JPM, Shein wakutana kikao cha ndani Dodoma

04Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
JPM, Shein wakutana kikao cha ndani Dodoma

RAIS Dk. John Magufuli na Mwenyekiti wa CCM Taifa, jana amekutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, katika kikao cha ndani kilichofanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu Chamwino, ilisema kikao hicho kimehudhuriwa na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bashiru Ally, kuzungumzia masuala ya chama hicho.

Taarifa hiyo ilisema, baada ya kikao hicho, Rais Shein alikwenda kuweka udongo katika jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za Ikulu na kukagua maendeleo ya kazi ya ujenzi wa ofisi hizo inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia shirika lake la Suma JKT.

Rais Shein alimshukuru Rais Magufuli kwa kumpa fursa ya kwenda kuweka udongo ikiwa ni kumbukumbu ya ujenzi wa ofisi hizo na kubainisha kuwa kujengwa kwa ofisi hiyo ni heshima kwa taifa na tafsiri sahihi ya kujitawala.

“Huko ndio kujitawala, kutawaliwa sio kuzuri, mtawala anafanya anavyotaka yeye, anafanya kwa utashi wake pale anapotaka yeye kufanya, tunapochukua hatua ya kujitawala wenyewe tunafanya mambo makubwa kama haya kwa ajili ya wananchi, hii ofisi ni ya wananchi wa Tanzania,” alisema Rais Shein.

Habari Kubwa