JPM: Tusihukumu

12Aug 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
JPM: Tusihukumu

RAIS John Magufuli amewaasa Watanzania kuacha kutoa hukumu kwa tukio la ajali ya gari la tangi la mafuta iliyotokea juzi eneo la Msamvu, mkoani Morogoro na kuteketeza maisha ya watu kwa moto na wengine kujeruhiwa.

Rais John Magufuli akiwajulia hali majeruhi wa ajali ya moto ambao wamelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili mara baada ya kusafirishwa kutokea mkoani Morogoro. PICHA: IKULU

Alisema sio kila aliyekutwa na ajali hiyo alikwenda kuiba mafuta.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipotembelea majeruhi wa ajali hiyo, waliohamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kuwajulia hali na kuwapa pole.

"Tusiwe wepesi wa kuhukumu, kutoa hukumu ni kitu kibaya! Tuvumilie! Hili lingeweza kumpata mtu yeyote, tushikamane katika hili, tumtangulize mbele Mungu, ni majaribu ya shetani na siku zote shetani atashindwa nasi tuendelee kuwa taifa moja," alisema huku wananchi wakiitikia, amina.

"Niwaombe Watanzania tuendelee kuwaombea huu si wakati wa kuwalaumu, kwa sababu nimekuwa nikisia baadhi ya watu wakisema kuwa walikwenda kuiba mafuta. Nimemwona dereva alisimamisha gari kwenda kumsaidia mwenzake, amefika moto ukalipuka, mwingine alikuwa anasafiri kwenda Mtwara amezuiwa moto ukalipuka akaungua," alibainisha.

"Niwaombe sana sana Watanzania wenzangu tusiwe na majibu ya haraka, hii ni kazi ya Mungu tujitahidi kuwaombea wagonjwa na marehemu wapumzike kwa amani," alisema na kuongeza:

"Sisi tusiwe majaji kwa sababu si kila aliyekuwapo pale alikwenda kuchukua mafuta, wapo waliokwenda kuokoa, wapita njia na safari zao wakapatwa na dhahama hizo," alisema.

Kufuatia ajali hiyo, Rais Magufuli amesema serikali itagharamia matibabu ya majeruhi wote huku akitoa Sh. 500,000 kwa kila mgonjwa aliyekuwa anajitambua na Sh. milioni moja kwa wagonjwa wengine  huku Sh. milioni mbili akitoa kwa wauguzi, manesi na madaktari.

Katika kila wodi aliyoitembelea Rais Magufuli alikwenda katika kila kitanda na kutoa pole ya maneno ya faraja pamoja na fedha, huku akiongea na wagonjwa, kuuliza majina yao na kwa wale wasiojiweza alitaka kutajiwa majina yao.

Aliwatembelea majeruhi katika wodi za Mwaisela, Sewahaji, Chumba cha Wagonjwa Mahututi na chumba cha dharura, na baadaye alizungumza na wananchi waliokusanyika nje ya hospitali hiyo.

Rais aliwapongeza wauguzi na madaktari kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuokoa maisha ya watu na kuwaomba Watanzania kuendelea kuwaombea kwa sababu wengi wamepata majeraha makubwa ya kuungua.

SERIKALI KUGHARAMIA MATIBABU

Rais Magufuli aliagiza majeruhi wote wahudumiwe kwa gharama yoyote na serikali itagharamia matibabu yote kwa sababu ni Watanzania maskini ambao hawakuitaka ajali na kwamba imetokea kwa bahati mbaya.

Baadaye Rais Magufuli aliongea na ndugu wa majeruhi hao na kuwasihi wamtangulize Mungu na kuwaombea na kurudia kusisitiza watu kuacha kuhukumu.

"Niwaombe Watanzania kazi ya ajali tusiwe wepesi wa kuhumu, nimeona watu ambao hata si wa Morogoro akiwamo dereva wa gari jingine aliyekwenda kutoa msaada na aliyekuwa anasafiri kwenda Mtwara," alisema.

Awali Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Juma Mfinanga, alisema walipokea majeruhi 46, kati yao watatu walifariki, wanane wamelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) wakisaidiwa kupumua kwa mashine baada ya kupata madhara kwenye mapafu, na wengine wameungua zaidi ya asilimia 70 hadi 100.

Alisema majeruhi wengine wamelazwa chumba cha dharura na wengi wameungua kwa zaidi ya asilimia 80.

"Sisi kama wauguzi tunafanyakazi kwa kila hali kuwahudumia kuhakikisha wanarejea kwenye hali zao. Majeruhi 15 ambao wameungua chini ya asilimia 10 wamebaki Morogoro kwa kuwa baada ya tathmini yetu tumeona Hospitali ya Rufani Morogoro inaweza kuwahudumia," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru, alisema wagonjwa 43 mahitaji yao ni mengi kwa kuwa wamepata majeraha makubwa ya moto.

Alisema hospitali itatoa huduma zote muhimu kwa majeruhi wawili ambao wameumia kwa asilimia 95 hadi 100.

"Tunawafanyakazi kutoka jeshi, madaktari wetu, tuna wauguzi 60 na tumepata wanafunzi manesi kutoka Muhas, imesaidia sana kuhakikisha huduma sahihi zinafanyika kwa majeruhi," alisema.

JPM WODINI

"Poleni sana tunawashukuru kwa yote mnayoyafanya, Mungu awajalie, tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu," alisema Rais.

Aliwatembelea wagonjwa watatu walioungua kwa asilimia 90 hadi 95, waliolazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Mgonjwa mmoja ameungua kwa asilimia 95 na kubaki sehemu ya kichwa na mwingine ameungua sehemu za mapafu.

"Tunawashukuru sana kwa huduma mnazozitoa, Mungu aendelee kuwajalia, na awajalie uponyaji wagonjwa wote," alisema.

Akiwa kwenye wodi ya Sewahaji, alimtembelea mgonjwa Lucas na kumwambia: "Mimi nimekuja kukusalimu, Mungu akusaidie Lucas, pole sana! Nashukuru baba yangu, Mungu akubariki," alisema na kisha kumpa Sh. 500,000.

Naye, Rajabu Mtita ambaye alisema alikuwa mpita njia kwenye eneo la tukio na moto kumfuata, alitumia dakika chache kumsifia rais kuwa anamwelewa na kumkubali.

MGONJWA AOMBA KITAMBULISHO

Mtita alitumia fursa hiyo ya kuongeza na Rais kwa kueleza suala la upatikanaji wa vitambulisho vya uraia lilivyo gumu na rais alimtaka apone kwanza ndiyo atashughulikia suala hilo.

DEREVA ALIYEUNGUA

Rais Magufuli pia alimtembelea Shaban Maliganya, ambaye alijitambulisha kuwa ni dereva wa lori, aliyekwenda kwenye gari lililoanguka kwa ajili ya kutoa msaada na moto kulipuka.

MAMA LISHE

Alipofika katika kitanda cha Asha Suleiman, ambaye ni mama lishe kwenye eneo hilo la ajali, Rais Magufuli alimpa Sh. 500,000.

Mama huyo alishukuru huku akilia na kusema amekuwa akimtazama Rais kwenye runinga.

Rais alimfariji na kumwambia Mungu ni mwema atamsimamia na atapona.

"Hii hapa itakusaidia nawe hata kununua juisi. Itakusaidia hii hapa Sh. 500,000," alisema wakati akitoa fedha kwa kila mgonjwa.

Pia, aliwapa madaktari na manesi wa wodi ya Sewahaji Sh. 500,000 na wodi ya wanawake Sh. milioni moja.

Katika wodi ya Mwaisela, Rais alipewa maelezo kuwa wamepokea wagonjwa 10 wanaume wenye miaka 26 hadi 50 ambao wanahitaji kupumua kwa mashine na watatu wanatumia Oxygen.

Alijulishwa kuwa hali za wagonjwa hao ni mbaya kwa kuwa wengi wameungua kwa asilimia 80 hadi 90 kwenye njia ya hewa na chakula hali inayowafanya washindwe kupumua.

Akiwa mwenye huzuni Rais alitoa Sh. milioni moja kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa 11 waliokuwapo na Sh. milioni mbili kwa ajili ya wauguzi, manesi na madaktari, huku akisisitiza kuwa hajawahonga fedha hizo.

AIFAGILIA MUHIMBILI

Aliipongeza Muhimbili kwa kuendelea kutoa huduma bora na nzuri, huku akisema kwa sasa wamebadilika na kwamba serikali itakamilisha mambo mbalimbali ambayo inapaswa kuyakamilisha.

"Tunawashukuru sana kwa kuwahudumia watu, Mungu awajalie msikate tamaa, mnafanya kazi ya Mungu tunawashukuru kwa juhudi, tuendelee kuwahudumia huku tukiwaombea kwa Mungu, sisi tunaweza kufanya kwa nguvu zetu, lakini bila msaada wa Mungu haiwezekani,” alisisitiza.

Juzi Rais alitangaza siku tatu za maombolezo na kuagiza bendera kupepea nusu mlingoti kwa kuwa ni kipindi kigumu kwa Watanzania.

Habari Kubwa