bado hatujafaidika, tumewaomba tujifunze kwao, kwa kukaribisha uwekezaji  ili tuone namna ya kuendeleza sekta ya mifugo,” alisema Rais Magufuli.

Jambo jingine ambalo walikubaliana ni kuanzisha vikao vya mazungumzo vya kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo ambavyo wamewaagiza mawaziri husika kushughulikia hilo ili vianze kati ya Machi na Aprili mwaka huu.

Pia Rais Magufuli alisema wameiomba nchi hiyo kuirejeshea Tanzania ardhi ambayo ilinyang`anywa baada ya kushindwa kuiendeleza kwa ajili ya kujenga ubalozi nchini humo, huku Tanzania nayo ikisema tayari imetoa hekta tano za ardhi kwa Ethiopia kwa ajili ya kuendeleza ubalozi wao jijini Dodoma.

“Ethiopia iko juu sana kiuchumi Afrika, na kama sikosei mpaka mwaka jana ulikuwa unakuwa kwa asilimia tisa, kwa hiyo kuna haja kuendeleza uhusiano uliopo ili pande zote zinufaike kiuchumi,” alisema Rais Magufuli.

“Tanzania na Ethiopia zina uhusiano mzuri tangu kuanzishwa kwa Umoja nchi za Afrika na harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na tumeendelea na uhusiano haya ambayo yamenufaisha nchi zetu.”

Rais Magufuli alisema katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo umeimarika.

“Kwenye miaka ya hivi karibuni ushirikiano wa kibiashara umeimarika, mwaka 2016 ulikuwa Sh. bilioni 3.07 na mwaka 2019/2020 umefikia Sh. bilioni 13.55, na kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesajili miradi 13 kutoka Ethiopia yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 14.57 ambazo zimetoa ajira 677,”alisema Rais Magufuli.

Sekta nyingine ambayo alisema wamekuwa wakishirikiana ni katika usafiri wa anga na utalii na kwamba Bodi ya Utalii nchini (TTB) na Shirika la Ndege la Ethiopia zimeingia makubaliano ya matangazo ambayo yamesaidia kuongeza idadi ya watalii Tanzania.

“Tumeshirikiana katika sekta ya usafiri wa anga na utalii, Shirika la Ndege la Ethiopia limekuwa likifanya safari zake katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema Tanzania pia imekuwa ikipata fursa ya masomo katika nyanja za marubani na wahandisi wa ndege na kwamba mpaka sasa marubani 75 na wahandisi wa ndege 20 wamepata masomo nchini humo.

Kwa upande wake Rais huyo wa Ethiopia, alisema nchi yake iko tayari kuongeza ushirikiano ili kukuza zaidi uchumi katika nchi hizo.  

“Tutajitahidi kufanya mikutano kwa kuanza katika kipindi ambacho tumekubaliana ili ushirikiano tunaotaka ambao una mizizi imara katika nchi ya Tanzania uendelee,” alisema Rais Zewde.

Pia alisema wako tayari kuanza kupitia makubaliano ya mikataba yote waliyoifanya katika nchi hizo mbili na kuangalia maeneo mengine mapya ya ushirikiano.

“Tunaona kwamba kuna eneo ambalo liko wazi kwa ajili ya kulijaza hususani katika uwekezaji, tumekubaliana biashara na uwekezaji kwa sababu tunaona kwamba nchi za Afrika lazima ziwekeze Afrika,” alisema Zewde.

Na eneo la mifugo ni la kipaumbele zaidi kwa uwekezaji kwa sababu nchi hizo zinaongoza katika sekta hii.”

Kuhusu suala la kujipanga kuja kuwachukua wahamiaji hao haramu, Rais Zewde aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kuwaachia bila masharti na kwamba watafanya kila njia kuja kuwachukua.

Pia aliishukuru Tanzania kwa kuwapatia walimu wa Kiswahili na kwamba wako tayari kuwapokea.

Habari Kubwa