JPM, Museveni wasaini mkataba bomba la mafuta

14Sep 2020
Gwamaka Alipipi
Chato
Nipashe
JPM, Museveni wasaini mkataba bomba la mafuta

SERIKALI za Tanzania na Uganda jana ziliingia makubaliano ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi mkoani Tanga, huku Tanzania ikitarajia kuchukua asilimia 60 ya faida itakayopatikana katika mradi huo.

Vilevile, Tanzania inatarajia kunufaika kwa kupata Dola za Marekani milioni 363 (sawa na Sh. trilioni 7.5), zitakazotokana na makusanyo ya kodi kwa kipindi cha miaka 25.

Utiaji saini wa makubaliano ya utekelezaji huo ulifanyika jana mkoani Geita, wilayani Chato kati ya Rais John Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Akizungumza baada ya mchakato huo, Rais Magufuli alisema mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 (Sh.tilioni 7.8), Tanzania itapa faida mbalimbali ikiwamo kutengeneza ajira za moja kwa moja 10,000 hadi 15,000, kuvutia wawekezaji, kukuza ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia kukuza ushoroba wa Kaskazini, zikiwamo nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi.

“Mradi huu utaleta faida nyingi sana, ni bomba refu zaidi duniani likiwa na urefu wa kilometa 1,415 na teknolojia ya kisasa ya kusafirisha mafuta yakiwa na joto. Kilometa 330 zitakuwa Uganda, kilometa 1,115 zitakuwa Tanzania,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Kwa upande wa Tanzania bomba hili litapita katika mikoa nane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara, Tanga, pia litapita katika wilaya 24, kata 132, pamoja na vijiji 186, kote huko litatoa ajira,” alisema Rais Magufuli.

Kadhalika, alisema wakazi zaidi ya 90,000 watakaoguswa na utekelezaji wa mradi huo watalipwa fidia ya Sh. bilioni 21 ili kupisha ujenzi.

“Rais Museveni amefanya mambo makubwa yasiyowezekana Afrika Mashariki kwa kugundua mafuta, haya mambo tulikuwa tukiyasikia tu katika nchi za uarabuni…yawezekana mazuri uliyoyafanya ukaambulia matusi, lakini ninachokusihi wewe chapa kazi na uwasamehe,” alisema Rais Magufuli.

Matokeo ya mradi huo alisema utawezesha uchumi wa Uganda na Tanzania kukua, pamoja na kuongeza undugu baina ya nchi mbili.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, alisema ulikwamishwa na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, na kwamba juzi alipigiwa simu na Rais Museveni akielezwa kukamilika kwa mazungumzo na kuomba makubaliano ya utekelezaji yafanyike.

Rais Magufuli alisema: “Baada ya kupigiwa simu na Rais Museveni na kuomba kuja Tanzania, nikamwambia njoo hata kesho, akaniambia atakuja na barakoa, nikamjibu wewe njoo hata na branketi uje kulala huku huku…Huu ni ushindi wa pili wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uganda baada ya ule wa awali wa kumwondoa Iddi Amini.”

Naye Rais wa Museveni alisema wataalamu wazawa ndio waliogundua hazina hiyo ya mafuta yapatayo mapipa bilioni 6.1.

“Tulitumia wataalamu wetu kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho, watu wa nje (wazungu) walikuwa wanatuchezea. Tulichokifanya tuliwachukua wazawa wetu waliosomea masuala ya Geology (elimu ya miamba), Geo-Physics, Chemistry (kemia) katika vyuo vikuu vya jijini London, Romania, Algeria, ambao wakasomea uzamili wa masuala ya mafuta,” alisema Rais Museveni na kuongeza:

“Mwaka 2006 ndiyo tuligundua mafuta hayo, muda mwingi wataalamu wangu walikuwa wanavutana na kampuni za kigeni juu ya kodi tutakayopata,” alisema Rais Museveni.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof. Adelardus Kilangi, akitaja makubaliano matatu yaliyomo katika mkataba huo kuwa: Mosi ni kila nchi kuchukua hatua za haraka kati yake na kampuni husika zitakazohusika katika mradi huo.

Pili, kila nchi kukamilisha kwa haraka mashauriano ya mikataba midogo itakayotakiwa kutekelezwa, tatu ni kila nchi kuchukua hatua ili kuwezesha utekelezaji wa haraka wa bomba la hilo la mafuta.

Habari Kubwa