Kada CCM amwangukia Magufuli katiba mpya

11Mar 2017
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Kada CCM amwangukia Magufuli katiba mpya

MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanawake na Katiba (Ulingo), Anna Abdallah, amemuomba Rais John Magufuli kurejesha mchakato wa upatikanaji Katiba Mpya, ili madai na haki za wanawake, ikiwamo usawa wa kijinsia yaingizwe katika katiba na kuwa sheria.

Mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali katika serikali ukiwamo ubunge, ukuu wa wilaya, ukuu wa mkoa na uwaziri pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema mambo yote mazuri yanayohusu wanawake lazima yapatikane kupitia Katiba mpya.

Anna ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), alisema bila katiba hiyo, madai hayo yataendelea kuzungumzwa katika majukwaa, mikutano na makongano, bila ya kuchukuliwa hatua za kuleta mabadiliko.

Rais Magufuli alitoa msimamo wake kuhusu katiba mpya, wakati akizungumza na vyombo vya habari nchini mwishoni mwa mwaka jana, na kusema kwamba katiba mpya si kipaumbele kwa sasa, bali ni muda wa kuinyoosha nchi.

Anna aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye kongamano la wanawake na uzinduzi wa kitabu cha ‘Nguvu Zetu, Sauti Zetu’ kilichoandaliwa na Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake (WFT).

Aliongeza kuwa masuala 12 muhimu ambayo yamependekezwa kuingizwa katika katiba mpya, ikiwamo utu wa mwanamke, kubatilisha sheria kandamizi, haki ya kupata huduma za msingi, kama afya, elimu, maji, uzazi salama pamoja na haki ya kumiliki rasilimali.

Masuala mengine ni haki za watoto wa kike, kuwapo kwa tume ya kusimamia haki za wanawake na wenye ulemavu na mahakama ya familia, yanahitaji kuingizwa katika katiba hiyo.

”Uhalalishwaji wa matendo ya ukatili hasa ndoa za utotoni kwa kisingizio cha mila, tamaduni hakikubaliki, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inakinzana na Sheria ya Kujamiiana ya Mwaka 1998, katiba ya sasa inatambua kila raia ana haki sawa, lakini wakati huo huo inaruhusu mila hizi, tunahitaji katiba mpya,” alisema.

Awali, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema safari waliyoianza wanawake na hatua waliyoifikia sasa kuhusu haki zao ni somo kwa nchi.

Alisema inapofika suala la mambo ya kitaifa nguvu ya pamoja bila kujali itikadi za vyama inahitajika, ili kuleta ufumbuzi.

Jaji Warioba alisema kitabu hicho kilichoandaliwa na asasi 65 nchini, ambazo kila moja ina ajenda na mtazamo wake, ni mfano wa kuigwa na viongozi nchini.

“Viongozi wengine waige mfano huu, milikaa meza moja na kujadili hoja za msingi kuhusu wanawake wa nchi nzima,” alisema.

Alitoa tahadhari kwa viongozi, wataalamu wa masuala ya kilimo na hali ya hewa kuendelea kutoa elimu kuhusu dalili za upungufu wa chakula nchini, ili wazitumie mvua zilizopo kuzalisha chakula cha kutosha.

Habari Kubwa