Kabudi: Hatuko tayari kudharauliwa kisa pesa

23Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kabudi: Hatuko tayari kudharauliwa kisa pesa

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania haitakubali kudharauliwa na taifa lolote kwa sababu ya misaada na pesa.

Amesema Tanzania iko tayari kuwasilikiza, kujadiliana na taifa lolote ambalo linadhani kuna upungufu umejitokeza.

Alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Nyerere ni kiongozi barani Afrika aliyefanya mambo makubwa kuliko mwingine yoyote. Aliwafukuza watalaam wa Kijerumani na kuwarudishia fedha yao yote Deutsch Mark milioni 35.

“Kati ya pesa na heshima ya nchi yetu, tutasimamia heshima ya nchi yetu, kati ya misaada na utu wetu tutasimamia utu wetu. Hatutakubali kutoheshimiwa na utu wetu kudharauliwa kwa sababu ya misaada na pesa,” alisema na kuongeza:

“Lakini tutashirikana na mataifa yote duniani ambayo yanatuheshimu kwamba sisi ni taifa huru, pamoja na kutuheshimu sisi ni binadamu tulio sawa kama binadamu wengine.”

Prof. Kabudi pia alisema uvumi kuwa yako mataifa yanatishia kutokutoa msaada kwa Tanzania hauwezi kuliyumbisha taifa.

Siku zote, alisema Tanzania iko imara na kwa hiyo haiwezi kukubali kupewa misaada ya aina yoyote ambayo mwisho wake si mwema kwa tamaduni na mila za taifa.

“Nayasema haya si kwa bahati mbaya, kuweni imara, fanyeni kazi kwa nidhamu kama ilivyo kwa wenzetu wa China, lakini ninyi na baadhi ya Watanzania wenzetu vikiwamo baadhi ya vyombo vya habari, naona mnashabikia mabaya tu. Hebu tangazeni mema ya nchi kwanza,” alisema Prof. Kabudi.

Alisema uchaguzi uliofanyika hivi karibuni uliioonyesha dunia kuwa, Tanzania ni nchi ya namna gani.

Alisema kuna watu wakiwamo watumishi wa Wizara wameanza kutikisika baada ya kutishiwa kuhusu kuondolewa kwa misaada jambo ambalo kwake anaona halina maana.

Akizungumzia uchaguzi mkuu, alisema kuna mataifa makubwa yamefanya uchaguzi kwa njia ya posta lakini wameanza kuwaletea shida, lakini Tanzania imefanya uchaguzi wakati wa ugonjwa wa corona kwa mazingira ya amani, utulivu, huru, haki na uwazi jambo linalosababisha wengi kuitamani.

Habari Kubwa