Jukwaa la Katiba waja na mpya

08Oct 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Jukwaa la Katiba waja na mpya

JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata), limesema limeandaa maandamano ya amani nchi nzima, kumuunga mkono Rais John Magufuli, hususan kwenye usimamizi rasilimali, kupiga vita rushwa na kuondoa watumishi hewa.

Mwenyekiti wa Jukata, Dk. Hebron Mwakagenda.

Aidha, jukwaa hilo limesema kuna haja ya kuyaweka

kwenye Katiba mambo makubwa ambayo Rais ameyafanya ili nchi na Watanzania wa kizazi hiki na kijacho wanufaike.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukata, Dk. Hebron Mwakagenda, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya mkutano mkuu wa dharura uliofanyika mkoani Dodoma.

Alisema ili Rais aache historia kwa vizazi vijavyo ni muhimu mambo yote yawe na msingi wa kikatiba na kuwapo kwa mfumo thabiti isiyoruhusu nchi kuchezewa na watu wachache.

Alisema mkutano huo ulitoa maazimio kwamba maandamano yafanyike Oktoba 30, mwaka huu, na kuhitimishwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kwamba kila wilaya nchini itafanya maandamano.

Alisema lengo la maandamano hayo ni kufikisha ujumbe wa mchakato wa Katiba mpya na kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

“Jukata tunamuunga mkono Rais Magufuli tumepanga kupitia maandamano yetu tufikishe pongezi na kumwomba aongeze kasi ili wabadhirifu bila kujali vyeo vyao wahukumiwe,” alisema Mwakagenda na kuongeza.

“Tumeshapeleka barua ya maandamano haya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kwa wakuu wa polisi wa mikoa na wilaya kuwafahamisha njia yatakapopita,” alisema.