Kabendera, serikali wamalizana

25Feb 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kabendera, serikali wamalizana

MWANDISHI wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera, amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kulipa faini na fidia ya Sh. milioni 273 baada ya kukiri makosa yaliyokuwa yakimkabili, likiwamo la kutakatisha fedha na kukwepa kodi.

Vilevile, mahakama hiyo imemhukumu Kabendera kulipa faini ya Sh. 250,000 au kwenda jela kutumikia kifungo cha miezi mitatu baada ya kukiri kosa la kukwepa kodi.

Mshtakiwa tayari ameshalipa Sh. milioni 100, faini ya Sh. 250,000 na mahakama imemtaka kulipa Sh. milioni 173 ndani ya miezi sita kuanzia jana kwa mujibu wa makubaliano yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Hukumu hiyo ilisomwa jana na mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega, aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo.
Mshtakiwa aliingia makubaliano na DPP kuomba msamaha na kukiri mashtaka yaliyokuwa yanamkabili.

Awali, upande wa mashtaka ulimfutia shtaka la kuongoza genge la uhalifu na kumsomea mashtaka ya kutakatisha fedha na kukwepa kodi.

Hakimu Mtega alisema katika kosa la kwanza la ukwepaji kodi, mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh. 250,000 au kifungo cha miezi mitatu jela. Pia atatakiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 173.

Alisema katika kosa la pili la utakatishaji fedha, mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 100 na kusisitiza kuwa adhabu hizo zinajitegemea, hivyo kila adhabu itakwenda peke yake.

Kabendera alilipa faini ya Sh. 250,000 na anatakiwa kulipa Sh. milioni 273 ambazo tayari ametanguliza malipo ya Sh. milioni 100, akitakiwa kumaliza Sh. milioni 173 ndani ya miezi sita kuanzia jana.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai mtuhumiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma, hivyo aliiomba mahakama itoe adhabu kulingana na makubaliano yaliyofanyika.

Wakili wa Mshtakiwa, Jebra Kambole, alidai kukiri makosa yake kumeipunguzia muda mahakama kuendesha mashtaka, ana familia na ndugu wanaomtegemea na pia ni zaidi ya miezi sita sasa amekaa mahabusu.

Alidai hali ya mshtakiwa kiafya si nzuri na akaomba katika kosa la kwanza alipe faini ya Sh. 250,000 kwa mujibu wa Sheria ya Kodi na alipe faini kwa kosa la pili pia.

Akisoma makubaliano ya mshtakiwa huyo na DPP, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai wameingia makubaliano na mshtakiwa huyo baada ya kukiri kosa la utakatishaji fedha na ukwepaji kodi, hivyo DPP ameamua kumwondolea kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Baada ya kusoma makubaliano hayo, Hakimu Mtega alimwapisha mshtakiwa na kumuuliza kama alitia saini kwa hiari yake na kudai alifanya hivyo kwa hiari yake.

Akisoma maelezo ya awali, Wakili Nchimbi alisema kati ya Januari Mosi 2010 na Julai 29, 2019, mshtakiwa alijihusisha na genge la uhalifu kwa kuingia mikataba isiyo halali na watu wengine ambao wapo nje ya Tanzania, wakiwamo watu maarufu ambao hawakuwa mahakamani.

Alidai mshtakiwa alikubali kufanya makosa ikiwa ni pamoja na kughushi, kukwepa kodi na utakatishaji fedha ambayo yanachangia kudidimiza uchumi.

Nchimbi alidai Machi 23, 2010 kampuni ya Kabendera iliyosajiliwa kama Voxy Media Center (T) Ltd na Wakala wa Usajili (Brela) na Januari 11, 2016, mshtakiwa pamoja na mkewe, Loy Kabendera, walisajili Kampuni ya Sitrep Company Limited na katika usajili huo, walighushi fomu mbalimbali na kuonyesha ofisi ya kampuni hiyo inapatikana kwenye nyumba namba 13 kitalu namba 23 Mbweni Mpiji Kinondoni ambayo ni nyumba yao ya kuishi.

Alidai mshtakiwa huyo pia katika mkakati wake wa kiuhalifu, alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kwa lengo la kuidanganya serikali na kujipatia fedha kwa njia ya uhalifu.

Nchimbi alidai Aprili 2, 2016, mshtakiwa huyo pamoja na mkewe walifungua akaunti mbili za fedha katika benki ya CRDB, moja ikiwa ya fedha za kigeni, pia mshtakiwa alifungua akaunti yake binafsi.

Alidai Januari Mosi, 2015 alipokea Dola za Marekani 230,358.83 kutoka kwa washtakiwa wenzake kupitia akaunti yake binafsi ambazo zilitoka kwa watu mbalimbali ikiwamo Kampuni ya K2 Intelligence Ltd, Palladium (Tanzania) Ltd, Sitrep Co. Ltd, Eurasia Group Ltd, International Crisis Rou na taasisi zingine za kigeni.

Nchimbi alidai Januari Mosi 2015 na Agosti 29, 2019, mshtakiwa na mkewe Loy, wakiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Sitrep, walipokea Dola za Marekani 432,000,541 na Paundi 119,000,130 na katika kipindi chote hicho hawakuwahi kulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Wakili huyo alidai mshtakiwa aliwaambia maofisa wa Jeshi la Polisi kuwa hajapokea fedha zozote kinyume cha taratibu kutoka katika vyanzo visivyo halali.

Pia, alidai mshtakiwa huyo alikataa kutoa taarifa zozote za benki na kampuni ya Sitrep.

Nchimbi alidai uchunguzi wa awali ulionyesha mshtakiwa huyo alijihusisha na shughuli za kihalifu na kufuatia uchunguzi huo, alifunguliwa mashtaka mbele ya mahakama hiyo ambayo baadaye alikiri kuyafanya.

Akisoma mashtaka mapya, Wakili Simon alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi 2015 na Agosti 29 2019, Kabendera alikwepa kodi ya Sh. 173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe TRA.

Katika shtaka la pili, Kabendera alidaiwa kutakatisha Sh. 173,247047.02 huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la ukwepaji kodi.

AZUNGUMZIA MAISHA YA MAHABUSU

Saa 9:47, Kabendera alipoachiwa rasmi kutoka mahabusu ya Mahakama ya Kisutu baada ya kukamilisha taratibu za mahakama hiyo, alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa baada ya kutoka mahabusu alikoishi miezi saba, jana ameanza rasmi kuomboleza kifo cha mama yake mzazi.

"Leo nimeanza rasmi kuomboleza kifo cha mama yangu mzazi, nawashukuru wanataaluma wenzangu, Watanzania wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kuhakikisha anazikwa na kupumzishwa kwenye nyumba yake," alisema Kabendera.

Alisema anakusudia kumtafuta mmoja baada ya mwingine waliofanikisha safari yake ya mwisho ya mama yake.

Akizungumzia Jeshi la Magereza, Kabendera alisema analishukuru jeshi hilo kwa jinsi walivyomhudumia alipoingia gerezani alikuwa mgonjwa sana, lakini wamempa huduma tofauti na alivyokuwa akiwafikiria.

"Ninawashukuru sana wanataaluma, ndugu na marafiki zangu kwa kuwa pamoja na mimi katika kipindi kigumu nilichowahitaji kuliko wakati wote," alisema.

Habari Kubwa