Jumuiya Burunge hifadhi inayojiendesha kwa mtindo wa serikali

10Jul 2020
Salome Kitomari
BABATI
Nipashe
Jumuiya Burunge hifadhi inayojiendesha kwa mtindo wa serikali
  • Ijue inakoelekea na ‘figisu’ zake

JANA katika sehemu ya tatu ya mfululizo wa taarifa zinazohusu Jumuiya ya Hifadhi za Jamii (WMA) Burunge, kulikuwa na ufafanuzi wa kina unaohusu ilivyoasisiwa, nyendo zake kiuchumi na namna ilivyoguswa na pigo la corona kama ilivyo kwenye maeneo mengine ya kiuchumi na kijamii nchini.

Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya Burunge, Benson Maise (katikati), akifafanua jambo kwa mwandishi wa habari, Salome Kitomari.
Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Emmanuela William. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Meneja Msaidizi wa Hoteli ya Burunge Tinted, Jackline Macha, anataja sababu za kuwekeza kwenye eneo hilo ni mvuto lilionao kitalii, mandhari yanatoa ushuhuda wa moja kwa moja kwa wanyama wanapokuwa katika nyendo zao, eneo jirani na hoteli, pia Ziwa Burunge.

Anasema katika hoteli yenye jumla ya vyumba 38, huwa wanapokea wageni kutoka mataifa mbalimbali, akinyambua takwimu zao kwamba katika msimu usio wa utalii, huwa ni wastani wa wageni 30 hadi 50 hotelini na msimu wa utalii hupokea wastani wa wageni 120.

Kwa mujibu wa Macha, mbali na wageni wanaofikia hotelini, wengine huishi kwenye mahema ndani ya mandhari ya kitalii, mfumo unaotumiwa pia kupendwa sana na watalii katika sehemu nyingi.

Macha aliiambia Nipashe hivi karibuni kuwa, mpango mkakati wao wa kimasoko ulitikiswa na mlipuko wa maradhi ya corona, kwa mpango wao kuwapokea kundi la wageni tangu Aprili iliyopita, lakini wakaangukia mbadala wa kufunga hoteli kwa muda, hatua iliyoenda sambamba na wafanyakazi 40 kupewa likizo.

Katika mazungumzo yake na Nipashe, wakati taifa likiwa kwenye mlipuko wa corona, Macha alifafanua: “Kwa sasa (wakati huo) tumebaki (wafanyakazi) saba kwa ajili ya usafi, ni kutokana na hali ya biashara. Tunatarajia kupokea wageni wengi Julai mwishoni na wafanyakazi wote watarudishwa kazini.”

Pia, katika kuhami mazingira ya hifadhi yawe rafiki kwa wanyama ambao ndiyo mvuto wa utalii, meneja huyo anasema wanashirikiana kulinda mazingira ikiwamo kuondoa mifugo inayoingia hifadhini kwa kuwa uzoefu wao unaonyesha wanyama hupakimbia mahali walipo wakiwaona binadamu.

MAUAJI KWENYE USHOROBA

Kimsingi, unapotaja ushoroba, maana yake halisi ni mapito ya wanyama kutoka eneo moja kwenda lingine. Hiyo kiasilia hutumiwa na wanyama ama kuzaliana au kutafuta madini maalum ya miili yao.

Katika eneo hilo kuna Hifadhi za Taifa Ziwa Manyara na Tarangire, zinazounganisha eneo hilo linaloendelea hadi kwenye Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Hifadhi za Serengeti na Masai Mara, iliyoko katika nchi jirani ya Kenya.

Benson Maise, Katibu wa Jumuiya hiyo, anafafanua kuwa, matumizi ya shoroba yametambuliwa na eneo hilo ndani ya WMA linalindwa kwa ushirikiano na vijiji wadau, kwa utaratibu wa watuhumiwa waharibifu kupelekwa vijijini kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zao ndogo.

Hata hivyo, Maise anakiri kuwapo kwa vikwazo kutoka barabara kuu ya Arusha-Babati, inayokatiza eneo hilo, akirejea utafiti unaoonyesha kuwapo kwa idadi kubwa ya wanyama wanaouawa kwa kugongwa na magari.

Anafafanua wanavyokusanya takwimu kwa kutumia pikipiki maalum, taarifa zikionyesha kila siku wanyama wanakufa. Anaendelea: “Wanyama wanauawa hasa katika eneo la ushoroba kuanzia Makuyuni hadi Kibao cha Tembo.

Wengine wanagongwa wakubwa kama twiga.” Wakati Maise akishauri Wakala wa Barabara (TANROADS) kuweka alama kwenye eneo hilo tajwa, Mtafiti wa Wanyamapori wa Mradi wa Simba, Dk. Benard Kissui, anasema kipindi kati ya Januari na Desemba mwaka jana, wanyamapori 380 walikufa kwa kugongwa na magari katika eneo hilo la ushoroba.

MIKASA YA UJANGILI

Dk. Kissui anasema kuwa hadi kufikia nusu ya kwanza ya mwaka huu, kulikuwa na watuhumiwa 28 wa ujangili na kati yao, 27 walihukumiwa. Pia, kulikuwapo kesi mbili zilizofutwa na tisa zinaendelea kusikilizwa.

Maise anafafanua kuhusu vikwazo wanavyokumbana navyo katika udhibiti wa ujangili unaofanywa kwa lengo la kuua wanyama kwa ajili ya kitoweo, kuwa ni nyendo za watu na tabia zao.

Anafafanua namna wanavyokabili tatizo hilo, akitamka: “Tunashirikisha jamii ipasavyo kuhakikisha wanaelewa na imefika mahali wananchi wanaelewa wanyama ni mali yao na wanawalinda na kutoa taarifa.”

Katibu huyo anatoa simulizi ya mfano wa mkasa wa ujangili uliowatokea Aprili 21 mwaka huu, watu wasiojulikana walipowapeleka pundamilia 11 na mtoto wa twiga hadi liliko Ziwa Manyara na kisha wakawachoma mikuki. “Pundamilia huwa haingii kwenye maji.

Walichofanya, waliwalazimisha kuingia na wakawachoma wakafa. Tulifanikiwa kuchukua mabaki ambayo tunatarajia kutengeneza sehemu ya kumbukumbu, ili itumike kutoa elimu kwa vizazi,” anasema Maise, akifafanua walikamatwa watuhumiwa 17 na kati yao, sita wana kesi ya kuhujumu uchumi.

MIFUGO VS WATU

Maise anakiri kuwapo tishio la ongezeko la mifugo na watu, linalochangia kilimo na malisho ya mifugo kuvamia eneo la hifadhi inayozaa mivutano ya kisheria kuhusu haki stahiki.

Diwani wa Mwada, Gerald Chembe, anasema mgogoro wa mazao kuliwa na mifugo na wanyamapori upo, huku akitaja kikwazo cha kisheria wanyama kama pundamilia kutoingizwa kwenye orodha ya wanaolipwa fidia. “Imefikia mahali simba anaingia kwenye boma anakula ng’ombe.

Kwa msimu huu, kuna watu mahindi yameliwa na pundamilia, ila kwa mujibu wa sheria, hawana fidia,” anasema.

HUJUMA KWA ASKARI

Mbali na msuguano wa hujuma za kiuchumi na kijamii kati ya wanyama na binadamu, wakazi jirani, walinda usalama askari nao wana malalamiko katika eneo hilo.

Diwani Chembe anasema, Baraza la Maliasili Babati, liliamua wavamizi wa eneo oevu waondolewe na askari walipokwenda kutekeleza amri hiyo inayokaidiwa, baadhi yao walihudhuriwa kwa mikuki, akigusia tukio mojawapo la Machi mwaka huu.

Pia, anakumbusha tukio lingine la mwezi uliofuata Aprili mwaka huu, askari walipothubutu kuwaondoa waliovamia hifadhini, baadhi walipata madhara makubwa. Katibu wa jumuiya hiyo, Maise, anasema mbinu wanayotumia wenyeji hao kutoka jamii za kifugaji, ni kujiunda kwa mfano wa kikosi kazi dhidi ya askari wanaothubutu kutetea mali za hifadhi.

“Uamuzi ulikuwa wavamizi kuondoka kwenye ardhi oevu iliyotolewa na vijiji vingine… vijiji ambao eneo lao lilivamiwa na kuharibiwa, vilinyimwa mgao na mwaka 2018 walipata nusu ya mgao,” anasema.

BURUNGE INAKOELEKEA

Makamu Mwenyekiti wa Burunge WMA, Emmanuela Willium, anasema mpango mkakati wa baadaye ni kutengeneza eneo la utalii katika Mlima wa Oridoi, ili mgeni akiwa juu alione pia eneo lote la WMA.

Anasema kuwa pia watatengeneza kambi za kulala wageni ambazo zitamilikiwa na WMA nje ya zile za wawekezaji waliopo kwa sasa.

Willium pia anadokeza mpango wa kuanzisha shughuli za utalii kama vile mbio za mitumbwi kwenye Ziwa Manyara na Burunge ili kuongeza mapato zaidi.

Habari Kubwa