Kabudi, Gavana wakaliwa kooni

15May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Kabudi, Gavana wakaliwa kooni

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imewataka viongozi wote walioshiriki kutia saini makubaliano na Kampuni ya Indo Power ya Kenya kwa ajili ya ununuzi wa korosho kujiuzulu kutokana na kuisababishia serikali hasara kubwa kwa uamuzi huo.

Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma jana hotuba kuhusu makadirio ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka ujao wa fedha, Cecil Mwambe, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Anthony Komu, alisema uamuzi huo umeisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani milioni 500 (Sh. trilioni 1.1).

Waziri kivuli huyo alilieleza Bunge kuwa Juni, mwaka jana, serikali ilizindua awamu ya pili ya mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo ambao unatekelezwa kwa miaka 10 ambao malengo yake ni pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji na kufanya kilimo kiwe cha kibiashara.

Hata hivyo, wakati serikali ikifanya hivyo, Mwambe aliliambia Bunge kuwa mapema mwaka huu, serikali kupitia Bodi ya Nafaka Mchanganyiko (CPB), iliingia makubaliano na kampuni hiyo ya Kenya kwa ajili ya ununuzi wa korosho tani 100,000 kwa bei ya Dola za Marekani milioni 180.2 (Sh. bilioni 418).

Alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mipango, mikakati na maelekezo ya serikali kuhusu korosho kushindwa kutekelezeka na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima wa zao hilo wanalolitegemea kama zao la biashara.

"Hata hivyo, miezi minne baadaye serikali imevunja mkataba na kampuni hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa kampuni hiyo kushindwa kutekeleza mkataba huo," alisema.

Mwambe alisema mkataba huo ambao serikali iliingia, ulitiwa saini mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria (kipindi hicho Prof. Palamagamba Kabudi), Naibu Waziri wa Kilimo, Dk. Innocent Bashungwa, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda.

Tukio la kutiwa saini kwa mkataba huo jijini Arusha Januari 30, pia lilishuhudiwa na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Florens Luoga, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu na makatibu wakuu wa wizara zinazohusika.

"Lakini tunaamini pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vina jukumu katika mikataba hii ambayo taifa linaingia. Taarifa za kwamba kampuni hii imeshindwa kutekeleza vifungu vya kimkataba inatia ukakasi kwa kuwa lilikuwa wajibu wa serikali kwa kutumia vyombo vyake kufanya uchunguzi wa kampuni hiyo.

"Haiingii akilini kwamba vyombo vyote walishindwa kujua uwezo wa kampuni husika. Ni kwa bahati mbaya haya yanatokea na mawaziri waliohusika wako ofisini utadhani hakuna kilichotokea

"Pamoja na udhaifu huo, matamko na maelekezo ya serikali kuhusu biashara ya zao la korosho yamesababisha hasara kubwa kwa wakulima na taifa kwa sababu ambazo zingeweza kuepukwa.

"Kutokana na sakata hili la korosho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka wahusika wote wajitafakari kama wanatosha kuendelea kushika nyadhifa walizo nazo ama wanapaswa kupisha ofisi hizo za umma kuongozwa na watu wengine kwa kuwa uamuzi wa CCM umelisababishia taifa hasara ya Sh. trilioni 1.18.

"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia inataka kufahamu ni gharama kiasi gani ambazo serikali ilitumia kukusanya zao hili la kibiashara kutoka kwa wakulima na kuzipeleka kwenye maghala ya serikali?

"Baada ya gharama zote zilizotumiwa na serikali, je, serikali ilitegemea kuuza korosho kwa bei gani? Mwambe alihoji.

Waziri Kivuli huyo pia alisema kambi yao inaishauri serikali kuboresha kwanza sekta ya kilimo na kujielekeza katika viwanda ambavyo vitaongeza thamani katika mazao ya mifugo kama vile maziwa, nyama, ngozi, damu, kwato, pembe na kusindika mazao yatokanayo na uvuvi.

Mwambe pia aliitaka serikali kuongeza bajeti ya wizara hiyo huku akiitaka ilieleze Bunge kiwango ambacho viwanda vyote vilivyopo nchini vinachangia kwenye Pato la Taifa.

Mwambe pia alisema bado wafanyabiashara wanakumbana na kadhia utitiri wa kodi na manyanyaso kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA).

Alisema kwa kipindi kirefu, TRA imeshindwa kubuni mkakati wa makusanyo ya kodi na badala yake wanatumia vibaya mamlaka katika kutekeleza majukumu na kusababisha malalamiko ya kuwapo vitendo vya rushwa.

Habari Kubwa