Jumuiya yaipongeza Tanzania kwa amani

28Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Jumuiya yaipongeza Tanzania kwa amani

WATANZANIA wamepongezwa kwa kuwa kisiwa cha amani kulikozifanya nchi nyingine barani Afrika kuitolea mfano na kuja kujifunza amani.

Kwa msingi huo, Watanzania wametakiwa kuidumisha, kuienzi, kutunza na kuithamini amani hiyo ambayo ndicho kitu chenye thamani zaidi duniani kuliko kitu kingine chochote.

Pongezi na wito huo ulitolewa na Kiongozi Mkuu wa Bara la Afrika wa Jumuiya ya Kiroho ya Brahma Kumaris, Raja Yoga Meditation Centre, Brahma Kumaris Sister Vedanti, katika ziara yake kuitembelea Tanzania, na kusema amani ya Tanzania inaigiwa mfano kuleta amani katika bara zima la Afrika.

Sister Vedanti, alisema amani ndicho kitu chenye thamani kubwa zaidi katika dunia hii, kwa sababu mahali pasipo na amani, hakuna maendeleo, hakuna maelewano, hakuna masikilizano, vita, fujo, machafuko, umaskini ni matunda ya ukosefu wa amani.

Akielezea kuhusu Jumuiya hiyo ya Brahma Kumaris Raja Yoga Meditation Centre, ni jumuiya ya kiimani, inayohubiri amani duniani kote, lakini ili dunia iwe ni kisiwa cha amani, lazima amani hiyo aianzie ndani ya moyo wa kila mtu, hivyo wanawafundisha watu kujitambua na kujitafakari kwa njia ya mazoezi yanayoitwa Raja Yoga, na kufanya meditation, kila mtu akiwa na amani, familia zitakuwa na amani, jumuiya zitakuwa na amani, nchi zitakuwa na amani na dunia nzima itakuwa na amani.

Akizungumzia kazi za jumuiya hiyo nchini, Mratibu wa Brahma Kumaris nchini, Brahma Kumaris Sista Lalita, alisema wamefungua vituo vya mafunzo ya Yoga na Meditation katika mikoa kumi nchini katika Jiji la Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza, Shinyanga, Moshi, Arusha, Tabora, Singida, Dodoma, Lindi na Morogoro.

Sista Lalita alisema jumuiya hiyo ni jumuiya ya kujitolea, na mafunzo hayo ya Yoga na Meditation, ni kwa ajili ya watu wa dini zote na mafunzo katika vituo hivyo hutolewa bure.

Jumuiya hiyo ya Brahma Kumaris ilianzishwa mwaka 1937 nchini India, na imesambaa katika mataifa 110. Kazi yake kubwa ni kuhamasisha maendeleo kupitia katika amani na utulivu na viongozi wake wote ni wanawake waliojitoa maisha yao yote kutumika kuleta amani ulimwenguni.

Habari Kubwa