Kachero adai Sabaya alimpiga, kumsababishia maumivu diwani

05Aug 2021
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Kachero adai Sabaya alimpiga, kumsababishia maumivu diwani

MKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Arusha, Mratibu Msaidizi Gwakisa Minga, amedai kwamba kipigo alichopata Bakari Msangi kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza kilimsababishia maumivu makali.

Minga (45) amedai hayo leo alipokuwa akiendelea kutoa ushahidi wake kwa upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, na wenzake wawili.

Mbali na Ole Sabaya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya unyang’anyi wa kutumia silaha ni Sylvester Nyegu (26) na Daniel Mbura (38).

Shahidi huyo pia alidai Sabaya na walinzi wake,  walimpiga, kumteka nyara, kumtishia kumuuwa na kumpora Sh.390,000 wakati wakifanya uhalifu  katika duka la Mohamed Saad. 

Alidai kuwa Msangi wakati akihojiwa na polisi alikuwa akitokwa na damu sehemu za masikioni, ndipo walipobaini uhalifu uliofanywa na Sabaya na walinzi wenzake. Pia, alidai msangi ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo, alitambuliwa kuwa alipigwa kwa kuwa alikuwa na alama za kupigwa usoni na kwenye mashavu na alikuwa akitokwa na damu masikioni.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdalah Chavula, Minga alidai kwamba baada ya kujiridhisha kuwa amefanyiwa vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria, alitoa taarifa kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha.

"Baada ya kutoa taarifa kwa OCD na RCO, walinipa maelezo kuwa nimjulishe aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kennan Kihongosi, kuwa watuhumiwa hawa hawakuwa na makosa baada ya kuwahoji,” alidai.

Baada ya kutoa taarifa hizo kwa Kihongosi, Sabaya na Nyegu walifika tena kituoni na kuwaeleza kwamba, baada ya kuwahoji alibaini kuwa Msangi na wenzake hawakuwa na kosa lolote.

"Baada ya hapo tukiwa polisi, Sabaya alimwagiza mshtakiwa wa pili kwenda kwenye gari kuchukua simu  za watuhumiwa na  aliwakabidhi mbele yangu. Taratibu za kukabidhiana simu zilipokamilika, Sabaya aliondoka kituoni bila ya kupekuliwa wala kukamatwa kwa kuwa alikuwa na mamlaka ya uteuzi, hivyo kiutaratibu upelelezi unapokamilika tunauwasilisha kwenye mamlaka iliyomteua,” alidai.

"Pia baada ya kumaliza mahojiano nilitoa agizo vijana wale wasindikizwe hadi nyumbani kwao, kwa kuwa walikuwa na hofu sana," aliongeza kudai.

Minga aliendelea kudai kuwa baada ya tukio hilo, uchunguzi ulianza ili kuthibitisha ukweli na wakati akiendelea na majukumu yake, Februari 10, mwaka huu, saa 6:00 usiku, alipigiwa simu na OCD, akampe maelekezo ya kufika haraka kituo cha polisi kwa kuwa yupo na Msangi amepigwa na kuporwa. 

"Nilipofika kituoni nilimkuta OCD. Muda si mrefu alifika Msangi akiwa ameambatana na mke wake, alikuwa na mikwaruzo na alama za kupigwa kwenye sehemu za usoni na mashavuni na alikuwa anatokwa na damu masikioni.

"Kutokana na hali ya Bakari ilivyokuwa mbaya, nilitoa maelekezo aandike maelezo yake haraka na baada ya hapo, alipewa fomu namba tatu ya Polisi (PF3) na nilimsindikiza hadi Hospitali ya Mount Meru, kwenda kupatiwa matibabu,” alidai.

Shahidi huyo alitoa PF3 hiyo mahakamani kama kielelezo cha ushahidi kwa kuwa Msangi aliitumia kwenye matibabu yake.

Pia, alidai kuwa Februari 12 mwaka huu, majira ya saa 10:00 jioni, walikwenda kukagua duka lililovamiwa katika mtaa wa Bondeni, jijini Arusha.

"Tulipofika kwenye duka tulikuta  limefungwa na Numan alifungua  na  alitueleza  kuwa tangu kutokea kwa uvamizi hawakuwa wamelifungua na tulipoingia ndani tulikuta vitu vimevurugwa kwa kutupwatupwa shagalabagala na kulikuwa na matone ya damu, majimaji na tulipoangalia duka lilikuwa na CCTV kamera.

"Na tulipochunguza vizuri tulibaini kuna CCTV camera nne, lakini zilikuwa zimechezewa kwa kugeuzwa, ili zisirekodi matukio yanayoendea kule ndani dukani huku kamera mbili zilielekezwa ukutani kwa kugeuzwa, ili zisirekodi vizuri matukio kwenye kona inayotakiwa,” alidai shahidi huyo.

Akihojiwa na wakili wa utetezi wa mshtakiwa wa kwanza, Mosses Mahuna, shahidi huyo alidai kwamba hakuna kosa la jinai linaweza kupelelezwa, ndani ya Wilaya ya Arusha bila yeye kujulishwa.

Wakili huyo alimuuliza shahidi jalada la uchunguzi wa kesi hiyo lilifunguliwa wakati gani na kudai kwamba halikuwa jalada la uchunguzi  na namba za jalada alizozitaja  si za kweli kwa kuwa uchunguzi ulishaanza muda baada ya Msangi kutoa malalamiko yake polisi.