Kabudi atetea kauli ya JPM corona kimataifa

24May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kabudi atetea kauli ya JPM corona kimataifa

TANZANIA imeitaka dunia na Jumuiya za Kimataifa kutambua kuwa kauli ya Rais John Magufuli kuwahimiza Watanzania kusali na kuliombea Taifa kuondokana na maradhi ya Covid -19 haikuwa kauli ya kupuuza kanuni za kisayansi za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi:PICHA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE

Akitoa salamu za shukrani kwa Mungu na Watanzania kwa niaba ya Rais Magufuli ikiwa ni hitimisho la siku tatu za kumshukuru Mungu baada ya maambukizo ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu Covid -19 kupungua nchini katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano Dayososi ya Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema licha ya kauli ya Rais kutaka Watanzania kusali bado serikali ilisisitiza kufuatwa kwa kanuni za kisayansi za kuepuka maambukizo ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Aliongeza kuwa hatua ya Tanzania kufunga maabara yake iliyokuwa ikipima virusi vya corona hapo awali kabla ya Rais Magufuli kubaini kasoro katika maabara kuu, hatua hiyo iliifanya Tanzania kuchukua hatua ya kujijengea uwezo wake wa ndani na kujenga maabara mpya yenye uwezo wa kuwapima watu wanaodhaniwa kuwa na virusi vya corona maradufu.

Prof. Kabudi alisema kupitia kwa waumini wa kanisa hilo, alisema Rais Magufuli anashukurani kubwa sana kwa Mwenyezi Mungu na kwa Watanzania wote kwa kuitikia wito wake wa wananchi kuondokana na hofu na badala yake wamlilie Mungu, jambo ambalo maombi hayo yamejibiwa kwa kupungua maambukizo licha ya uwapo wa ubashiri juu ya idadi ya watakaoathirika na kufariki dunia kwa maradhi ya Covid-19 kufikia 100,000 kwa Tanzania pekee.

Akizungumza wakati wa mahubiri Canon Francis Xavery kwa upande wake, alimshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kutofunga nyumba za ibada, yakiwamo makanisa na misikiti licha ya mashinikizo kutoka sehemu mbalimbali, jambo lilimfanya Mwenyezi Mungu kusikia maombi ya Watanzania kwa kuwa walimwamini Mungu.

Padri Jacob Kahemele wa Kanisa la Kuu la Mtakatifu Albano Dayosisi ya Dar es Salaam, alisema kanisa hilo limeungana na waamini nchini kote kuitikia rai ya Rais, huku akiwataka Watanzania kuacha kujipa hofu hususani katika mambo ambayo yanapita upeo wa binadamu na badala yake kila mmoja kwa imani yake kujinyenyekeza mbele ya Mungu ambaye ni suluhisho la mambo yote yanayoonekana na yasiyoonekana.

Habari Kubwa