JPM: Mali za Waislamu ziliuzwa na Waislamu

18Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
JPM: Mali za Waislamu ziliuzwa na Waislamu

RAIS John Magufuli amesema mali za Waislamu ziliuzwa na Waislamu wenyewe.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza katika maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Rais Magufuli alisema uchunguzi uliofanyika kufuatilia mali za Waislamu umebaini baadhi ya mali hizo ziliuzwa kinyemela na Waislamu wenyewe.

Alisema amepewa taarifa na Mufti Mkuu, Sheikh Aboubakar Zubeir kuwa baadhi ya mali hizo zimeanza kurejeshwa.

Katika maadhimisho hayo, Rais alisema serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa na midogo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme katika Mto Rufiji, maarufu Stiegler's Gorge na ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.

Rais Magufuli pia alisema serikali inaendelea kukarabati reli ya zamani huku ikijenga reli ya kisasa kwa ajili ya treni ya umeme.

Alisema serikali pia inajenga meli kwenye maziwa makuu nchini ili kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi huku serikali yake ikiongeza bajeti ya sekta ya afya na kujenga mamia ya vituo vya afya na hospitali 67 za wilaya.

"Kila eneo tunaligusa. Tuna pesa kwa sababu tumebana mafisadi. Hizi fedha zilikuwa zinapotea kwenye mikono ya watu wachache na tumeondoa pia watumishi hewa," alisema Rais Magufuli.

"Tumechoka kuitwa nchi maskini. Tanzania ni tajiri na Watanzania ni matajiri. Ndugu zangu, tuna wajibu wa kuitunza amani yetu."

Rais Magufuli pia alimpongeza Mufti Zubeir kwa uongozi mzuri akimwelezea kuwa ni kiongozi wa kipekee.

"Leo (jana) nitoe siri ambayo sijawahi kuitoa. Mzee (Jakaya Kikwete (Rais wa nne wa Tanzania) alipopata msiba kule Msoga, nilienda kumpa pole.Tulipokuwa malaloni, nilipokuwa nikichungulia kule chini, nikamwona Mufti akihangaika kutoa udongo kwenye kaburi.

"Nikasema huyu ni mtu wa pekee, sijawahi kumwona Padri au Askofu anaingia kaburini. Huyu ni mtu tofauti, wakati mwingine hata watu wazuri hawakubaliki ndani ya taasisi zao. Katika kipindi cha miaka mitatu umewaunganisha Waislamu na Wakristo wa Tanzania."

Katika maadhimisho hayo, Rais Magufuli alitoa zawadi ya Sh. milioni 30 kwa Bakwata kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Habari Kubwa