Kadi mtoto mwenye betri yaagizwa Afrika Kusini

09Aug 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Kadi mtoto mwenye betri yaagizwa Afrika Kusini

KADI ya kumtambulisha Happiness John (5) kimataifa baada ya kufanyiwa upasuaji na kuwekewa betri ndani ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), inatengenezwa nchini Afrika Kusini, imeelezwa.

Happiness ambaye alifanyiwa upasuaji huo Julai 15 na kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo wiki moja iliyopita, anatakiwa kuwa na kadi tambulishi ambayo itamuwezesha kutofanyiwa ukaguzi wa kielektroniki.

Kwa sasa mtoto huyo amepewa kadi ya muda ambayo inamruhusu kutopita katika maeneo yenye mionzi kwa ajili ya ukaguzi, ikiwamo viwanja vya ndege na majengo yenye ulinzi mkali.

Kupatikana kwa kadi hiyo kutoka Afrika Kusini kutamuwezesha Happiness, mkazi wa Arusha, kupita bila kukaguliwa kielektroniki duniani kote.

Ofisa Uhusiano wa JKCI, Maulid Mohammed aliiambia Nipashe kuwa kadi hiyo imeagizwa nchini humo na kwamba kadi anayotumia hivi sasa ni ya muda.

“Atakaporejea baada ya miezi mitatu tangu aruhusiwe (Novemba), Happiness atahitajika kutumia kadi maalum ya kimataifa ambayo inatambulika ili asiweze kupitishwa kutoka maeneo ya ukaguzi yanayotumia mionzi kama viwanja vya ndege,” alisema Maulid.

Kutokana na kuwapo kwa woga wa mashambulizi ya kigaidi, na hasa baada ya kuibuka kwa makundi kama IS na Al Qaeda barani Asia na Al Shabab na Boko Haram kwa Afrika, maeneo mengi yamekuwa na ulinzi wa kielektroniki kwa ajili ya kukagua silaha na mabomu.

Ni jambo la kawaida kukuta mitambo hiyo katika viwanja vya ndege, mahoteli na majengo nyeti.

Happiness alifanyiwa upasuaji huo ili kuongeza kasi ya mapigo ya moyo wake kutoka 20-60 kwa dakika alipokuwa mgonjwa mpaka kati ya 60-80, ambayo ni ya kawaida ya binadamu, sasa.

Aidha, wakati akiruhusiwa, mama yake alikabidhiwa CD ambayo ina maelekezo kwa daktari ya cha kufanya endapo atapata matatizo madogo madogo akiwa nyumbani kabla ya kurudi tena JKCI.

MASHARTI MAGUMU

Akizungumza na Nipashe muda mfupi kabla ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, mama mzazi wa Happiness, Elitruda Malley alisema mtoto huyo hatakiwi kuchezea sumaku.

“Sumaku ambazo watoto huwa wanachezea nazo hazitakiwi kuwa jirani nae, hivyo usimamizi wa karibu kwa Happiness unahitaji umakini zaidi,” alisema Elitruda.

Aidha, mama huyo alisema mwanawe hatakiwi kuishi karibu na minara ya simu.

Maeneo mengi ya makazi ya watu nchini yamezingirwa na minara ya kampuni tano kubwa za mawasiliano ya simu za mkononi, hata hivyo, ambazo karibu zote zinamiliki binafsi miundombinu hiyo.

Elitruda alisema Happiness kwa sasa anahitaji uangalizi wa hali ya juu kutokana na betri ya moyo kuongoza mapigo ya moyo wake kuhitaji umakini mkubwa.

Aidha, Elitruda alisema ameshauriwa kumuangalia kwa karibu anapokuwa nyumbani na kuwa naye makini na aina ya michezo anayocheza na watoto wenzake.

“Kabla sijaruhusiwa, daktari amesema nitapewa maelekezo (zaidi) ya namna ya kumuangalia kwa makini mwanangu kwa kuwa bado ni mdogo,” alisema Elitruda.

“(Madaktari wamesema) pale anapocheza na watoto wenzake wanaweza wakamkanyaga kifuani kwa bahati mbaya na kuhatarisha afya yake.

“Hata namna walivyoweka kifaa hicho, haihitaji kuishi jirani na maeneo yaliyo na minara au kupita eneo lenye mionzi kwa sababu programu inaweza ikajibadilisha mfumo wake.”

Licha ya masharti hayo magumu kulingana na umri wa mwanawe, Elitruda alisema anamshukuru Mungu na anafurahi kuona afya ya mtoto wake inaimarika baada ya upasuaji.

Habari Kubwa