Jumuiya ya Kihindu kuwezesha watoto 30 kutibiwa moyo

17May 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jumuiya ya Kihindu kuwezesha watoto 30 kutibiwa moyo

Jumuia ya Kihindu Tanzania (BAPS) imetoa kiasi cha shilingi milioni 68 fedha ambazo ziatumika kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto wenye matatizo hayo  hapa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akisalimiana na kaimu kiongozi wa Jumuia ya Kihindu Duniani (BAPS) Mtukufu Bhaktipriyadas Swami alipotembelea Tanzania hivi karibuni.

Fedha hizo ambazo   zitatumika kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto 30 wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) zimetolewa hivi karibuni na Kaimu Kiongozi wa Dunia wa Jumuia hiyo.

Akizungumza kuhusu msaada huo Kaimu kiongozi wa Jumuia ya Kihindu Duniani, Mtukutu Bhaktipriyadas  Swami alisema wametoa fedha hizo kwa ajili ya kusaidia jamii yenye uhitaji hasa watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi alishukuru kwa msaada huo na kusema kuwa fedha zilizotolewa zitatumika kwa walengwa ambao ni watoto wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Prof. Janabi alisema kuwa Taasisi hiyo imekuwa na  uhusiano mzuri na Jumuia ya BAPS ambao kila mwaka wamekuwa wakichangia fedha kwaajili ya matibabu ya moyo kwa watoto ambao baada ya matibabu wamepona na wengine wamerudi shuleni kuendelea  na masomo yao.

Tangu mwaka 2016 BAPS wamekuwa wakitoa fedha kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto ambapo hadi sasa jumla ya watoto 290 wameshafanyiwa upasuaji. 

Habari Kubwa