Kakobe acharuka

28Jan 2019
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Kakobe acharuka

MKUU wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Askofu Zachary Kakobe, ameeleza kuchukizwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya wanasiasa aliodai kuwatukana viongozi wa dini kwenye mitandao ya kijamii.

MKUU wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Askofu Zachary Kakobe

Amedai wanasiasa wote waliowatukana viongozi wa dini baada ya kufanyika kikao kati yao na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, wanapaswa kutubu, vinginevyo “wataanguka kwenye shimo refu na hawatainuka tena".

Askofu Kakobe aliyasema hayo jana wakati wa ibada iliyofanyika kwenye kanisa hilo jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa kumekuwa na lugha za matusi zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa dhidi ya viongozi wa dini.

Januari 23, mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na viongozi wa dini Ikulu jijini Dar es Salaam na kuwapa nafasi ya kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

”Viongozi wa siasa ambao wamewatukana viongozi wa dini kwenye mitandao ya kijamii, wanapaswa kutubu haraka sana, wakikaidi agizo hilo, chama chao kitatumbukia kwenye shimo refu ambao hakitainuka tena," alisema na kuongeza:

”Kuwatukana viongozi wa dini kwa sababu hawakuzungumza yale mliyotaka kuyasikia, ni utovu wa nidhamu, ni kiburi."

Askofu Kakobe alidai kuwa, baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Rais Magufuli na viongozi wa dini, kuna baadhi ya viongozi wa siasa, waliwatukana viongozi wa dini kupitia mitandao ya kijamii.

Alidai hajawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa nchini, ingawa amekuwa akialikwa kushiriki shughuli mbalimbali zinazoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wala ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Sijawahi kuwa mwanachama wa Chadema wala CCM," Askofu Kakobe alidai, "sina kadi ya vyama hivyo, sijawahi kuwasiliana na kiongozi yeyote wa Chadema wala kuonana nao ana kwa ana.

"Wala hawajawahi kuja ofisini kwangu, halijawahi kutokea. Naendelea kusisitiza kuwa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship halijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa. Hata Mbunge wa Jimbo ambalo Kanisa hili lipo, (Saed Kubenea - Chadema) sijawahi kuonana naye wala kuzungumza naye.”

Askofu Kakobe alidai aliwahi kuitikia mwaliko wa Chadema mara moja miaka michache iliyopita wakati wa mkutano uliofanyika Mlimani City, na alienda kama "baba anayeweza kualikwa na watoto".

Alidai kuwa wakati yuko kwenye mkutano huo, hakuzungumza na kiongozi yeyote wa chama na hakuwa na mawasiliano na kiongozi aliyekuwa anawania nafasi ya urais wakati huo.

“Leo (jana) ninanena waziwazi, kanisa langu siyo Chadema wala CCM, wala chama kinginge chochote, lakini waumi wake ni wanachama wa vyama hivyo vya siasa," Askofu Kakobe alisema.

Kiongozi huyo wa kiroho alidai kuwa wakati wa vuguvugu la katiba, aliwahi kwenda kwenye mkutano wa Chadema uliokuwa unafanyika kwenye Viwanja vya Jangwani jijini na alizungumza na John Mnyika (mmoja wa viongozi na wabunge wa Chadema) kwa simu kuhusu kuhudhuria mkutano huo, na aliitikia wito.

Askofu Kakobe alidai amewahi kuhudhuria mikutano mingi ya CCM kuliko Chadema wakati Yusuph Makamba alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na hakuwa na kadi ya CCM wala TANU. Alisema alikuwa anakwenda kwenye mikutano kutokana na uswahiba uliokuwapo kati yake na Makamba.

”Nakumbuka wakati mmoja niliwahi kuhudhuria mkutano wa wazee kumuaga Rais Benjamin Mkapa pale Diamond Jubilee, na nilialikwa na Yusuph Makamba. Wakati wa uongozi wake hapa Dar es Salaam, nilihudhuria mikutano mingi kwa sababu Makamba alikuwa rafiki yangu,” alidai Askofu Kakobe.

Kiongozi huyo wa kanisa alisema kuhudhuria kwake kwenye sherehe za kiserikali ambazo Rais Magufuli anakuwa mgeni rasmi, haimaanishi kuwa yeye ni mwanachama wa CCM, bali anaitikia wito anaoalikwa.

HATAKI UTEUZI

Askofu Kakobe alidai kuwa hata Rais Magufuli akimteua kushika nafasi ya uongozi ndani ya nchi, hawezi kukubali kwa kuwa ana kazi maalum ya kumtumikia Mungu.Alisema kuhudhuria kwake mikutano ya Rais Magufuli kumeibua mitazamo tofauti, wengine wakieleza amehaidiwa ubunge na wengine wakidai amenunuliwa.

”Siwezi kuwa mbunge wala waziri, na hata siku ikitokea nimeteuliwa na Rais, nitasema asante, lakini sitakubali," alisisitiza.

”Waumini wangu si mnajua nina pesa, si mnafahamu nilisema mimi ni tajiri kuliko serikali, si TRA wanajua walikuta fedha nzuri tu benki, si walikuta akiba nzuri katika akaunti ya kanisa, utaninunua kwa bei gani? Sina bei mimi,” Askofu Kakobe alitamba.

Alidai kuwa miaka 20 iliyopita, aliwahi kuwa na kadi ya Chama cha TLP kilichokuwa kinaongozwa na Augustine Mrema, na aliamua kukata kadi ya chama hicho "kwa uchokozi" ambao baada ya kuufanya, aliichama kadi hiyo mbele ya waandishi wa habari.

“Niliamua kuchukua kadi ya TLP kwa sababu CCM wakati ule ilikuwa inabagua makanisa ya Pentekoste, lakini kwa sasa Rais Magufuli siyo mbaguzi wa madhehebu wala dini, anawapenda watu wote," Askofu Kakobe alisema.

 

 

Habari Kubwa