Julius Mtatiro afunguka kuanza majukumu u-DC

20Jul 2019
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe
Julius Mtatiro afunguka kuanza majukumu u-DC

MKUU mpya wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro, ameomba ushirikiano kwa viongozi wenzake katika kuiongoza wilaya hiyo ili kufanikisha kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

MKUU mpya wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro.

Alitoa ombi hilo jana baada ya kula kiapo kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, mjini Songea.

Mtatiro alisema nafasi aliyopewa ni kubwa, hivyo inahitajika uongozi wa ushirikishwaji ili kufanikisha kutatua changamoto zinazowakabili wanachi.

Mtatiro alimshukuru Rais John Magufuli kwa kumteua kushika nafasi hiyo ambayo ilikuwa inashikiliwa na Juma Homera, ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

“Namshukuru Rais John Magufuli kwa kuniona kuwa ninafaa kumsaidia katika kazi ya ukuu wa wilaya …na mimi namuahidi kuwa nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote ili mwisho wa siku Rais aone kuwa hakukosea kuniteua,” alisema Mtatiro ambaye akiwahi kuwa mmoja wa viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kujiondoa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, wakati akiitisha zoezi hilo la kuapisha alimtaka mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, kwenda kufanya kazi za Wananchi kama Rais alivyomtuma.

“Kwa upande wake RC Mndeme alimweleza Mtatiro kuwa: “Katika uteuzi watu wengi wanaweza kukupongeza na wengine wakajenga chuki na wewe bila sababu za msingi, hivyo kikubwa ni kuwatumikia wananchi kwa kufuata miongozo inayotakiwa ikiwamo kufuata maadili.”

Habari Kubwa