JPM: Viongozi wa dini wahamasishe kupiga kura

15Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
JPM: Viongozi wa dini wahamasishe kupiga kura

RAIS John Magufuli amewataka viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kushiriki katika uchaguzi mkuu, hasa siku ya kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu.

Kiongozi huyo wa nchi alitoa rai hiyo alipohutubia mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Kanisa la Asemblies of God (TAG) uliofanyika jijini hapa jana.

Alisema siku ya uchaguzi ni siku ya mapumziko na waendelee kumwomba Mungu wapatikane viongozi wenye maono.

“Wachapakazi na wazalendo kwa taifa letu, tusiangukie mikononi mwa viongozi wabadhirifu, wabinafsi au vibaraka maana kazi ya viongozi kama hao huwa ni kubomoa badala ya kujenga, kung’oa badala ya kupanda na kutawanya badala ya kukusanya,” alisema.

Rais Magufuli alisema ni vyema wakamwomba Mungu awajalie hekima ya kufanya uamuzi sahihi.

“Katika baadhi ya nchi wakati mwingine zoezi la uchaguzi limekuwa chanzo cha kuzuka kwa vurugu na fujo. Kwa msingi huo, niwaombe viongozi wa dini kuliombea na kuliweka mikononi mwa Mungu taifa letu ili tumalize salama uchaguzi wetu huku tukiendelea kubaki na amani, umoja na mshikamano.

“Kwangu mimi ninaliona taifa la Tanzania ni muhimu zaidi kuliko mifarakano ya mambo mengine," alisisitiza.

Aliwahakikishia viongozi hao kuwa serikali imejipanga kuona uchaguzi mkuu unakuwa wa huru na wa haki.

Aliwasihi wanasiasa kufanya kampeni za kistaarabu na kutotumia lugha za kuwatisha wananchi.

“Niwaombe Watanzania tuwakatae wanasiasa wenye kuhubiri chuki na kutoa maneno ya vitisho, wanafanya hivyo kwa sababu hawana sera na wanajua vurugu zikitokea wao wanapo mahali pa kwenda kuishi,” alisema.

“Dini isitugawe, vyama visitugawe, wala makabila yasitugawe, tuishi tukijua tuna Mungu ambaye ni mtawala wa dunia yote, tuna imani kuwa mkisimama tutavuka salama,” alisema.

Rais Magufuli alieleza kufurahishwa na kusanyiko la maaskofu na wachungaji takribani 4,000 waliohudhuria mkutano huo uliodhihirisha uwapo wa Mungu na aliwashukuru viongozi hao kwa kazi kubwa wanayoifanya kuliombea taifa na kutoa huduma za kijamii kupitia shule na vyuo, vituo vya watoto yatima na watoto wa mitaani, miradi ya maendeleo na visima vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.

Pamoja na kulipongeza kanisa hio, Rais Magufuli pia aliahidi kuwa serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu ambao upo kwa mujibu wa katiba na itaendelea kutoa ushirikiano katika juhudi mbalimbali za kanisa hilo kuhudumia jamii ikiwamo ujenzi wa chuo kikuu jijini Dodoma, akimwagiza Mkuu wa Mkoa Dk. Binilith Mahenge kuhakikisha mpango huo unafanikiwa na uwekezaji mwingine wowote ambao kanisa hilo litaona unafaa kuufanya.

“Ninafikiri msiishie tu kujenga chuo, ila mnaweza kutenga eneo lingine ili muanzishe ujenzi wa viwanda, ninawahakikishia kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wenu hivyo tunaahidi kuendelea kushirikiana nanyi kwa karibu sana,” alisema.

Alisema serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ili taasisi za dini kuendelea kuchangia maendeleo ya nchi katika uwekezaji.

Rais Magufuli aligusia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana ikiwamo kukarabati treni ya kwenda mkoani Arusha ambayo ilisimama kwa zaidi ya miaka 20.

“Miradi yote tunayoifanya nchini ni kwa mapenzi makubwa ya Mungu wetu ambaye tuna wajibu wa kumtumikia kupitia kuwatumikia wananchi na kuwatatulia changamoto zao,”alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alishukuru kwa tuzo maalum ya heshima kutoka kwa baraza hilo kwa kutambua jinsi alivyoliongoza taifa kumtegemea Mungu katika kipindi kigumu cha mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapatu inayosababishwa na virusi vya corona, maarufu Covid-19.

Katika mkutano huo, Askofu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la TAG ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Assemblies of God barani Afrika, Dk. Barnabas Mtokambali, alimkabidhi Rais Magufuli tuzo hiyo kutambua namna alivyoliongoza taifa kumtegemea Mungu katika kipindi hicho cha mlipuko wa virusi hivyo.

Habari Kubwa